HAMZA KALALA-2 : Alilipwa Sh11,000 na maisha mengine yakafuata
Muktasari:
Mzee Kawawa akafurahishwa na muziki waliuporomosha siku hiyo, ndipo alipouliza hawa vijana wanatokea wapi.
KATIKA toleo la jana Jumatatu makala haya yalizungumzia namna ambavyo Hamza Kalala alivyopigishwa msoto akivizia ajira ya muziki. Na hapa anaendelea kuzungumzia mambo mbalimbali yaliyojitokeza, lakini kuna wakati walilipwa Sh 11,000 ili wakapige kazi. sasa endelea...
Walipwa Sh11,000
Bendi hiyo ikafanya kazi na shirika hilo hadi maadhimisho ya miaka 10 ya uhuru yalipokwisha, ndipo wakaambiwa kuwa watakuwa wakilipwa posho ya Shilingi 50 kwa mwezi. Baada ya miezi mingi kupita, akaja Mzee Andrew Shija akashangaa kuwaona wakizagaa nje ya ofisi.
Akatoa amri wapelekwe Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wakafunzwe nidhamu.
“Tukapelekwa kambi ya JKT Ruvu tukiwa na Hassan Dalali na Dk. Charles Kimei,” anasema Kalala.
Baadaye walipelekwa mpakani mwa Tanzania na Uganda vitani, ambavyo hata hivyo hawakupigana vita. Waliporejea wakatunga wimbo unahusu kifo cha marehemu Abeid Amani Karume.
Mgeni wa heshima siku hiyo alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu, Rashid Mfaume Kawawa na Makamu wa Rais wa Kenya, Daniel Arap Moi.
Mzee Kawawa akafurahishwa na muziki waliuporomosha siku hiyo, ndipo alipouliza hawa vijana wanatokea wapi.
Alipewa majibu, akatoa maelekezo ya kuanzishwa bendi ya Vijana Jazz.
Baada ya kuanzishwa bendi hiyo, mwisho wa mwezi ulipofika walienda katika ofisi za Chama iliyopo Mtaa wa Patrice Lumumba, jijini Dar es Salaam wakaanza kulipwa posho ya Shilingi 150 kutoka Shilingi 50 za awali.
Kiwango hicho kilikuwa ni kikubwa sana kwa matumizi ya kawaida wakati huo.
Mwaka 1974/75 wakatoka na wimbo ‘Kuruka Ukuta’ uliotungwa na Hemedi Maneti, aliyejiunga akitokea Morogoro. Kalala akatunga wimbo wa Magdalena nipeni pole. Wakenya waliusikia wimbo huo wakaupenda sana. Akaja Mkenya aliyejulikana kwa jina la Oluochi Kanindo, akawaomba kwenda Kenya kurekondi nyimbo zao kwenye kampuni yake huko Nairobi.
Ofa ya kurekodi
Mwaka 1977 Kalala akaihama Vijana Jazz na kutua UDA Jazz.
Akiwa na bendi hiyo kuna siku alikutana na Mzee Ambros Mbura aliyekuwa mmiliki wa Bendi ya Super Matimila. Akamwambia aende katika Hoteli ya Kilimanajaro akiwa na Maneti kwa ajili ya mazungumzo.
Mazungumzo hayo yakafikia mwafaka wa kuondoka kwenda Songea kujiunga katika Bendi ya Super Matimila. Kufuatia barabara ya kuwa mbaya, Mzee Mbura aliwakodia ndege lakini Maneti hakuweza kwenda kwani hadi ndege inapaa angani, alikuwa hajafika uwanja wa ndege.
Mkataba wake na Mzee Ambrose ulikuwa mnono, lakini akachukua wa miaka miwili hadi 1979 akamaliza mkataba wake. Mwaka 1979 wakati wanajeshi wa JWTZ wanarejea kutoka vitani Uganda, akatengeneza wimbo uitwao Mchakamchaka.
Baadaye Komando Kalala akarudi jijini Dar es Salaam, baada ya kuhitajika tena na UDA Jazz ndipo akajiunga nayo kwa mara nyingine tena na kubuni mtindo wa ‘Bayakanta’.
Mwaka 1981 Bendi ya Matimila ikahamia Dar es Salaam, ndipo Mzee Ambrose akamtaka Hamza Kalala arudi kwenye bendi yake.
Maslahi yaliyokuwa mazuri, yakamshawishi kuondoka UDA Jazz, akaenda kujiunga na Super Matimila hadi mwaka 1981, akishirikiana vyema na Dk. Remmy Ongala, Skassy Kasambula na Kasaloo Kyanga.
Mwishoni mwa mwaka huohuo alifuatwa na Kapteni Mchunga aliyefuatana na Maneti wakimtaka afike Ofisi ya Umoja wa Vijana.
Kalala akaambiwa kuwa aliyekuwa mpiga gitaa la solo wa bendi hiyo Hassan Daalali ameondoka.
Hivyo wakamtaka ashike nafasi yake na kuwa kiongozi wa bendi ya Vijana Jazz. Mwaka 1982 akajiunga rasmi Vijana Jazz, akatoka na wimbo wa Maisha ya Amba.
Maisha ya ndoa
Miaka ya 1985 hadi 1988 Vijana Jazz ikatoka na Mitindo ya Takatuka, Hekaheka na Pambamoto. Wimbo wa sifa za Stella aliutunga mahsusi ikiwa ni njia ya kumshawishi mkewe ambaye wakati huo alikuwa mwanafunzi wa chuo mjini Morogoro ili kufunga naye ndoa. Kalala alifanya hivyo kutokana na mkewe huyo nyumbani kwao kuwa geti kali. Stella ni binti wa aliyekuwa Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Momose Cheyo ‘Mzee Mapesa’. Stella alivutika na kuwa mpenzi wake hadi kufunga naye ndoa na kupata watoto wawili ambao nao wamefuata nyayo za baba yao.
Watoto hao ni Toto Kalala na Kalala Junior. Kalala Komando anao watoto wengine wawili wa kike.
Mwaka 1988 Komando Kalala alijiunga katika Bendi ya Washirika Tanzania Stars ‘Watunjatanjata’.
Wakiwa na bendi hiyo walitoka na vibao vya Mandela Mwana wa Afrika, Nimekusamehe lakini Sitakushau, Jullie ( utunzi wa Madaraka Morris) na nyingine nyingi.
Kalala alipiga muziki katika bendi hiyo kwa mwaka mmoja tu ikiwa ni njia ya kutafuta jinsi ya kujitegemea mwenyewe.
Alifanikiwa kuanzisha Bendi ya Bantu Group ambako aliwashirikisha wapiga magitaa wakiwemo kina Mangele Sange (solo), Ally Adinani, Rashid Kalala (besi na solo).
Wengine ni Bati Peter na Michael Liloko (drums), Ally Choki na Muumin Mwinjuma na Musemba wa Minyugu wakiwa ni waimbaji. Alla Mashoom (tumba).
Kwa ‘vichwa’ hivyo vilitengeneza vibao murua vilivyotikisa miji na majiji vya Baba Jenny na Suvuya wa Nimba, Nalila Masumanda na Kasimbagu na Ngozi ya Kiti moto.
Kwa mujibu wa Kalala bendi yake ya Bantu Group bado ipo, japokuwa inapungukiwa na baadhi ya vyombo vya muziki kuchakaa sana.
Anasema yupo kwenye michakato yakinifu ya kuandaa vibao vikali vitavyotikisa masikio ya wapenzi wa muziki hapa nchini kama zamani.
Aidha anadai atahakikisha weledi wake unainufaisha familiya yake na jamii kwa ujumla. Pia, Kalala ametoa ushauri kwa wanamuziki wa kizazi kipya wapige muziki live.
Kwa kumalizia makala haya nakupa sehemu ya wimbo huu aliotunga alipokuwa ya UDA Jazz: “Tulizaliwa wote kijiji kimoja,
Lakini ulishindwa kunioa kwa sababu, ulisema sina tabia nzuri eeh. Sasa nimeolewa kaka, Unaanza kuleta chokochoko, kujifanya wewe unazo pesa nyingi univurugie. Wenyewe tumetulia. Kama ni tabu ni zetu, Kama unachoringia ni pesa kaka, Pesa si msingi.
Kutokana na mpangilio wa vyombo, sauti na mashairi zilivyosikika katika wimbo huu, hapana shaka msomaji wa makala haya utaungama kuwa Kalala ni ‘moto wa kuotea mbali’.
Kalala katika tasnia ya muziki wa dansi, wapenzi wa muziki huo wamempachika majina bandia kama vile Mzee wa Madongo na Komando.
Kila la heri Komando Hamza Kalala, dumisha utamaduni wetu.
Mwandishi wa makala haya ni mahiri katika habari za muziki wa dansi, anapatikana kwa namba 0784/0767/0713 na 0736-331200.