Jeshi la Simba lilivyovamia Bunju
Msemaji wa Klabu ya Simba, Asha Muhaji akifafanua jambo mbele ya wanachama waliotembelea eneo la uwanja wao uliopo Bunju B, Dar es Salaam jana Jumapili. Picha na Mwanahiba Richard
Muktasari:
Kamwaga katika moja ya vipaumbele vyake Simba ni ujenzi kwenye uwanja huo na ameanzisha kitu kinachoitwa ‘Operesheni Bunju’.
JANA Jumapili wanachama na viongozi wa Klabu ya Simba wakiongozwa na Katibu Mkuu Ezekiel Kamwaga na Ofisa Habari, Asha Muhaji walikwenda kujionea eneo la uwanja wao lililopo Bunju B, Dar es Salaam.
Kamwaga katika moja ya vipaumbele vyake Simba ni ujenzi kwenye uwanja huo na ameanzisha kitu kinachoitwa ‘Operesheni Bunju’.
Eneo hilo lina ukubwa wa ekari 25 ambazo zinaonekana kama zimetelekezwa kutokana na viongozi wa Simba kutotembelea wala kuweka alama zozote zinazoonyesha kuwa eneo hilo lina mmiliki, hata hivyo Simba hawakuweza kufanya hivyo kwa sababu lilikuwa halijalipiwa.
Mpaka sasa Simba imelipa Sh70 milioni na kubakiwa na deni la Sh 20 milioni kati ya Sh91 milioni ambazo zilikuwa ni fedha za jumla baada ya kupunguziwa kutoka Sh103 milioni, wakimaliza deni hilo Serikali itawapa hati ya kumiliki uwanja huo.
Msafara wa wanachama hao ulianzia Makao Makuu ya Klabu ya Simba mtaa wa Msimbazi Kariakoo, saa 2 asubuhi ukiwa na watu 36 wakitumia usafiri wa gari la klabu yao aina ya Toyota Coster huku wakionekana wana shauku kubwa ya kulifahamu eneo lao.
Wanachama hao walifika katika eneo hilo saa 4 asubuhi lengo likiwa ni kujionea eneo hilo baada ya Mwanaspoti kuandika kwa mara ya kwanza makala tatu mfululizo jinsi eneo hilo lilivyotelekezwa.
Wanachama mbalimbali kutoka matawi ya Simba ya Mpira na Maendeleo, Tawi la Wailes, Mpira Pesa, Tawi la Tegeta, Makao Makuu na Tawi la Bunju walianza kuzungukia eneo hilo huku baadhi yao wakionekana kutokuwa wageni wa eneo hilo na ndio waliokuwa wakiwaongoza wenzao.
Wanachama hao walilipongeza Mwanaspoti huku wakitamka kuwa isingekuwa kuandikwa kwa habari ya eneo hilo kwenye gazeti hili basi huenda viongozi hawakuwa na mawazo ya kuwapeleka huko, wengine walitamka maneno hayo bila kujua kama mwandishi wa gazeti hili yupo kwenye msafara huo.
Wanachama walijionea nyumba zilizokuwa zimejengwa ndani ya eneo lao ingawa tayari zilibomolewa baada ya kupewa tahadhari kuwa eneo hili linamilikiwa na Simba, pia walijionea mifugo; ng’ombe na mbuzi wakiwemo eneo hilo ambalo limegeuka kuwa malisho yao.
Baada ya kumaliza zoezi la kuzunguka mipaka ya eneo hilo, wanachama,viongozi na mashabiki wa Simba walifanya jaribio la kufyeka baadhi ya vichaka vilivyomo ndani ya uwanja huo.
Mohamed Mashango ambaye ni Katibu wa Vijana wa Simba Tanzania anasema: “Tunashukuru Gazeti la Mwanaspoti kwa kuwafumbua macho viongozi wetu hadi wameamua kutuleta huku ili tujionee wenyewe maana tulikuwa tunasimuliwa tu kuwa kuna uwanja.”
“Naamini utata juu ya uwanja huu utakuwa umemalizika, kitakachofuata ni kufanya vitendo, hii ni kwa kushirikiana na viongozi na wanachama wenyewe, deni lililobaki limalizwe ili tupewe hatimiliki,” anasema Mashango.
Mwanachama Ally Suru yeye anasema: “Viongozi mnatakiwa kufanya jambo litakalowawezesha kukusanya fedha ili kuanza hatua za mwanzo za kuuweka uwanja huu katika hali ya kueleweka. Tumeliona eneo na sasa iwe mipango ya kuhakikisha tunapata fedha za kumalizia deni, watu wa ardhi waje wapime ili tujue mpaka wetu ni upi.”
Kauli hiyo iliungwa mkono na wanachama wote walioonekana kubishana kwenye mpaka kutokana na nyumba moja ambayo inadaiwa kujengwa ndani ya eneo la Simba huku wengine wakidai kuwa ipo nje ya eneo hilo.
Wanachama wengine waliotoa mawazo ni Karim Boimanda (Mwenyekiti wa Vijana wa Simba Tanzania), Amina Moyo, Abubakari Mwinchande na Rakhim Rashid ambao kwa pamoja walikubaliana kuanza utekelezaji wa kuutengeneza uwanja huo kwa hatua za mwanzo.
Kamwaga, anasema kuwa hiyo ni hatua ya kwanza ambayo wamekubaliana na wanachama wao kuwa waangalie eneo hilo ndipo hatua nyingine zifuate.
“Tunapata mawazo mbalimbali kutoka kwa wanachama wetu, kama tulivyosema kuna wengine walikuwa hawalifahamu eneo hili na hii ndiyo mara yao ya kwanza, tumekubaliana kwa pamoja kwani nao wameridhishwa na kufurahishwa na jambo hili.
“Baada ya wiki mbili tutarudi tena tukiwa na wanachama zaidi ya hawa, kwa wakati huo tutakuja kikazi, tutaleta gari la kusawazisha ‘greda’ na vifaa vingine vitakavyotusaidia kufyeka ili kuliweka eneo safi, tunataka tusawazishe ili tupande nyasi za kawaida tutaweka na magoli.
“Mambo ya nyasi bandia yatakuja baadaye kwani hiyo ni hatua ya mbele zaidi, naamini hatua ya mwanzo itafanikiwa kwani hata wanachama wenyewe wana nia na uwanja wao na wanapenda kuona upo katika hali nzuri, utafikia hatua ya kufanyiwa mazoezi hata siku moja moja,” anasema Kamwaga.
Kamwaga anasema kuwa Sh20 milioni ni lazima zipatikane haraka ili wamalizie deni kwani mambo mengine yanapaswa kufanyika ndani ya miezi minne ijayo na kudai kuwa serikali imewaruhusu kufanya mambo mengine ambayo ni ya hatua za mwanzo ikiwemo kuzungushia uzio.
“Simba haiwezi kukosa Sh20 milioni kwa kipindi tulichokusudia, tutatafuta mpaka zipatikane kikubwa tutachotaka ni kuwa na hatimiliki kwani hata ukienda benki kukopa wanataka tuwape hati ya uwanja ndiyo tupewe mkopo, hivyo ni jambo la kulifanyia kazi haraka,” anasema Kamwaga.
Asha Muhaji naye alikuwa na haya: “Hili suala linawezekana kama alivyosema katibu wangu, wanachama wamejionea wenyewe na utekelezaji ndiyo unaofuata, nafikiri kwa kipindi tulichopanga kitakuwa ni kizuri kukamilisha jambo hili.
“Hili si suala la viongozi pekee bali ni letu wote na wanachama, hivyo siku tutakapokuja huku kwa ajili ya kazi tunawaomba wanachama wote wajitokeze, tunaamini wanachama wetu wana mapenzi na klabu yao, tukiliweka sawa tutalizungushia uzio eneo hili,” anasema Asha.
Safari yetu ya kuufuatilia uwanja wa Simba imeishia hapa na sasa tunasubiri utekelezaji kutoka kwa viongozi wa klabu hiyo kwani wameonyesha nia lakini wasiishie njiani watekeleza kile waliochokiahidi kwa muda waliojiwekea.
Hadithi na vitendawili vya miaka mingi tunaamini kwa sasa zimepata ufumbuzi kwa viongozi wa Simba na wanachama wao na mabadiliko yataonekana.