HATARI! Cheki derby za kibabe Afrika

Muktasari:
MWISHO wa ubishi. Kuanzia saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, jijini Dar es Salaam kuna shughuli pevu itafanyika wakati vikosi vya Simba na Yanga vitakapovaana katika mechi yao ya kiporo cha Ligi Kuu Bara.
MWISHO wa ubishi. Kuanzia saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, jijini Dar es Salaam kuna shughuli pevu itafanyika wakati vikosi vya Simba na Yanga vitakapovaana katika mechi yao ya kiporo cha Ligi Kuu Bara.
Simba na Yanga zinakutana kwenye mechi yao ya 106 katika Ligi ya Bara tangu 1965, huku ikiwa ni mtihani mkubwa kwa makocha wa timu hizo wanaokutana kwa mara ya kwanza, Didier Gomes wa Simba na Nasreddine Nabi.
Mfaransa Gomes atakuwa mwenyeji wa Nabi katika pambano hilo la kiporo baada ya awali timu zao kushindwa kuvaana Mei 8 kwa sababu ya kuahirishwa kitatanishi muda mchache kabla ya kufanyika kwake.
Ila kama hujui ni kwamba Kariakoo Derby ni moja kati ya derby kali za Afrika, huku kesho Jumapili kutakuwa na derby nyingine matata ya Mashemeji itakayopigwa kwa majirani zetu wa Kenya wakati Gor Mahia na AFC Leopards zitakapokwaruzana kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho (Betway Cup).
Hapa chini ni derby kali za Afrika ikiwamo ya leo pale kwa Mkapa na nyingine pale Uwanja wa Utalii.
SIMBA v YANGA
Hii ni moja ya derby matata Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla ikivuta hisia za wengi na mara nyingi mwamuzi huwa na kazi ya ziada kuhakikisha anapunguza presha ya mashabiki pamoja na wachezaji ili kila kitu kiende salama.
Kabla ya leo Simba na Yanga zimeshakutana mara 105, huku Yanga ikishinda mara 37 na Simba 31 na michezo 31 ikiisha kwa sare, huku rekodi zikionyesha kwenye mechi hizo, Jangwani wamefunga mabao 111 na Msimbazi 100, huku kipigo kikubwa cha kihistoria ikiwa ni kile cha mwaka 1977 Simba iliposhinda mabao 6-0.
Timu hizi zilianza kuwa wapinzani tangu Simba ilipojiengua kutoka kwa Yanga mwaka 1936 na zimeanza kukutana katika Ligi ya Bara kuanzia 1965 na huwa na joto la aina yake kabla na baada ya kuchezwa kwake na leo kazi ipo mikononi mwa Emmanuel Mwandembwa kama mwamuzi wa kati.
GOR MAHIA v AFC LEOPARDS
Mashemeji derby, wanakutana kesho tu katika mechi yao ya Kombe la Shirikisho (FKF Betway) kwenye Uwanja wa Utalii.
Ingwe na Kogal’O huwa ni shughuli pevu kwelikweli kwani wakati mwingine derby yao inahamia hadi mitaani kutokana na ushabiki wao ulivyojikita kwenye ukabila zaidi tofauti na Kariakoo derby.
Timu hizi mbili zinashikilia rekodi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Kenya mara nyingine, lakini pia kutawala sehemu kubwa ya soka la nchi hiyo, licha ya kipindi cha sasa ndio zinarudisha makali baada ya misimu kadhaa nyuma kuyumba kutokana na tatizo la kiuchumi.
ESPERANCE v ETOILE DU SAHEL
Ni klabu mbili zenye upinzani mkubwa katika soka la nchini Tunisia, zote zikitokea kwenye jiji la Tunis zikiwa na mashabiki wengi katika nchi hiyo.
Mchezo huu unatajwa kama vita ya timu mbili zilizojichimbia na kujivunia kutokana na maeneo ya vitongoji vyao vilipo.
Mwanzoni klabu ya Esperance ilikuwa ikitajwa kama klabu ya serikali na ya watu wenye nyadhifa kubwa serikalini huku Club Africain ikitajwa kama klabu ya watu wa kawaida jambo linalonogesha upinzani wa klabu hizo zikikutana.
Hata hivyo, kuna derby ya Tunis ‘Derby Tunisois’ kati ya Esperance na Club Africain katika Uwanja wa El Menzah uliokuwa unachukua idadi ya watazamaji 45,000 kabla ya kuhamia Olympique de Rades unaokusanya watazamaji 60,000 kama ulivyo Uwanja wa Mkapa.
ORLANDO PIRATES v KAIZER CHIEFS
Hii ni zaidi ya mechi ya watani wa jadi. Ni klabu mbili kutoka kitongoji cha Soweto ambacho ni moja ya vitongoji maarufu nchini Afrika Kusini, umaarufu unaojengwa na historia ya kitongoji hicho ambacho kimejaa matukio mengi.
Klabu ya Kaizer Chiefs ‘Amakhosi’ ilianzishwa na mchezaji wa zamani wa Orlando Pirates ‘Motaung’ iliasisiwa mwaka 1970 yaani miaka 51 iliyopita.
Lugha rahisi unaweza kusema Kaizer Chiefs ilitokea kwa Orlando Pirates.
Mwanzoni zilikuwa klabu mbili zenye ukaribu mkubwa lakini kadri miaka ilivyokuwa ikisonga ndivyo utani wao wa jadi ulivyokuwa ukiongezeka mpaka kufikia leo ambapo inaelezwa Kaizer Chiefs ndiyo klabu yenye mashabiki wengi nchini Afrika Kusini na nje ya nchi hiyo yenye mashabiki zaidi ya milioni 20.
Klabu ya Orlando Pirates ndio klabu kongwe zaidi Afrika Kusini baada ya kuanzishwa mwaka 1937 yaani ni miaka 74 iliyopita.
Licha ya ushindani wa klabu hizi mbili kwenye soka lakini zimekuwa zikihusika katika kupambana na ubaguzi wa rangi.
RAJA CASABLANCA v WYDAD ATHLETIC
Moja kati ya michezo inayovutia kwenye soka la Afrila ni kutazama mchezo huu unaozikutanisha klabu mbili pinzani zaidi nchini Morocco.
Ni rangi ya kijani dhidi ya nyekundu.
Moja ya sifa kubwa inayoufanya mchezo wa klabu hizi kutajwa kama mchezo mkubwa wa watani wa jadi ni kutokana na aina ya soka linalochezwa uwanjani huku likinogeshwa na jinsi mashabiki wanavyotimiza wajibu wao wa kuimba kwa nguvu zote kuanzia dakika ya kwanza mpaka kuisha kwa mchezo.
AL AHLY v ZAMALEK
Hii ndio mechi inayotajwa kuwa nambari moja kwa watani wa jadi Afrika.
Ni klabu zinazopatikana katika mji mkuu wa Misri, Cairo.
Chama cha soka nchini Misri huwa kinaandaa kalenda maalumu kuhusu mchezo utakaozikutanisha klabu hizi mbili zenye upinzani mkubwa kutokana na historia yao ilivyo.
Kwasasa zikikutana mashabiki hawaruhusiwi kuingia kutokana na fujo zilizowahi kutokea kwenye mchezo baina ya timu hizo na kusababisha vifo vya mashabiki.