Himid Mao: Ngoma bado mbichi hii
KIUNGO wa Azam FC, Himid Mao amesema licha ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya ZED FC ya Misri mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika anaamini bado mechi ya marudiano ipo wazi kwa timu zote.
Mao amesema hawawezi kupuzia kuona watakuwa na kazi rahisi kutokana na bao walilopata ugenini jambo la msingi kwao ni kujipanga kuhakikisha wanautumia vizuri uwanja wao wa nyumbani.
“Haikuwa mechi rahisi, lakini angalau tumetoka sare ya bao 1-1 kwa upande wangu naona bado mechi ni 50 kwa 50 kwa maana hatuwezi kuridhika bado tuna kazi ya kufanya ili tusonge mbele kwenye michuano hiyo” amesema Mao na kuongeza;
“Jambo la kwanza ni kusahau matokeo yaliyopita ili kuyatafuta matokeo ya ushindi ndipo tutapata hatua nyingine ya kupambania hatua makundi, lakini kikubwa mechi za CAF zinahitaji umakini wa hali ya juu.”
Amesema wanatamani kuhakikisha msimu huu wanatinga hatua ya makundi kwenye michuano ya CAF kama ilivyokuwa msimu uliopita:”Lengo ni kupiga hatua zaidi, lakini ili tufikie hatua kubwa zaidi lazima tuanze na kufika makundi kwanza”
Amesema anaamini kocha ameyaona makosa ya kuboresha ambayo atawaelekeza ili mechi ya marudiano wafanye vizuri.
“Kocha ameona ni wapi ambapo ataturekebisha ili kufanya vizuri zaidi hasa kupata ushindi.”