Hofu yaiponza Kilimanjaro Wonders Queens
HOFU ya kukutana na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Wanawake Tanzania Bara, Simba Queens, imetajwa kuchangia Kilimanjaro Wonders Queens kushindwa kutumia nafasi ilizopata na kukubali kichapo cha mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza wa ligi hiyo msimu wa 2026-2027, uliofanyika Uwanja wa Ushirika uliopo Moshi mkoani Kilimanjaro.
Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Wonders Queens, Daudi Macha, amekiri kuwa wachezaji wa kikosi chake walikosa utulivu mbele ya Simba Queens, hali iliyowafanya washindwe kutumia nafasi za kufunga na kuishia kuanza msimu kwa matokeo mabaya nyumbani.
Macha amesema licha ya kikosi chake kupata nafasi kadhaa za kufunga, uzoefu wa Simba Queens uliwapa wakati mgumu, hasa ikizingatiwa kuwa kwa Wonders huu ni msimu wake wa kwanza tangu ipande daraja.
“Mchezo ulikuwa mzuri. Kikubwa tulikuwa tunacheza na Simba ambayo ina uzoefu, halafu ni mabingwa watetezi vilevile,” amesema Macha.
Ameongeza kuwa kushindwa kutumia nafasi walizopata ni miongoni mwa upungufu ambao benchi la ufundi litafanyia kazi kabla ya michezo inayofuata.
“Wakati mwingine unaweza kupata nafasi sita ukashindwa kuzitumia kutokana na utayari wa wachezaji. Hii ni mechi yetu ya kwanza kwenye ligi na tumekutana na timu yenye wachezaji wa kimataifa kutoka Kenya, Uganda na Tanzania. Tunarudi kwenye uwanja wa mazoezi kufanyia kazi makosa,” amesema.
Wakati Wonders ikijutia nafasi ilizopoteza, Simba Queens ilionyesha uzoefu wake kwa kutumia vyema mipango ya mchezo na kuanza msimu kwa ushindi muhimu ugenini.
Kocha wa Simba Queens, Musa Mgosi, amesema kikosi chake kilitumia kipindi cha kwanza kuzisoma mbinu za wenyeji kabla ya kufanya marekebisho yaliyowasaidia kupata ushindi katika kipindi cha pili.
“Pongezi kwa wachezaji wote wa timu zote mbili kwa sababu kila timu imeonyesha kile inachokihitaji. Kama nilivyosema jana, tulikuwa tunacheza na timu ambayo hatuijui vizuri,” amesema Mgosi.
Ameongeza: “Kipindi cha kwanza tuliingia kwa mpango wa kuisoma mbinu yao. Kipindi cha pili tukafanya marekebisho ya ndani, tukaweka mipango ya kutumia nafasi na kupata picha halisi ya Kilimanjaro Wonders.”
Mgosi amesema Simba Queens haitaki kulegeza kamba katika mbio za kutetea ubingwa, akisisitiza kuwa lengo lao ni kupata pointi tatu katika kila mchezo.
“Kila mechi kwetu ni fainali na lazima tuhakikishe tunapata pointi tatu,” amesema kocha huyo.
Beki wa Simba Queens, Fatuma Issa, amesema ushindi huo ni mwanzo mzuri kwa kikosi chao, hasa kwa kuwa walikuwa wakicheza ugenini katika mchezo wa ufunguzi wa ligi.
“Kwanza tunapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hiki alichotupatia kwa sababu si rahisi. Kama mnavyojua, huu ni mwanzo wa ligi na tuko ugenini,” amesema Fatuma.
Amesema maandalizi yao yalilenga kupata pointi tatu na kufunga mabao, huku sasa wakielekeza nguvu kwenye mchezo unaofuata ili kuendeleza matokeo mazuri.
“Tulijipanga kwamba kila mechi tuweze kupambana kupata alama tatu muhimu pamoja na mabao. Sasa tunaangalia mchezo unaofuata ili tuweze kufanya vizuri zaidi,” amesema.
Kwa upande wake, nahodha wa Kilimanjaro Wonders Queens, Kadoshi Shekigenda, amesema kichapo hicho kimewapa funzo muhimu watakalolitumia kujiandaa kwa michezo ijayo.
“Sisi kama timu tumepoteza mchezo, lakini tumejifunza mengi sana kupitia wenzetu wa Simba kwa sababu ni timu bora yenye wachezaji wazuri,” amesema Kadoshi.
Ameongeza: “Hii ni mara yetu ya kwanza kuingia kwenye ligi kuu. Tutaenda kusahihisha makosa yetu na mwalimu ili twende sawa kwenye michezo ijayo.”
Naye shabiki wa Kilimanjaro Wonders Queens, Musa Said maarufu kama Musa Kipipa, amewataka wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hiyo badala ya kuzipa sapoti timu za wageni.
“Tumeona Simba ni timu kubwa, lakini tumepunguza magoli kwa sababu timu yetu ni changa iliyopanda daraja msimu huu,” amesema Kipipa.
Ameongeza: “Nitoe wito kwa mashabiki wa Mkoa wa Kilimanjaro; hii ndiyo timu yetu ya wanawake, tuishabikie kwa wingi. Isije ikawa Simba inakuja hapa mnashangilia Simba halafu uwanjani hamna mashabiki wa Kili Wonders. Tuisapoti timu yetu!”