Karate yamlilia Sensei Chikoko
Muktasari:
- Taarifa ya kifo hicho imetolewa na Shirikisho la Karate Tanzania (TSKF), ikieleza kuwa Chikoko alikuwa miongoni mwa walimu wa muda mrefu waliotoa mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza Karate nchini.
FAMILIA ya mchezo wa Karate nchini Tanzania, imeingiwa na simanzi kufuatia kifo cha mmoja wa walimu na viongozi wakongwe wa mchezo huo, Sensei Philip Kolowa Chikoko, aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo Agosti 31, 2026 nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya kifo hicho imetolewa na Shirikisho la Karate Tanzania (TSKF), ikieleza kuwa Chikoko alikuwa miongoni mwa walimu wa muda mrefu waliotoa mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza Karate nchini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Katibu Mkuu wa TSKF, Jerome G. Mhagama, familia ya Karate imepoteza mwalimu mwenye ujuzi, weledi na uzoefu mkubwa, ambaye kwa miaka mingi alihusika katika kuwafundisha na kuwaongoza makarateka mbalimbali nchini.
Mbali na kazi yake ya ualimu, Chikoko aliwahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya taasisi za Karate hapa nchini, akianza kwa kuwa Mwenyekiti wa Tanzania Shotokan Karate Association (TASHOKA), kisha kuwa Katibu Mkuu wa Tanzania Karate Federation (TKF).
Pia aliwahi kuwa kiongozi katika SKITZ, hatua inayodhihirisha nafasi kubwa aliyokuwa nayo katika maendeleo ya mchezo huo na namna alivyohusika katika uendeshaji wa shughuli za Karate nchini kwa kipindi kirefu.
Kifo chake kimeacha pengo kubwa si kwa familia yake pekee, bali pia kwa makarateka, wanafunzi na wadau wa mchezo huo waliokuwa wakinufaika na maarifa na uzoefu wake.
TSKF imesema Chikoko alikuwa zaidi ya mwalimu kwa wanafunzi wake, kwani aliishi nao na kuwafundisha kwa ukaribu, huku akitumia uzoefu wake katika kuwajenga kimchezo na kinidhamu.
Katika salamu zake za rambirambi, TSKF imetoa pole kwa familia ya marehemu, makarateka wote nchini, wanafunzi wake pamoja na wadau wa mchezo wa Karate kwa ujumla kutokana na msiba huo mkubwa.
“Familia ya Karate nchini imempoteza mmoja wa walimu wa siku nyingi mwenye ujuzi na weledi ulio wasaidia wengi,” imesema sehemu ya taarifa hiyo ya TSKF.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, Chikoko anatarajiwa kuzikwa Jumatano Septemba 2, 2026 katika makaburi ya Kinondoni Mwembe Jini jijini Dar es Salaam.