Hili ndio chama la Kachwele Ukraine
Muktasari:
- Kachwele mwenye miaka 21, ameingia Kryvbas baada ya msimu uliopita kucheza kwa mkopo HFX Wanderers ya Canada hivyo uwezo wake unatarajiwa kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
WIKIENDI hii mshambuliaji wa Tanzania, Cyprian Kachwele FC alitambulishwa Kryvbas Kryvyi Rih ya Ukraine baada ya klabu hiyo kumsajili kwa mkataba wa miaka minne, akitua kama mchezaji huru baada ya kumalizana na Vancouver Whitecaps ya Canada.
Kachwele mwenye miaka 21, ameingia Kryvbas baada ya msimu uliopita kucheza kwa mkopo HFX Wanderers ya Canada hivyo uwezo wake unatarajiwa kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Timu hiyo ilimaliza msimu uliopita katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 48, huku ikifunga mabao 53 katika michezo 30, wastani unaoonyesha kuwa timu hiyo ilikuwa na uwezo wa kutengeneza na kufunga mabao.
Hata hivyo, uwepo wa Kachwele unaweza kuongeza ubora na ubunifu mbele, hasa kutokana na uwezo wake wa kucheza kama mshambuliaji wa kati na kutumia nguvu pamoja na urefu wake katika mapambano ya ndani ya eneo la hatari.
Msimu uliopita Kachwele alikuwa sehemu ya HFX Wanderers kwa mkopo, baada ya awali kupitia mfumo wa Vancouver Whitecaps, akijenga uzoefu wa kucheza soka la Canada kabla ya sasa kuhamia Ukraine.
Kachwele alitimkia Canada akitokea Azam FC mwaka 2023, ambako alikuwa amepitia akademi ya klabu hiyo na baadaye kupandishwa kikosi cha kwanza na timu ya vijana. Baada ya kujiunga na Vancouver Whitecaps FC 2, alianza kujenga jina katika MLS NEXT Pro, akicheza mechi 39 na kufunga mabao 11 na asisti mbili.
Msimu wa 2024, Kachwele alicheza mechi 20 za MLS NEXT Pro, akifunga mabao manne na kutoa asisti moja. Mwaka uliofuata alikuwa na kiwango bora, akicheza mechi 19, akifunga mabao saba na kutoa asisti nne.
Kachwele pia alipata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza cha Vancouver Whitecaps katika MLS. Klabu hiyo ilimpa nafasi ya kuanza kwenye baadhi ya mechi akianza mechi moja kwenye michezo mitatu aliyokuwa benchi.
Mshambuliaji huyo aliyeitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa michezo ya kufuzu AFCON 2027 dhidi ya Guinea Bissau na Madagascar na mchezo wa kirafiki dhidi ya Ghana anaongeza idadi ya nyota kutoka Tanzania kucheza ligi hiyo baada ya awali Novatus Miroshi kukipiga Shakhtar Donetsk.