Ishu ya Mnigeria Geita Gold iko hivi!
Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Geita Gold, Samwel Dida amesema uongozi unaendelea kupambana kwa ajili ya kuhakikisha kipa huyo anacheza, huku mchakato huo ukiwa pia katika hatua nzuri na za mwisho ili kukamilika.
UONGOZI wa Geita Gold umesema sababu kubwa ya kipa mpya wa timu hiyo raia wa Nigeria, Kayode Bankole Iyanu kukosekana katika mechi za Ligi Kuu Bara tangu msimu wa 2026-2027 umeanza ni kutokana na kuchelewa kibali cha kazi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Geita Gold, Samwel Dida amesema uongozi unaendelea kupambana kwa ajili ya kuhakikisha kipa huyo anacheza, huku mchakato huo ukiwa pia katika hatua nzuri na za mwisho ili kukamilika.
"Ni kweli Kayode haonekani uwanjani kwa sababu ya suala la kibali cha kazi, uongozi unaendelea kulishughulikia na hadi Ligi Kuu Bara itakaporejea ni matumaini yetu kila kitu kitaenda vizuri, hivyo mashabiki wasiwe na hofu," amesema Dida.
Aidha, Dida amesema lengo la timu hiyo ni kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali msimu huu hasa Ligi Kuu na tayari wameonyesha kwa mechi walizocheza, hivyo kazi iliyobakia ni kupata kibali cha kipa huyo ili aongeze ushindani kikosini.
Kipa huyo alijiunga na Geita Gold, Agosti 5, 2026, akitokea TS Galaxy ya Afrika Kusini kwa lengo la kuongeza nguvu ndani ya kikosi hicho kutokana na uzoefu wake, kwa msimu huu wa 2026-2027 wa mashindano mbalimbali hususani ya Ligi Kuu Bara.
Kayode aliyezaliwa Oktoba 16, 2002, ni kipa mzoefu aliyecheza klabu mbalimbali za Shooting Stars FC kuanzia mwaka 2019 hadi 2020, kisha Remo Stars FC 2020–2025 zote za kwao Nigeria na mwaka 2025 alijiunga na TS Galaxy FC ya Afrika Kusini.