Hesabu zaibeba Yanga
KITENDO cha Simba kuwa na nafasi ya kuwatoa kileleni ikiwa watashinda mechi zao za viporo kwenye Ligi Kuu pengine kinawapa wasiwasi mashabiki wa Yanga ambao timu yao inaongoza msimamo wa ligi.
Kabla ya mechi ya jana baina ya Yanga na Kagera Sugar, Yanga ilikuwa na pointi 45 huku ikiwa imecheza mechi 19 - mbili zaidi ya zile ambazo watani wao wa jadi wamecheza na ikiwa Simba itapata ushindi katika mechi mbili za viporo itakwea kileleni ikikusanya pointi 45.
Hata hivyo, Simba wanakabiliwa na mechi sita za nguvu katika Ligi Kuu ambazo wasipochanga karata zao vyema wanaweza kuwapa fursa nzuri Yanga kuendelea kuongoza msimammo wa ligi na hata kutwaa ubingwa msimu huu.
Historia ya ushindani baina ya timu hizo pamoja na mazingira ya baadhi ya viwanja ambavyo vitatumika kwa mechi hizo, vinailazimisha Simba kutazama kila mchezo kati ya hiyo mitano kama fainali ili ishinde na kutimiza malengo yake ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Mechi ya kwanza ni ile ya kiporo baina ya Simba na Namungo ambayo itachezwa katika Uwanja wa Kassim Majaliwa, Ruangwa - Lindi.
Namungo licha ya ubora wa kikosi chake ambacho kimekuwa kikicheza vyema dhidi ya Simba, watakuwa na faida ya kucheza nyumbani ambako mara zote huisumbua Simba.
Simba imecheza mbili katika uwanja huo na zote zilimalizika kwa sare, matokeo ambayo kama yatatokea hivyo katika mechi ya kiporo msimu huu au Simba kupoteza, yatainufaisha Yanga.
Ukiondoa mechi dhidi ya Namungo, Simba pia ina kibarua cha mechi mbili kubwa dhidi ya washindani wao wawili wakubwa kwenye mbio za ubingwa msimu huu ambao ni Yanga na Azam.
Katika mzunguko wa kwanza, Simba ilivuna pointi mbili tu katika mechi dhidi ya timu hizo mbili na ili ijiweke katika nafasi nzuri ya kutwaa taji, inapaswa kuhakikisha inapunguza au kuongeza pengo la pointi dhidi ya timu hizo mbili kwa kuibuka na ushindi na sio vinginevyo.
Yanga katika siku za hivi karibuni imeonekana kuleta ushindani mkubwa kwa Simba pindi wakutanapo na ushahidi wa hilo, katika mechi tatu zilizopita imepata ushindi mara moja na timu hizo zimetoka sare mara mbili.
Mbali ya mechi hizo, Simba pia itakabiliwa na mechi mbili ugenini dhidi ya timu za Polisi Tanzania na Kagera Sugar, mahali ambako timu pinzani zimekuwa zikipata wakati mgumu kupata matokeo mazuri.
Uwanja wa Kaitaba unaotumiwa na Kagera Sugar ndio umekuwa ukionekana mgumu kwa Simba katika miaka ya hivi karibuni kwani mara kwa mara imekuwa ikipata wakati mgumu kushinda mbele ya Kagera Sugar uwanjani hapo na takwimu zinaonyesha kwamba Simba imeshinda mara tatu huku ikifungwa mara mbili.
Mechi mbili ambazo Simba itacheza na Prisons na Mtibwa Sugar jijini Dar es Salaam nazo zinaweza kuwa kigingi kingine kwa Simba kutokana na historia ya timu hizo kuwavimbia pindi wanapokutana iwe nyumbani au ugenini.
Msimu uliopita, Prisons iliwalazimisha sare ya bila kufungana pindi Simba walipokuwa wenyeji na msimu huu tayari ilishachukua pointi tatu baada ya kuibuka na ushindi wa bao 10 dhidi ya Simba.
Lakini kama ilivyo kwa Prisons, Mtibwa Sugar nao wanaweza kuwashangaza Simba jijini Dar es Saam ikiwa wataingia kwa kubweteka.
Kocha wa Yanga, Cedrick Kaze alisema kuwa timu yake imejipanga kusaka pointi kwa nguvu zake pasipo kutegemea matokeo ya nyingine.
“Sisi hatuangalii wengine wanafanya nini. Tunajipanga kuhakikisha tunapata ushindi kwenye mechi zetu na tunaamini tukifanya vizuri tutamaliza vyema pasipo kuanza kuwaza nani amfunge nani,” alisema Kaze.
Ligi ni ngumu na kila timu ni nzuri hivyo tunatakiwa kuhakikisha tunakuwa bora muda wote.”