Jamus yatibua hesabu Simba, Singida BS zikiaga CECAFA Kagame
Muktasari:
- Matokeo hayo yameifanya Simba kumaliza hatua ya makundi ikiwa na pointi tano katika Kundi B, nyuma ya Jamus FC ya Sudan Kusini iliyofikisha pointi saba baada ya kuichapa Mogadishu City mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kigali Pele.
LICHA ya Ibrahim Doumbia na Elie Mpanzu kuifungia mabao Simba, Wekundu hao wa Msimbazi wameshindwa kuendelea na safari nusu fainali ya Kombe la CECAFA Kagame licha ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars.
Matokeo hayo yameifanya Simba kumaliza hatua ya makundi ikiwa na pointi tano katika Kundi B, nyuma ya Jamus FC ya Sudan Kusini iliyofikisha pointi saba baada ya kuichapa Mogadishu City mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kigali Pele.
Hivyo, Simba na mabingwa watetezi Singida Black Stars wameaga mashindano hayo kwa pamoja.
Akihitaji ushindi ili kuongeza nafasi ya kutinga hatua inayofuata, kocha Steve Barker alifanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake ikilinganishwa na mechi mbili zilizopita dhidi ya Mogadishu City na Jamus.
Mahamadou Kassaly alirejea langoni huku Nickson Kibabage, Ismael Toure, Rushine De Reuck na David Kameta 'Duchu' wakiongoza safu ya ulinzi.
Katikati walikuwepo Yusuph Kagoma na Keletso Makgalwa, wakati Clatous Chama, Anicet Oura na Libasse Guaye wakicheza nyuma ya Doumbia aliyeongoza safu ya ushambuliaji.
Kwa upande wa Singida Black Stars, Muhibu Kanu hakubadili kwa kiasi kikubwa kikosi kilichoichapa Mogadishu City mabao 4-1 huku Mathew Tegisi na Henry David wakiendelea kuaminiwa kuanza.
Dakika za mwanzo zilikuwa za ushindani mkubwa huku timu zote zikicheza kwa tahadhari lakini Simba ilionekana kuwa na utulivu zaidi katika kumiliki mpira na kutengeneza nafasi.
Baada ya kucheza dakika 180 bila kufunga bao katika mashindano hayo, Simba hatimaye ilivunja ukame huo dakika ya 21 kupitia Doumbia aliyefunga kwa kichwa.
Bao hilo liliwapa Wekundu wa Msimbazi kujiamini zaidi na kutawala sehemu kubwa ya mchezo huku Singida ikitafuta kwa nguvu bao la kusawazisha kabla ya mapumziko bila mafanikio.
Singida ilirejea kipindi cha pili ikiwa na kasi mpya na juhudi zake zilizaa matunda dakika ya 50 baada ya Mathew Tegisi kuisawazishia timu hiyo huku ikiwa ni bao lake la tatu katika mashindano hayo.
Barker alifanya mabadiliko ya haraka akiwaingiza Elie Mpanzu, Bakari Msimu na Ibraheem Jabaar badala ya Doumbia, Libasse Guaye na Keletso Makgalwa, hatua iliyoongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji.
Dakika ya 66, mabadiliko hayo yalizaa matunda baada ya Mpanzu kufunga bao la pili lililoipa Simba ushindi muhimu.
Hata hivyo, ushindi huo haukutosha kuiokoa Simba baada ya Jamus kushinda mchezo wake dhidi ya Mogadishu City na kutinga nusu fainali kama kinara wa kundi.
Simba ilimaliza nafasi ya pili ikiwa na pointi tano, Singida Black Stars ikawa ya tatu kwa pointi tatu huku Mogadishu City ikiburuza mkia kwa pointi moja.