Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HERSI: Mchakato wa mabadiliko Yanga umekamilika

Muktasari:

  • Hersi aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa utekelezaji wa mradi wenye thamani ya Sh5.5 bilioni wa ujenzi wa jengo la Yanga Tower lililopo Mtaa wa Mafia na Nyamwezi, Kariakoo, litakalokuwa na ghorofa 14.

RAIS wa Yanga, Mhandisi Hersi Said, amesema mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji ndani ya klabu hiyo umeshakamilika rasmi, na sasa wanajiandaa kuingia kwenye hatua mpya ya utekelezaji.

Hersi aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa utekelezaji wa mradi wenye thamani ya Sh5.5 bilioni wa ujenzi wa jengo la Yanga Tower lililopo Mtaa wa Mafia na Nyamwezi, Kariakoo, litakalokuwa na ghorofa 14.

Kiongozi huyo amewatoa hofu wanachama na mashabiki wa Yanga kwa kuweka wazi kuwa mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji ulikuwa unasubiri hatua za kisheria na kiofisi, ambapo kinachofuata sasa ni kuanzishwa kwa kampuni maalum itakayoiendesha klabu hiyo pamoja na kuanza uuzaji wa hisa.

"Mchakato wa mabadiliko umeshakamilika. Kilichokuwa kinatakiwa kwetu sisi ni kupiga hatua zinazofuata, ambazo hatua zenyewe ni kufungua kampuni. Kampuni hiyo ndiyo itakayoiendesha klabu yetu na tutaanza kuuza hisa," alisema Hersi.

Akiweka sawa dhana ya umiliki na faida za kifedha kwa wanachama, Hersi alibainisha kuwa Yanga ikiwa kama chama au taasisi inaendelea kuwa mali ya umma na mwanachama ndiye mmiliki mkuu.

Hata hivyo, alifafanua kuwa uanachama kwenye taasisi ya umma haumpi mtu faida ya moja kwa moja ya kuingiza fedha mfukoni, bali faida yake kuu ni kunufaika na burudani pamoja na huduma zinazotolewa na klabu hiyo.

"Ukija kwenye swali la msingi la mwanachama, klabu ya Yanga ikiwa ni ya mwanachama, mwanachama yeye ni mmiliki kwa sababu taasisi yetu ya Yanga ni mali ya umma. Mali ya umma ni mali ambayo haimnufaishi mtu kitaalamu kwa kupata fedha, lakini inamnufaisha kwa yeye kuwa mwanachama wa hiyo taasisi na kuburudika na hiyo huduma," alieleza Hersi.

"Unaposema leo Yanga inaendesha biashara ya mpira, faida kubwa unayoipata ukiwa mwanachama ni kunufaika na burudani inayotolewa na taasisi, lakini hakuna faida ya kifedha unayoipata mfukoni," aliongeza.

Kuhusu miradi ya miundombinu na majengo ya klabu, Hersi alieleza kuwa uwekezaji huo una dhamira kuu ya kuipatia Yanga uimara wa kifedha kama taasisi, jambo linalosaidia uendeshaji bora wa shughuli zote za klabu.

Aliongeza kuwa, uimara huo wa kifedha ndio unaowezesha klabu kusajili wachezaji bora, kuleta makocha wa kiwango cha juu, na kuimarisha operesheni za klabu ili kupata matokeo mazuri uwanjani.

"Jengo kama hili ni linakupa uimara wa kifedha wa taasisi yako. Taasisi yako ikipata uimara wa kifedha itaweza kuwa na uendeshaji mzuri na mwisho wa siku itakuwa imara kwenye kuendesha shughuli zake. Utapata wachezaji wazuri, makocha wazuri, na operesheni za klabu zitakwenda vizuri," alisema Hersi.

"Mwisho wa siku timu itafanya vizuri, na hilo ndilo lengo hasa la wewe kuwa mwanachama na shabiki wa Yanga kuhakikisha unafurahia huduma na matokeo uwanjani," alihitimisha.

Ikumbukwe kuwa, mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa Klabu ya Yanga, umepitia hatua mbalimbali za kihistoria zenye lengo la kuifanya klabu hiyo kujiendesha kisasa na kwa ufanisi wa kifedha.

Wazo la kufanya mabadiliko ya uendeshaji ndani ya Yanga lilikuwepo kwenye Katiba ya klabu hiyo tangu mwaka 2010, ingawa lilikaa kwa takriban miaka 10 bila kufanyiwa kazi.

Mchakato huo ulianza kushika kasi baada ya kuundwa kwa kamati ya mabadiliko chini ya Alex Mgongolwa, iliyofanya kazi kwa ushirikiano na ushauri wa kitaalamu kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Hispania (La Liga) na Klabu ya Sevilla. Ripoti ya kamati hiyo ilikabidhiwa kwa Mwenyekiti wa Klabu wa wakati huo, Dk Mshindo Msolla na aliyekuwa Mshauri wa Klabu, Senzo Mbatha, ili kuandaa muundo mpya wa uendeshaji.

Baadaye, uongozi uliunda kamati ya mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na mwanasheria Raymond Wawa ili kurekebisha Katiba ya Yanga iendane na ripoti ya mabadiliko. Mchakato huo pia ulihusisha utafutaji wa miongozo na kibali kutoka kwa vyombo vya serikali na mamlaka za michezo kama vile Wizara ya Michezo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi, na Tume ya Ushindani Halali wa Biashara (FCC).

Juni 27, 2021, wanachama 1,170 waliojiandikisha katika Mkutano Mkuu uliofanyika ukumbi wa DYCC jijini Dar es Salaam, walipitisha rasmi mabadiliko hayo ya uendeshaji na katiba kwa kura za ndiyo. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na mgeni rasmi, Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete.

Kulingana na Rais wa Yanga, Mhandisi Hersi Said, muundo huo mpya unaiunganisha klabu kuwa kampuni, ambapo wanachama wanamiliki asilimia 51 ya hisa na wawekezaji wanamiliki asilimia 49 za hisa. Katika asilimia hizo 49 za wawekezaji, zimepangwa kugawiwa kwa wawekezaji wanne ambapo kila mmoja atakuwa na asilimia 12.5.

Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Yanga SC itaundwa na jumla ya wajumbe tisa (9), wakitoka watano (5) upande wa wanachama na wanne (4) kutoka upande wa wawekezaji. Aidha, tathmini rasmi iliyofanyika ilibainisha kuwa thamani ya Klabu ya Yanga ni Sh100 bilioni.

Katika kuimarisha miundombinu na uendeshaji wa klabu, Yanga pia iliingia mkataba wa ubia wa umiliki wa asilimia 50 kwa 50 na GSM Group kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa kisasa wa klabu hiyo eneo la Jangwani, ambapo Yanga imetoa eneo la ardhi lenye ukubwa wa mita za mraba 35,000 na GSM inagharamia ujenzi huo.