Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jamani! Kulikoni Yanga, Azam zote kuanzia nyumbani

Muktasari:

SIMBA ya Dar es Salaam iliweka historia kwa kuwa timu ya kwanza Tanzania kuitupa nje timu ya Misri katika michuano ya Klabu za Afrika na kuingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

SIMBA ya Dar es Salaam iliweka historia kwa kuwa timu ya kwanza Tanzania kuitupa nje timu ya Misri katika michuano ya Klabu za Afrika na kuingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Timu hiyo ya Tanzania iliweka rekodi hiyo mwaka 2003 kwa kuitoa Zamalek ya Misri kwa mikwaju ya penalti baada ya timu hizo kwenda sare ya bao 1-1 baada ya Simba kushinda bao 1-0 nyumbani na timu hiyo ya Misri kushinda nyumbani kwao.

Kabla ya hapo, Simba ilikuwa inazifunga timu za Misri, lakini ilikuwa haijapata nafasi ya kuzitoa katika mashindano na mara zote Simba ndiyo ilikuwa ikitupwa nje kwenye mashindano hayo.

Wakati tunakumbuka historia hiyo ya Simba, timu mbili za Tanzania, Yanga na Azam zote za Dar es Salaam zina mtihani wa kupambana na timu kutoka Arabuni katika michuano ya Afrika.

Yanga itakumbana na Al-ahly katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika na Azam itapambana na Esperance ya Tunisia katika michuano ya Kombe la Shirikisho ikiwa ni hatua ya pili baaya ya Yanga kuitupa APR ya Rwanda na Azam kuitoa Bidvest Wit ya Afrika Kusini.

 

WANABEBWA

Historia inaonyesha kuwa kila timu za Tanzania zinapopangiwa kucheza na timu za Afrika ya Kaskazini katika michuano ya Klabu Barani Afrika ni lazima zianze mechi ya kwanza nyumbani.

Katika historia yangu ya uandishi wa habari za michezo kwa miaka kadhaa sijawahi kuona timu ya Tanzania ikianza kucheza mechi ya kwanza ugenini inapopangiwa timu za Afrika Kaskazini hasa Misri.

Jambo hili haliwezi kuwa linatokea kwa bahati mbaya lakini huenda Maofisa wa Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) yenye Makao Makuu yake Cairo, Misri wanaopanga ratiba hizo watakuwa wanafanya kwa makusudi ili kupendelea timu hizo.

Haiwezekani kama jambo hilo halifanywi kwa makusudi liwe linatokea kila mara kwa timu za Misri kuanzia ugenini na kumalizia mechi zake nyumbani kila zinapocheza na timu za Tanzania.

 

WAARABU WAMECHUJA

Tofauti na miaka ya nyuma timu za Afrika Kaskazini zilipokuwa zinatisha kwa ukali na kuogopwa katika michuano ya Klabu ya Afrika sasa timu hizo ubora wake na kiwango chake cha mchezo kimeporomoka. Hakuna siri kwamba Al-ahly au National na Esperance na timu nyingine za nchi hiyo zimeshuka kiwango na hazitishi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Sasa hivi wapinzani wao wakijipanga vizuri wanaweza kuwafunga ugenini na nyumbani na kuwatoa katika mashindano na sasa sio jambo la ajabu tena kuzing’oa timu hizo ambazo zilitawala soka la Afrika kwa miaka mingi.

Miaka ya nyuma hasa timu za Misri zilipokuwa zinaanza mechi ya awali ugenini zilikuwa zinapigania kutoka sare au hata kupata ushindi finyu ili kuvutia watazamaji katika mechi za marudiano na zilikuwa na uhakika wa kupata ushindi mnono.

Kile kipindi cha timu za Misri kuwafunga wapinzani wao mabao 4-0 au zaidi kimepotea na sasa hata zikipata ushindi ni wa kutafuta kwa mbinde na haiwi rahisi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

 

SILAHA YA MASHABIKI

Yanga na Azam zinaanza nyumbani April 9 na April 10 hivyo zitakuwa na mtaji mkubwa wa mashabiki ambao, watafurika Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Azam Complex zitakapochezea mechi hizo.

Kwa hiyo, Yanga na Azam zijipange ili ziweze kufanya vizuri katika hizo mechi za awali na kujipanga kwenda kuwakabili wapinzani wao nyumbani kwao na kuweza kuwang’oa katika mashindano hayo.

Huu ni wakati mwafaka kwa Yanga na Azam kuifikia rekodi ya Simba kwa kuzitoa timu za Arabuni kwani zipo katika kiwango kizuri na zina ubora wa hali ya juu, kitu pekee kitakachowabeba ni kujiamini na kuifanya kazi hiyo vizuri.

 

USHINDI NYUMBANI

Silaha kubwa kwa Yanga na Azam ni kupata ushindi mkubwa katika mechi za awali zitazochezwa nyumbani kwani, huo ndio utakuwa msingi mkubwa wa kuzishinda timu hizo za Misri na Tunisia.

Ushindi huo utazifanya ziende kwenye mechi za marudio ugenini zikiwa na hazina nzuri ambayo kama watailinda bila shaka wataibuka kidedea na kuweka historia mpya.

Yanga na Azam zinapaswa kujituma ili kupata magoli ya kutosha ya kufunga na kuhakikisha kwamba nyavu zake haziguswi ili kuondoa fursa ya kuwapa wapinzani wao faida ya goli la ugenini ambayo inaweza kuwabeba iwapo timu hizo zitatoka sare katika mechi zote mbili.

Kwa miaka hii kuzifunga timu za Misri na Tunisia ni jambo la kawaida tu ambalo linataka dhamira na maandalizi ya maana ambayo bila shaka Yanga na Azam watayapata kwani wana viongozi madhubuti.

Zikicheza mbele ya mashabiki wao Yanga na Azam zijipange vizuri ili zipate ushindi mnono zikielewa kwamba katika mechi za marudiano zitakazofanyika ugenini zitakuwa na washabiki wachache.

 

WASOME NYAKATI

Ni wajibu wa Kocha wa Yanga, Hans Pluijm na wa Azam, Stewart Hall kusoma na kuzigundua mbinu za wapinzani wao kimchezo na kuwaelimisha wachezaji wao jinsi ya kuzikabili na kuzishinda.

Kama ilivyo kwenye mtihani kuelewa swali ni nusu ya kufaulu na pia katika mpira wa miguu kuzielewa mbinu za mpinzani wako zinakujengea mazingira mazuri ya kupata ushindi.

Pamoja na hilo wachezaji wa Yanga na Azam hawana budi kuwa makini na kujituma ili kuzitetea vyema Klabu zao na kuipa heshima Taifa kwa kuibuka na ushindi na kusonga mbele katika mashindano hayo.

Hakuna kisingizio kitakachokubalika iwapo Yanga na Azam wataipoteza nafasi hii adhimu ya kuzitupa nje timu hizo za Misri na Tunisia katika mashindano ya Klabu Barani Afrika.

 

PENATI

Jambo lingine muhimu ni kwa makocha wa Yanga na Azam kuwatayarisha na kuwanoa wachezaji wao ili wawe tayari kwa mtindo wa kupigiana mikwaju ya penalti tano tano.

Si jambo la ajabu katika mpira wa miguu kwani, lolote linaweza kutokea kwa timu hizo kwenda sare na kwa hiyo mshindi hutakiwa kupatikana kwa mchakato wa kupigiana penalti.

Ni vyema makocha wakawatayarisha wachezaji wa kutosha wa kupiga penalti ili kuikabili hali hiyo pale itakapotokea baada ya penalti tano tano timu hizo ziko sare na kutakiwa kupigwa penalti za ziada.

Ni jambo la bahati mbaya kwamba timu nyingi zinakuwa na wachezaji wazuri katika penalti tano za kwanza, lakini baada ya hapo zinakosa mwelekeo.

 

MASHABIKI

Ni muhimu kwa mashabiki watakaojitokeza uwanjani wazishangilie timu za Yanga na Azam na ushabiki wa Usimba na Uyanga uwekwe pembeni kwani timu hizo zinawakilisha taifa.

Ile desturi ya kushangiria timu ngeni zinapocheza nyumbani iachwe na mashabiki kwani ni sumu ya maendeleo ya mpira wa miguu nchini.

 

Mwandishi wa Habari Mwandamizi amewahi kufanya kazi Televisheni Zanzibar, Uhuru na Mzalendo, Bussiness Times (Mhariri mwanzilishi wa Spoti Starehe) na Mwananchi. Alikuwa Mkurugenzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania[TEF]. Anapatikana kwa email [email protected] simu 0712-020020