Jangwani giza, halafu mwanga tena
Muktasari:
MABINGWA wa soka nchini, Yanga wapo hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa inakabiliwa na mtihani mgumu wa kusaka kuweka rekodi ya kucheza nusu fainali.
MABINGWA wa soka nchini, Yanga wapo hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa inakabiliwa na mtihani mgumu wa kusaka kuweka rekodi ya kucheza nusu fainali.
Wawakilishi hao wa Tanzania na Afrika Mashariki wiki ijayo itakuwa na kibarua kigumu mbele ya Wakongo, TP Mazembe katika mchezo wao wa pili, baada ya kuanza vibaya ugenini nchini Algeria kwa kulala 1-0 dhidi ya MO Bejaia.
Mchezo huo wa Yanga na TP Mazembe utapigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na vijana wa Jangwani inahitajika kushinda ili kujiwekea mazingira mazuri kwa mechi zake zijazo za Kundi A lenye timu ya Medeama ya Ghana.
Tofauti na wao, wapinzani wao yaani Mazembe walianza vyema mechi zake za kundi hilo kwa kuilaza Medeama kwa mabao 3-1 na kuipa uongozi wa kundi, kitu ambacho kwa Yanga ni mitihani kwelikweli wa staili ya ‘kuuma jongoo kwa meno’.
Mechi hiyo ijayo ya Yanga ndiyo itakayotoa uelekeo wa kundi hilo ili kujua ni timu zipi zitajiweka katika mazingira mazuri ya kuingia nusu fainali baada ya kila timu kucheza mechi sita zikiwemo tatu za nyumbani na tatu za ugenini.
Yanga lazima ishinde
Ndiyo, katika mechi hii ni lazima itafune jongoo kwa meno kwani ni ushindi pekee utakaofufua matumaini yao ya kufika nusu fainali ya michuano hiyo kutoka kundi hilo.
Pamoja na kwamba soka halitabiriki na lolote linaweza kutokea, lakini hali halisi ni kwamba kama Yanga haikupata ushindi mbele ya Mazembe wiki ijayo itakuwa na maana ya kujiwekea mazingira magumu ya kufika hatua ya nusu fainali.
Katika mashindano ya mechi sita ukipoteza mechi mbili mfululizo ni dhahiri kwamba, unajiweka katika mazingira ambayo unategemea zaidi kudra za Mungu kusonga mbele kuliko hali halisi ya matokeo ya hali ya mchezo.
Wapinzani wako wakiwa na pointi sita mkononi na wewe ukiwa huna pointi hata moja na kila moja imebakisha mechi nne ni mazingira magumu ambayo yanahitaji miujiza kuweza kuibuka mshindi wa nafasi mbili za juu katika kundi.
Katika mazingira hayo Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm na msaidizi wake, Juma Mwambusi pamoja na wachezaji wafanye kazi kubwa na kupaswa kutuliza akili kama wanataka kuweka hai matumaini ya kusonga mbele.
Siyo kazi ya mchezo kwani inahitaji juhudi za ziada kuwabwaga TP Mazembe ambao mara kadhaa wameshaonja ladha ya kuwa Mabingwa wa Afrika.
Katika mechi hii Yanga haina njia ya mkato isipokuwa kupata ushindi na iwapo itapata sare ni jambo lisilofurahisha, lakini ikitokea kama itafungwa ni jambo la kuhuzunisha.
Ikifungwa katika mechi hiyo Yanga itakuwa na mlima mrefu kuupanda kwani italazimika kushinda mechi zote nne zilizobaki zikiwemo mbili za nyumbani na mbili za ugenini.
Hata hivyo, Mazembe kama ikishinda Dar es Salama itakuwa vigumu kufungwa nyumbani kwao katika mechi ya marudiano kwa hiyo kupunguza idadi ya mechi ambazo inatakiwa ipate ushindi na kubaki tatu ambazo ikishinda zote itafikisha pointi tisa.
Hata hivyo, hayo ni mahesabu ya kufikirika na siyo lazima yatokee kweli kwa hiyo Yanga hawana mbadala kama wanataka kuweka hai matumaini yao ya kusonga mbele ni lazima waitoe na kilio Mazembe Uwanja wa Taifa.
Kwa uzoefu wangu wa soka kwa miaka mingi sioni dalili iwapo Yanga itakubali kufungwa na Mazembe na baadae ikapata nafasi ya kuingia nusu fainali ya Afrika.
Mazembe sio wa kubeza
Pamoja na kwamba Mazembe imetolewa na kushindwa kuingia katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu, lakini siyo timu ya kubezwa ama kuidharau kwa kudhani ni dhaifu.
Mazembe mwaka huu ilizidiwa ujanja na kujikuta ikitolewa Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini bado ni timu ngumu na yenye uwezo mkubwa.
Kuondoka kwa mshambuliaji wa Tanzania, Mbwana Samatta na kwenda Genk ya Ubelgiji hakujapunguza ukali wa timu hiyo ambayo imekuwa tishio Afrika kwa kipindi cha miaka ya karibuni.
Kwa hiyo Yanga isiweke mawazo kwamba Mazembe ya sasa ni dhaifu kuliko ile ya Samatta bali wajiandae kwa upinzani mkali ambao itakumbana nao.
Kwa hiyo Yanga inatakiwa ijiandae kikamilifu ili kupambana na hatimaye kuibuka na ushindi katika mechi hiyo ambayo umuhimu wake ni mkubwa kuliko mechi nyingine zote za Kombe la Shirikisho.
Mechi hiyo itakuwa ni ya umuhimu kwa vile ndiyo mechi ambayo itatoa dira ya uelekeo wa Yanga katika mechi nne zilizobaki.
Uzalendo usiwashinde
Kuna msemo katika soka kuwa mchezaji wa 12 ni mashabiki wanaofika uwanjani kuishangilia timu.
Katika mazingira ya kawaida kwa vile Yanga inacheza kwenye uwanja wa nyumbani ilipaswa ipate ushangiliaji mkubwa zaidi kuliko wapinzani wao TP Mazembe.
Hata hivyo, katika mazingira ya Dar es Salaam, Yanga itaingia uwanjani ikiwa na idadi ya washangiliaji karibu sawa na wa Mazembe kwani, kwa kawaida ilivyozoeleka mashabiki wote wa Simba wataiunga mkono wageni hao.
Hili limekuwa donda ndugu ambalo limekuwa likitafutiwa dawa kwa miaka mingi ili kuliondoa, lakini imeshindikana na linaendelea kuitafuna soka la Tanzania.
Katika miaka ya karibuni ilifanyika kampeni kubwa iliyoshirikisha vyombo vya habari la kuondoa tatizo hilo mwaka 1992 wakati Yanga ilipocheza na Ismailia ya Misri katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
Juhudi hizo zilionekana kutaka kuzaa matunda pale Yanga walipoingia uwanjani na mashabiki wa Simba kuanza kuishangilia na wale walioshindwa wakaamua kubaki kimya bila ya kuwazomea.
Hata hivyo, mambo yalitibuka baada ya Yanga kufungwa bao la kwanza katika mchezo huo waliofungwa 2-0 baada ya mashabiki wa Simba kulipuka kwenye jukwaa lao kama vile wameambizana huku wakiimba “Uzalendo umetushinda”.
Kuanzia hapo, ikawa kweli uzalendo ukawashinda Simba na wakaanza kuishangilia Ismailia kama vile timu yao ya nyumbani ndiyo inayocheza dhidi ya Yanga.
Kibao kiligeuka mwaka 1993 wakati mashabiki wa Yanga walipoombwa kuibeba Simba kwa kuishangilia ilipocheza na Stella Abidjan ya Ivory Coast katika mechi ya Fainali ya Kombe la CAF.
Mechi ilipoanza mashabiki wa Yanga walitulia bila kuizomea Simba, lakini mambo yaliharibika pale Stella ilipopata bao la kwanza katika mechi hiyo iliyoshinda 2-0 na mashabiki wa Yanga kama walivyofanya Simba mwaka 1992 walilipuka wakiimba “Uzalendo umetushinda”.
Ni vizuri sasa mashabiki wa timu hizi zenye upinzani na utani wa jadi kufungua ukurasa mpya na kuungana kuwa kitu kimoja ili kuhakikisha timu za Tanzania zinapata ushindi kwa faida ya Taifa.
Kuwapa Mazembe faida ya ushangiliaji wa karibu ya nusu ya watazamaji watakaoingia Uwanja wa Taifa ni hasara kubwa kwa Taifa kwani, kutaiongezea nguvu timu hiyo kutoka DR Congo.
Ni wazi kwamba TP Mazembe itakuja na mashabiki wake wa kuishangilia wakiwa na ngoma zao kubwa, lakini kama mashabiki wote wa Tanzania wataungana na kuwa kitu kimoja hawatafua dafu mbele yao.
Kwa hiyo kama vile Yanga inavyotakiwa kutafuna jongoo kwa meno ili iishinde Mazembe basi na mashabiki wa Simba nao watafune Jongoo kwa meno kuwashangilia watani wao. Inawezekana kwa vile ukarimu huanzia nyumbani.
Masoud Sanani ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi amewahi kufanya kazi Televisheni Zanzibar,Uhuru na Mzalendo,Bussiness Times[Mhariri mwanzilishi wa Spoti Starehe] na Mwananchi.Alikuwa mkurugenzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania[TEF].Anapatikana kwa email [email protected] simu 0712-020020