Hesabu kali Raskazone Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- Mara ya mwisho timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu iliitembezea kibano Mafunzo cha mabao 2-0 na kushika nafasi ya saba na pointi 10.
KOCHA Mkuu wa Raskazone, Salum Ali Haji amesema kwa sasa malengo yao ni kukusanya pointi zitakazowaweka katika mazingira mazuri katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL).
Mara ya mwisho timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu iliitembezea kibano Mafunzo cha mabao 2-0 na kushika nafasi ya saba na pointi 10.
Kocha huyo amesema Ligi Kuu ni ngumu, hivyo lazima kwanza wajipange kukusanya pointi mapema zitakazoiondosha katika hatari ya kushuka daraja.
Amesema, baada ya kujihakikishia hilo, itaangalia namna nyingine kama ya kupigia hesabu ya ubingwa au kumaliza ndani ya nne bora kupata nafasi ya kushiriki Kombe la Muungano.
“Tunashuruku mpaka sasa tuna alama kumi na tupo nafasi ya saba, tunaamini tukifanya vizuri katika michezo mitatu ijayo tutaingia katika nne bora,” amesema.
Kocha Salum amesema mpaka sasa maandalizi yanaendelea vizuri kujiandaa na mchezo wao unafuata dhidi ya Polisi utakaochezwa Oktoba 12, 2026 kwenye Uwanja wa Kitogani uliopo Kusini Unguja.