Ibenge, Mgunda vitani Azam Complex
Muktasari:
- Azam yenyewe katika michuano ya kimataifa itaanzia raundi ya pili tofauti na Simba, Yanga na Singida Black Stars ambao wikiendi walikuwa mzigoni, hivyo kikosi hicho cha Florent Ibenge kwa sasa kina nafasi ya kuelekeza nguvu zake katika michezo ya Ligi Kuu Bara.
WAKATI wenzao wakipigania nafasi ya kutinga raundi ya pili mashindano ya kimataifa, Azam FC yenyewe itakuwa mzigoni leo Jumatatu kuendelea na mikiki ya Ligi Kuu Bara kwa kucheza dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Azam yenyewe katika michuano ya kimataifa itaanzia raundi ya pili tofauti na Simba, Yanga na Singida Black Stars ambao wikiendi walikuwa mzigoni, hivyo kikosi hicho cha Florent Ibenge kwa sasa kina nafasi ya kuelekeza nguvu zake katika michezo ya Ligi Kuu Bara.
Mchezo wa leo utakuwa pia kipimo kingine kwa makocha wawili, Ibenge wa Azam na Juma Mgunda wa Namungo, ambao wote watakuwa na jukumu la kuhakikisha timu zao zinapata pointi muhimu katika vita ya msimu huu.
Azam inaingia kwenye mchezo huo ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikikusanya pointi 11, wakati Namungo ikiwa nafasi ya 11 ikiwa na pointi sita. Tofauti hiyo ya pointi tano inaifanya Azam kuwa na mwanzo mzuri zaidi, lakini Namungo ina nafasi ya kupunguza pengo hilo endapo itapata ushindi Chamazi.
Kikosi cha Ibenge pia kinaingia kwenye mchezo huo kikiwa na hali nzuri kwa kuangalia matokeo ya mechi zake tano zilizopita. Azam haijapoteza mchezo wowote katika mechi hizo, ikishinda mitatu na kutoka sare mbili.
Azam ilianza mwenendo huo kwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania, kabla ya kuifunga TRA United mabao 2-1 na Pamba mabao 2-1 katika michezo iliyofuata. Namungo yenyewe katika mechi zake tano zilizopita, timu hiyo imeshinda mbili na kupoteza tatu.
Hata hivyo, rekodi ya mechi za hivi karibuni kati ya timu hizi mbili inaonyesha kuwa Namungo imekuwa ikitoa ushindani dhidi ya Azam. Katika mechi zao nne zilizopita, Azam imeshinda mbili huku michezo miwili ikiisha kwa sare. Katika mchezo wao wa mwisho uliopigwa Mei 5, 2026, Azam ilishinda bao 1-0 dhidi ya Namungo.