Kamungo: Kiingereza nimejifunzia YouTube
Muktasari:
- Kamungo anayekipiga FC Dallas ya Marekani, ambaye alikulia Tanzania katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu, anasema alipofika Marekani alikuta mazingira mapya kabisa huku lugha ikiwa miongoni mwa vitu vilivyompa wakati mgumu.
WAKATI wewe unapita zako YouTube kushangaa video za vichekesho na nyimbo za wasanii mbalimbali, Winga Mtanzania, Bernard Kamungo aliutumia mtandao huo kujifunza lugha.
Kamungo anayekipiga FC Dallas ya Marekani, ambaye alikulia Tanzania katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu, anasema alipofika Marekani alikuta mazingira mapya kabisa huku lugha ikiwa miongoni mwa vitu vilivyompa wakati mgumu.
Wakati huo alikuwa akifahamu Kiswahili na Kifaransa tu lakini Kiingereza kilikuwa lugha ngeni kwake.
"Lugha ninazozijua ni Kiswahili kwa sababu niliishi Tanzania kwenye Kambi ya Nyarugusu na Kifaransa kwa sababu baba yangu anatokea DR Congo. Nilikuwa napata tabu, lakini nilijifunza Kiingereza," amesema Kamungo.
Changamoto hiyo ilifanya aanze kutafuta njia nyingine njia ambazo zingemsaidia kuendana na mazingira mapya. Miongoni mwa njia alizotumia ni kujifunza kupitia mitandao ya kijamii, hasa YouTube, ambayo kwake ikawa sehemu muhimu ya kuongeza uelewa wa lugha.
"Pia, nimekulia kwenye mazingira ambayo wazungu ni wengi hivyo kuzungumza nao na kujifunza kulinisaidia kuijua lugha hiyo."
Winga huyo amejumuishwa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa, Taifa Stars chini ya kocha Miguel Gamondi kwa ajili ya maandalizi ya mechi mbili za kuwania kufuzu Afcon 2027.
Nyota huyo mzaliwa wa Congo aliyekulia katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu, Tanzania maisha yake ya soka amekulia Marekani akitumikia klabu ya North Texas (2021/22) ya Ligi Daraja la Tatu ambako kwenye mechi 52 alifunga mabao 22.
Kamungo amecheza jumla ya dakika 1,230 katika mechi 16 alizoitumikia FC Dallas msimu huu. Mchezaji huyo mwenye asili ya Tanzania ameweka rekodi mpya ya msimu kwa kufikisha asisti nne.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 alisaini mkataba mpya na FC Dallas Januari 7, 2025, utakaomuweka klabuni hapo hadi mwisho wa msimu wa 2027, huku klabu ikiwa na chaguo la kumuongezea mkataba hadi 2028 na 2029.
FC Dallas imekuwa na rekodi ya kushinda nane, sare moja na kupoteza nne katika michezo ambayo Kamungo ameanza kwenye kikosi cha kwanza.