BWANGA: Nilikurupushwa wakati nauza kuku kwenda kuzichapa, sasa ni historia
Muktasari:
- Bwanga ambaye mpaka sasa hana jina lolote la utani ambalo limekuwa rasmi, lakini safari yake katika ngumi za kulipwa ilianza 2022.
SAID Bakari Bwanga ni mmoja kati mabondia wakali wakiwa ndani ya ulingo na tayari ameshajitengezea himaya yake katika mchezo wa ngumi za kulipwa nchini.
Bwanga ambaye mpaka sasa hana jina lolote la utani ambalo limekuwa rasmi, lakini safari yake katika ngumi za kulipwa ilianza 2022.
Bondia huyo ambaye alianza kwa rekodi ya ushindi kwa kumchapa Naimu Mtupa kwa pointi katika pambano la raundi nne, lakini akaja kupoteza dhidi ya Shaban Kimimbi kisha akaambulia sare na Hassan Kidebe, lakini alikuja kupigwa tena na Haidari Mchanjo mwaka huohuo.
Huenda 2022 ndiyo ulikuwa mwaka wa mwisho kwa Bwanga kuendelea kunyanyasika mbele ya mabondia wa ndani baada ya 2023 kupata nafasi ya kimazabe ya kupigana na Emmanuel Mwakyembe.
Kabla ya kupata nafasi ya kupigana na bondoa huyo, Mwakyembe alikuwa amepangiwa kupigana na mtu mwingine kabisa ambaye hakutokea siku ya kupima uzito na kusababisha akose mpinzani wa kupigana naye.
Lakini siku ya pambano ndipo alipatikana Bwanga yaani saa chache kabla ya pambano, akapandishwa bodaboda kutoka Mbagala hadi Ubungo Plaza na kilichotokea siku hiyo Mwakyembe hawezi kukisahau kwani alipokea upinzani mkali kwa bondia asiyekuwa na jina wala kujulikana na pona yake akaambulia sare.
Kuanzia hapo jina la Bwanga likaanza kuwa katika vinywa vya wadau wa ngumi na wengi wakitaka kujua ametokea wapi kutokana na uwezo alioonyesha kwenye pambano hilo ambalo hakuwa hata na maandalizi zaidi ya kukurupushwa.
Bwanga mpaka sasa kwenye rekodi yake amefikisha mapambano 12 akiwa ameshinda manane na kati ya hayo matatu akishinda kwa knockout, amepigwa mara mbili na kutoka sare mara mbili.
Bondia huyo ambaye ni namba moja kwenye uzani wa light hapa nchini wakati duniani akiwa wa 125 katika mabondia 2,639 na katika ‘pound for pound’ ya mabondia bora wa Tanzania anashika nafasi ya tisa huku akiwa na hadhi ya nyota mbili na nusu.
Mwanaspoti limepiga stori na bondia huyo ambaye anasema sababu kubwa ya kuwa mwanamasumbwi ni baba yake kutokana na kuona picha zake alipokuwa akicheza karate akiwa na mkanda mweusi na ndizo zilizomvutia kuingia katika michezo hiyo.
“Kitu cha kwanza kupenda au kunipa hamasa ya kuingia katika hii michezo ya mapigano ni baba yangu kwa sababu alikuwa anacheza karate na alikuwa na mkanda mweusi na hayo niliona kupitia picha zakem” anasema Bwanga.
“Lakini jambo lingine ambalo limechangia ni mambo ya uonevu wakati wa utoto. Sasa ikawa sababu ya kufanya (kupigana ngumi) ili watu waweze kuniheshimu.”
SWALI: Ngumi umeanza kujifunzia wapi?
JIBU: Ngumi nimeanza kujifunzia nyumbani. Baba yangu mzazi nilishawahi kushirikiana naye baadhi ya mazoezi kwa sababu alikuwa mtu wa ngumi. Zikaja ngumi za mtaani. Mtaani nilikuwa nafanya mazoezi mwenyewe nikakutana na mwalimu Ally Kisogo wa B Combination na wao ndiyo wamenipa msingi bora na kuanza kucheza mapambano na bado nipo nao hadi sasa.
SWALI: Umepigana sana kwenye ngumi za ridhaa mategemeo yalikuwa kitu gani kabla ya kuhamia kwenye ngumi za kulipwa?
JIBU: Katika ngumi za ridhaa sikuwahi kupigana kwa muda mrefu. Nilicheza mapambano matano nikaweza kufika hadi fainali nikapoteza na lengo la kucheza ngumi zile ilikuwa kujiweka fiti. Lakini baadaye yakaja mawazo naweza kupata ajira jeshini, lakini ukweli sikuweza kukaa kwa muda mrefu kwenye ngumi za ridhaa.
SWALI: Nini kimekuhamasisha kuingia kwenye ngumi za kulipwa kutoka kwenye ridhaa?
JIBU: Kwanza ni huo muda, kwenye ridhaa unapigana halafu hulipwi na mimi muda wangu ulikuwa mchache nikawa nakosa muda wa kwenda kushiriki mashindano ya ridhaa na hiyo ikanisukuma kwenda kwenye ngumi za kulipwa na mchezo ulishaingia kwenye damu.
SWALI: Ni kweli ulikuwa unategemea kupata ajira jeshini kupitia ngumi za ridhaa? Nini kimekwamisha?
JIBU: Unajua niliingia kwenye ngumi za ridhaa kwa lengo la kutaka kujiweka fiti na siyo kupata ajira jeshini, lakini malengo yalibadilika na kutaka kwenda jeshini baada ya kuona watu wengi wanafokasi huko, hivyo nikaingia kwenye huo mkumbo na kilichokwamisha ni kwa sababu sikuweza kushiriki sana ngumi za ridhaa.
SWALI: Familia yako imechukuliaje kuingia kwenye huu mchezo, hujakutana na vikwazo vyovyote?
JIBU: Mwanzoni wakati naanza hata familia yangu sikuwashirikisha. Nilianza tu mwenyewe mpaka nacheza ngumi za ridhaa. Nakumbuka nilikuwa namuaga mjomba wangu peke yake kwa sababu nilikuwa nafanya naye kazi na ndiye alikuwa anajua.
Lakini kwa upande wa familia walikuwa wanapokea stori kutoka kwa watu wengine na wakati mwingine nilivyokuwa nanusurika na matukio ya hatari ingawa kwa upande wa baba haikuwa changamoto sana kwa sababu alikuwa ni mtu wa michezo, ila upande wa mama kidogo ilikuwa shida kutokana na wengi wanatafsiri ngumi kama mchezo wa kihuni ingawa sasa wote wananipa sapoti.
SWALI: Pambano lililokufanya watu wakutambue ni ile dhidi ya Mwakyembe, ilikuwaje kupata nafasi na ulilipwa kiasi gani?
JIBU: Nakumbuka nilikuwa zangu sokoni nauza kuku wa nyama (broiler) wa mjomba wangu ambaye alikuwa kama amenijiari. Nilipokea simu majira ya saa tisa mchana kwamba kuna hilo pambano natakiwa kucheza siku hiyo.
Nilichouliza hilo pambano litakuwa linarushwa ‘live’ kwenye runinga? Nikaaambiwa ndiyo. Basi nikampigia mwalimu wangu na uzuri nilikuwa fiti nikasema acha nikajaribu bahati yangu. Binafsi sikutaka hata kujua nalipwa kiasi gani zaidi ya kutambua ni pambano la leoleo na pia nililipwa kati ya Sh300,000 hadi 400,000.
SWALI: Hivi ni kweli uliwahi kuwa unauza kuku wa kuchoma?
JIBU: Hapana nilikuwa nauza kuku wa nyama (broiler) ambao ni wazima siyo wa kuchoma yaani naenda kununua kwa wafugaji halafu napeleka sokoni kuuza.
SWALI: Nje ya ngumi unajishughulisha na nini kwa sasa?
JIBU: Kiukweli sijishughulishi na chochote zaidi ya ngumi na mazoezi kwa sababu huu mchezo unahitaji muda wa kutosha ingawa napambana ili niweze kuwa na vitega uchumi kwa sababu napenda, lakini hata nikiwa kama sipo vitasaidia.
SWALI: Kitu gani huwezi kusahau ambacho umekutana nacho kwenye ngumi?
JIBU: Daah! Siwezi kusahau sapraizi ya pambano la Mwakyembe kwa sababu siku ile ilikuwa siku kubwa, siku nzuri ambayo Mungu alifanya nifahamike na watu wengi, siku ambayo imenipa konekisheni nyingi na siku ambayo imenitoa kwenye ngumi na watu wengi wanikubali, sitaweza kusahau kwenye maisha yangu.
SWALI: Jambo gani unajutia sana kila unapokumbuka?
JIBU: Hakuna jambo ambalo najutia kwa sababu naamini kila jambo anayepanga ni Mungu. Kila kibaya kitakachotokea naamini kitakwisha. Kuna kupanda na kushuka na kuna kukereka na kufurahi, kikubwa ni kumuomba Mungu na vyote navitafsiri sawa.
SWALI: Mchezo wa ngumi unatajwa kuwa na mambo ya ushirikina vipi wewe umewahi kupata hiyo changamoto?
JIBU: Kiukweli hapana. kuumia ni kawaida kwa sababu unaweza ukawa unafanya mazoezi ukateleza ukaanguka. Siamini sana kwenye ushirikina naamini zaidi Mungu, naswali sana kumuomba Mungu wakati wote na hata kabla ya kwenda kupigana.