Jamani eeh! Tuirudishe Simba yetu kwenye mstari
Muktasari:
- Katika Ligi Kuu 2013/14 tulitoka nao sare mabao 3-3 Oktoba 2013 katika mchezo wa kwanza ambao kuna watu waliokuwa uwanjani waliamini 5-0 tulizowapiga Yanga Mei 6, 2012 zingerudi, lakini vijana wa King Kibadeni na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ walitufariji kurejesha mabao matatu ya kipindi cha kwanza.
WAKATI wa uongozi wa Mwenyekiti, Ismail Aden Rage, Simba tulikuwa na furaha kwa misimu miwili tu. Mwaka 2011, wakati tuliposhiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ingawaje tulitolewa na TP Mazembe, lakini tulifuzu baada ya Rage kukata rufaa na kushinda.
Tukacheza na Raja Casablanca ya Morocco ambapo tulifungwa mabao 3-0 na kuangukia kwenye Kombe la Shirikisho.
Furaha ya pili chini ya uongozi wa Rage ilikuwa ni mwaka 2012, pale tulipoua ndege wawili kwa jiwe moja, kwanza tulichukua ubingwa wa Ligi Kuu tukamfunga Kwalalumpa mabao 5-0.
Mateso yakaanza
Baada ya hapo hali ilikuwa mbaya sana, wanachama wa Simba tukaingia kwenye kipindi cha majonzi, wenyewe tulikiita kipindi cha eda.
Hatukuwa na furaha, tulikuwa kama wajane tuliofiwa na waume zetu. Simba ilitolewa katika Ligi Mabingwa wa Afrika na Libolo kwa jumla ya mabao 5-0. Lakini pamoja na unyonge tuliokuwa nao chini ya uongozi wa Rage, msimu wa 2012/13, Yanga hawakutunyanyasa sana, walitufunga mabao 2-0 katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, Mei 2013.
Baada ya mchezo wa mzunguko wa kwanza walichomoa bao letu na kutoka nao sare 1-1. Nje ya Ligi tukawachapa 3-1 katika Nani Mtani Jembe, Desemba 2013 na 2-0 mwaka 2014.
Katika Ligi Kuu 2013/14 tulitoka nao sare mabao 3-3 Oktoba 2013 katika mchezo wa kwanza ambao kuna watu waliokuwa uwanjani waliamini 5-0 tulizowapiga Yanga Mei 6, 2012 zingerudi, lakini vijana wa King Kibadeni na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ walitufariji kurejesha mabao matatu ya kipindi cha kwanza.
Kisha tukatoka nao sare ya 1-1, Aprili 2014 katika mchezo wa mzunguko wa pili.
Ukombozi unakuja
Wanachama wa Simba baada ya kushindwa kumuondoa Rage madarakani kwa mapinduzi hatimaye aliondoka kwa hiari yake Juni, 30, 2014 baada ya kufanyika uchaguzi mkuu.
Ndipo wengi tulipoamini kuwa ukombozi umerudi na Simba itarudisha heshima yake chini ya Rais, Evans Aveva na Makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’.
Hapo tuliamini tutakuwa tunatoka eda na kurudia enzi zile za kuitwa Taifa Kubwa, kwa kutamba nyumbani na anga za kimataifa, lakini haikuwa hivyo.
Siyo kwenye soka tu, tuliamini Simba itakuwa katika ubora wake kwa kusimamia mapato na hata kuwa na uwanja wake kule Bunju kama harakati zilivyoanzishwa na Rage. Tuliamini kuwa furaha itarejea Msimbazi na kushika hatamu.
Msimu wa 2014/15 Simba tukitumia wachezaji wachanga, baada wale wa kutegemewa kufanyiwa figisufigisu, tulilazimisha sare ya 0-0 Oktoba 2014 dhidi ya Yanga.
Asante Okwi
Katika mchezo wa marudiano, Simba tuliifunga Yanga bao 1-0 lililofungwa na Mganda, Emmanuel Okwi.
Huo ulikuwa ni ushindi wa kwanza wa Simba katika Ligi Kuu kwa Yanga tangu 2012 tuliposhinda 5-0. Tulimaliza ligi tukiwa katika nafasi ya nne nyuma ya Yanga, Azam na Mbeya City.
Sasa tumekuwa wa matopeni
Msimu wa 2015/16, mbali na kukosa nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa, tumefungwa mechi zote mbili za Ligi Kuu kwa mabao 2-0 (ndani na nje) dhidi ya Yanga na kuambulia nafasi ya tatu.
Wakati tukiwa tunaelekea kwenye msimu wa 2016/17 bado Simba hatuna uhakika wa kufanya vizuri kwenye msimu huo.
Sasa tumefikia hatua ya kuitwa vyura wakati vyura wanapatikana Jangwani, tumeitwa wa matopeni wakati makao makuu yetu yapo katikati ya mji, Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Kabla ya kukutwa na majanga haya, Simba ilikuwa tamu, miaka michache nyuma tulikuwa na raha ikafikia hatua tukasema ikifika 2015 kila mtu atashabikia Simba.
Huu ni mwaka 2016, hali imekuwa mbaya zaidi kwa kuendelea kuitwa majina ya kejeli na Kandambili, mara wa mchangani au wa hapahapa, inauma sana.
Friends of Simba hoi
Rais wetu, Aveva amekiri kwamba klabu kwa sasa haina fedha za kuwekeza na kuendesha timu. Kwa maana nyingine hilo linatufanya tuwe wanyonge mbele ya Yanga na Azam pindi tunaposhindania wachezaji wazuri.
Imefika pahala Azam wanatupatia wachezaji wa mkopo! Yaani wale wa ziada.
Hiyo maana yake ni kwamba, viongozi hao wameshindwa kutumia rasilimali watu waliyokuwa nayo, wameshindwa kutumia majengo ya Simba kuweza kuingiza mapato na kuipaisha Simba kimataifa kwa kuwa timu bora na ya kisasa.
Imefika hatua Simba tunasubiri Azam na Yanga wachukue wachezaji wazuri na siye kusubiria wale wa bei rahisi ambao hawawahitaji.
Tumekuwa tukifanya usajili wa mabonanza ambao hauna kichwa wala miguu kwa ajili ya wachezaji wa nje. Haiwezekani mchezaji mzuri akatoka Congo, Ivory Coast au Ghana kuja kufanya majaribio Tanzania. Huku ni kuutukana mchezo wa soka na kutukosea heshima sisi Wanasimba.
Hili linashangaza kwa kuwa siku zote sisi ndio tumekuwa wajanja na tunaojua kusajili kuliko Yanga. Mara nyingi Kandambili wamekuwa wakiwatafuta wachezaji ambao waliosikia sisi tunawawinda.
Mifano iko mingi sana, tukianzia kwa Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite na Malimi Busungu na hivi karibuni Beno Kakolanya, Juma Mahadhi na wengine wengi.
Kama watu ambao tuliwaamini kwamba wangeweza kutuokoa katika mateso haya, Kundi la Friends of Simba wameshindwa ni nani atatuokoa? Hakuna cha Aveva, Kaburu wala Kasimu Dewji. Imefika mahali Simba inashindwa hata na kiburi cha Mbeya City ambayo ni timu ya Halmashauri? Simba tumepotea njia.
Maamuzi magumu
Mkutano Mkuu wa Simba unafanyika kesho Jumapili katika Ukumbi wa Bwalo la Polisi la Oysterbay jijini Dar es Salaam, je, tufanye maamuzi magumu?
Bila shaka kama tutaingia kwenye ligi msimu huu tukiwa na chini ya uongozi wa Aveva na wenzake, tutakuwa tunacheza bahati nasibu. Hilo halina ubishi. Suala kubwa linalosemwa ni kuhusu uamuzi wa kumpa au kutompa timu Mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘MO’.
Wanachama na wapenzi wa Simba mpaka sasa hatujui cha kufanya, kwa kuwa wengi hatuna elimu ya kutosha juu ya hilo. Nataka niwaulize wanachama wenzangu, mashabiki na wapenzi wa Simba, wanapata faida gani pindi Simba ikiwa chini ya uongozi wa kina Aveva, Rage na Hassan Dalali?
Furaha kubwa ni ushindi au siyo? Na tofauti yake ni kilio kwetu, huku kukiwa hakuna faida nyingine. Basi kama tunakata kutembea vifua mbele, hatuna budi kuuza hisa za klabu yetu.
Mashabiki watapata raha ya kuendelea kuishangilia Simba ambayo sasa itakuwa inafikiria kushindana na timu kama TP Mazembe, Etoile du Sahel, Enyimba na hata Al Ahly.
Wanachama wa Simba watanufaika kwa kupewa hisa katika klabu na kuweza kujiingiza kipato, hili si jambo dogo. Tahadhari ninayoitoa hapa ni kwamba, siyo lazima auziwe MO la hasha. Kama atamudu vigezo auziwe, lakini kama ni heri akauziwa tajiri mwingine yeyote.
Ili mradi tupate fedha ya kujiendesha, kusajiliwa wachezaji wa maana na kuwalipa kwa wakati bila kupigia magoti miungu watu. Pia, tukipata mtu mwenye fedha zake itarudisha jeuri ya Simba na hata ligi yetu itanoga tofauti na sasa. Haiwezekani Yanga na Azam zijibinafsishie nafasi mbili za juu kila siku. Na tunakoelekea kama tusipofanya maamuzi ya maana kesho pale kwenye mkutano tukaendelea kuwapigia makofi hawa viongozi kuna hatari hata Mbeya City wakatunyang’anya na hiyo nafasi ya tatu msimu ujao.
Mwandishi wa makala haya ni kada mkubwa wa Simba anayeishi Mabibo, Jijini Dar es Salaam.