Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hivi mmeielewa hukumu ya TFF?

Rais wa TFF, Jamal Malinzi

Muktasari:

KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilitoa hukumu juu ya suala la upangaji matokeo lililokuwa zinazikabili timu nne kutokana na mechi zao za Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.

KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilitoa hukumu juu ya suala la upangaji matokeo lililokuwa zinazikabili timu nne kutokana na mechi zao za Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.

Hukumu hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa mpira wa miguu nchini imetegua kitendawili kutokana na sakata hilo lililochukua miezi kadhaa.

Katika hukumu yake Kamati ya Nidhamu imezishusha daraja timu zote nne, kuwafungia viongozi, makocha, marefa na wachezaji wanaodaiwa kuhusika katika upangaji huo wa matokeo.

Timu ambazo zinaathirika kutokana na sakata hilo ni Geita Gold, Kanembwa JKT, JKT Oljoro na Polisi Tabora ambazo zimeshushwa daraja katika msimu ujao wa ligi.

 

Ni uamuzi wa aina yake

Uamuzi huo wa kamati ya Nidhamu ya TFF ni wa kihistoria kwani kwa muda mrefu adhabu za kufungiwa maisha zilikuwa hazijasikika Tanzania kwa makosa mbalimbali yanayotokana na mchezo wa mpira wa miguu.

Adhabu hizo zitakuwa zimetoa somo katika familia ya soka na iwapo kuna usikivu inatarajiwa kwamba suala la upangaji matokeo litakuwa historia Tanzania.

Kwakweli adhabu hizo ni kubwa lakini kwa upande mwingine zinatoa funzo kubwa kuwa suala la upangaji wa matokeo ya michezo ni jambo lisilofaa na ni kikwazo cha maendeleo ya mpira wa miguu.

Kamati ya Nidhamu pamoja na kufanya kazi nzuri lakini hukumu yao ina baadhi ya dosari ambazo zimepunguzia ubora wake. Ndio maana nauliza hivi mmeielewa?

 

Adhabu ya vifungo

Kwanza mara nyingi kumekuwa na desturi ya kutolewa kwa adhabu ya vifungo. Adhabu ya kuwafungia watu maisha ni adhabu kubwa sana kwani zinawaumiza wachezaji ambao ndio iliokuwa njia yao kuu ya maisha yao ya kila siku.

Sio kwamba kosa lao ni dogo, lakini kuwafungia maisha ni kuwanyima uhuru wao na kuwajengea mazingira mabaya ya maisha yao ya baadaye.

Pia, kumfungia mchezaji wa ridhaa kifungo cha miaka 10 na kumtaka alipe faini ya Shilingi 10 milioni ni kichekesho kwani ni vigumu sana kulipa faini hiyo.

Kama mchezaji angepigwa faini na kufungiwa kwa miaka michache kungetoa matumaini kwa klabu yake ingeweza kumlipia kwa matumaini kwamba atarudishwa tena uwanjani kuichezea timu hiyo.

Lakini unapomfungia mchezaji miaka mingi kiasi hicho ni kama umemfungia maisha kwani baada ya miaka hiyo ni vigumu kurudi mchezoni akiwa na kiwango kizuri cha mchezo ambacho kitampa nafasi ya kusajiliwa na timu yoyote.

Mchezaji anayefungiwa miaka 10, sio rahisi kuweza kulipa faini ya Shilingi 10 milioni kwani haitamsaidia lolote kwani hata akimaliza kifungo hicho atakuwa hana thamani tena katika ulimwengu wa soka.

Kwa hiyo faini hii ya Shilingi 10 milioni na kifungo cha miaka 10 ni adhabu ngumu kutekelezeka na itashangaza iwapo wachezaji hao watalipa faini hizo.

 

Geita Gold ibaki FDL

Baada ya mechi za mwisho za Ligi za Daraja la kwanza Tanzania Bara, Geita Gold ilikuwa imepanda Ligi Kuu Bara kama ilivyokuwa kwa African Union na Ruvu Shooting ya Pwani.

Katika hali hiyo, Geita ilikuwa si timu ya daraja la kwanza bali ilikuwa katika Ligi Kuu kwahiyo kwa kuinyima tiketi ya kucheza katika ligi hiyo kubwa nchini ilikuwa ni adhabu tosha na kubwa kwa kupanga matokeo.

Lakini kuishusha Geita hadi Ligi la Daraja la Pili ni kuionea na haistahili adhabu hiyo kwani inapaswa ibaki Ligi Daraja la Kwanza ambapo itakuwa kama vile imeshushwa daraja kwani tayari ilishakuwa Ligi Kuu.

Geita haiwezi kupewa adhabu sawa na JKT Oljoro na Polisi Tabora ambazo zilikuwa FDL baada ya kumaliza msimu wa ligi hiyo ya Daraja la Kwanza na sasa zimepelekwa zote tatu katika Ligi Daraja la Pili.

Kanembwa JKT ambayo ishashuka kutoka Daraja la kwanza na kwenda la Pili lakini imeshushwa zaidi hadi Ligi ya Mkoa jambo ambalo ni sahihi lakini inashangaza Geita Gold haikutendewa haki hiyo.

Ni vyema adhabu ya Geita Gold ikatizamwa upya na kurudishwa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) mahali ambapo timu hiyo inayofundishwa na Kocha wa Selemani Matola inastahili.

 

Viongozi wameepukaje?

Kuna baadhi ya viongozi wa timu hizo nne kutokana na madai ya kupanga matokeo wameathibiwa, lakini ilishangaza watendaji wengine wakuu wa timu hizo wamechomoka katika tuhuma hizo.

Jambo hilo linaleta walakini kwa baadhi ya viongozi wakuu kama vile makatibu au makocha wakuu kuwa hawahusiki katika madai ya timu zao kupanga matokeo.

Inawezekana uchunguzi wa kina haukufanya au viongozi hao wamefanyiwa upendeleo hatua ambayo imewafanya viongozi hao wakwepe rungu hilo la adhabu.

Ni vigumu kuamini kwamba viongozi hawa hawakuhusika kwa namna yoyote ile katika tuhuma hizo za kupanga matokeo ambao zimekuwa gumzo baada ya kumalizika Ligi Daraja la Kwanza.

 

Funzo tosha

Suala la upangaji wa matokeo ya michezo ya mwisho ya Ligi Daraja la kwanza ambapo Geita iliifunga Kanembwa JKT mabao 8-0 na JKT Oljoro iliilaza Polisi Tabora mabao 7-0 ni jambo ambalo linatakiwa litoe funzo kwa Watanzania.

Inawezekana mazingira yaliosababisha matokeo haya ndio yaliosababisha kuwepo kwa tuhuma za upangaji wa matokeo, lakini haidhaniwi matokeo yenyewe ndio yawe chanzo cha kuwepo kwa tuhuma hizo.

Kwani katika miaka ya karibuni imetokea hata katika Ligi Kuu Bara ambapo Yanga ya Dar es Salaam iliifunga Coastal Union ya Tanga mabao 8-0 na Taifa Stars ya Tanzania ilifungwa mabao 7-0 na Algeria katika mechi za kufuzu fainali za Kombe la Dunia lakini hakukuwepo tuhuma za upangaji matokeo.

Kwa hiyo tuhuma za upangaji matokeo zilihitaji uchunguzi makini ambao unapaswa kufanywa na viongozi waadilifu ili isije ikatokea timu ambayo haina makosa ikaathiriwa na uamuzi wa kutolewa kwa kusingiziwa kuwa ilipanga matokeo.

 

Hongera zao

African Lyon na Ruvu Shooting zimepata nafasi ya kupanda Ligi Kuu bila kutarajia kwa hakika zinastahili pongezi kwa mafanikio walioyapata. TFF itufafanulie mapema klabu ipi kutoka Kundi C itaungana na klabu hizo?

Licha ya kuwepo kwa fununu kwamba Mbao FC ilikamata nafasi ya nne itapewa nafasi hiyo, lakini tujiridhishe kwa kanuni ipi? Kama hakuna kanun, basi timu zilizosalia katika kundi hilo ikiwamo Mbao FC, Panone FC, Polisi Mara na Rhino Rangers zicheze play-off baina yao kisha bingwa apande Ligi Kuu moja kwa moja.

Kwa timu zilizopanda licha ya kuzipongeza, lakini pia nizikumbushe kuwa, kupanda Ligi Kuu ni jambo moja, kuweza kumudu mikiki mikiki ya ligi hiyo ni jambo tofauti.

Masoud Sanani ni mwandishi wa habari mwandamizi amewahi kufanya kazi Televisheni Zanzibar, Uhuru na Mzalendo, Business Times ( Mhariri mwanzilishi wa Spoti Starehe ) na Mwananchi. Alikua Mkurugenzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania ( TEF). Anapatikana email [email protected] simu 0712-020020