Kabaddi yaacha alama, yaomba sapoti
Muktasari:
- Mbali na mafanikio hayo, walinzi wawili wa Tanzania, Hafidh Ali na Massoud Omary, waliingia katika orodha ya walinzi watano bora wa mashindano, huku mwamuzi Ramadhan Mrisho akipata nafasi ya kuchezesha michezo ya nusu fainali na fainali.
LICHA ya Timu ya Kabaddi ya Tanzania kwa wanaume kushindwa kutwaa ubingwa wa Michuano ya Jumuiya ya Madola, imeonyesha kiwango kizuri huku baadhi ya wachezaji na mwamuzi kutoka nchini ni miongoni mwa waliofanya vyema.
Mshambuliaji Juma Sultan aliibuka mfungaji bora wa timu hiyo baada ya kukusanya pointi 80 katika mashindano hayo.
Mbali na mafanikio hayo, walinzi wawili wa Tanzania, Hafidh Ali na Massoud Omary, waliingia katika orodha ya walinzi watano bora wa mashindano, huku mwamuzi Ramadhan Mrisho akipata nafasi ya kuchezesha michezo ya nusu fainali na fainali.
Michuano hiyo ya Commonwealth Kabaddi Championship, iliyohusisha wanaume na wanawake, ilifanyika Uwanja wa Veer Savarkar nchini India kuanzia Oktoba 21 hadi 30, 2026.
Nchi 13 zilishiriki mashindano hayo, zikiwemo Tanzania, Nigeria, Australia, Bangladesh, Scotland, Canada, Singapore, Sri Lanka, Malaysia, Kenya, Uganda, England na wenyeji India.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Msaidizi wa Shirikisho la Kabaddi Zanzibar, Ramadhan Mrisho, amesema Tanzania haikuwa na uzoefu mkubwa wa mashindano ya kiwango hicho, lakini iliipeperusha vyema bendera ya nchi.
Mrisho amesema timu hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya maandalizi kutokana na mchezo wa Kabaddi kutopata kipaumbele cha kutosha.
Amesema licha ya kutokuwa na maandalizi bora, wachezaji walipambana na kuonyesha kiwango kizuri katika mechi walizocheza.
“Sehemu tuliyofeli ni maandalizi. Tumeshindwa hata kuiweka timu kambini kwa sababu hatukuwa na fedha, kwani wadau bado hawajaupa kipaumbele mchezo huu,” amesema Mrisho.
Amesema ushiriki katika mashindano hayo umewapa uzoefu mkubwa kuliko walivyokuwa nao awali, hivyo wanaahidi kujiimarisha ili kufanya vizuri zaidi katika mashindano yajayo.