Habibu Kinyogoli afariki dunia akiacha pigo kwenye ngumi
Muktasari:
- Agosti mwaka huu, Kinyogoli ambaye hadi anafariki alikuwa na umri wa miaka 78, alifanya mahojiano maalum na Mwananchi Digital na kusema kuwa angefanya kazi ya ukocha wa ngumi hadi umauti utakapomfika.
Mchezo wa ngumi nchini umepata pigo kufuatia kifo cha kocha mkongwe na bondia mstaafu Mzee Habibu Kinyogoli.
Kinyogoli amefariki usiku wa kuamkia leo Jumanne, Novemba 17, 2026 baada ya kupata ajali ya gari katika eneo la Tabata Mataa.
Bado taarifa kamili kuhusu mazishi yake haujatolewa na familia yake.
Hadi anakutwa na umauti, Kinyogoli alikuwa Kocha wa Bondia wa Ngumi za kulipwa, Ibra Classic.
Agosti mwaka huu, Kinyogoli ambaye hadi anafariki alikuwa na umri wa miaka 78, alifanya mahojiano maalum na Mwananchi Digital na kusema kuwa angefanya kazi ya ukocha wa ngumi hadi umauti utakapomfika.
Kauli hiyo ya Marehemu Kinyogoli imetimia miezi mitatu baadaye baada ya ajali kukatisha uhai wake.
Alinukuliwa akisema kuwa licha ya umri wake mkubwa, bado alikuwa na ndoto ya kuhakikisha anawatengenea vijana wengi ili waje kuwa mabondia wakubwa na kuipeperusha vema bendera ya Tanzania nje ya mipaka.
“Sina mpango wa kuacha kufundisha ngumi kwa sababu ya umri, labda niugue maradhi yatakayonifanya nishindwe kufanya kazi yangu au umauti utakaponikuta.
“Mimi sina kazi nyingine ya kufanya zaidi ya hii na kwa hakika naifurahia, niache ngumi ili nifanye nini, vijana bado wanahitaji mafunzo yangu.
"Kwanza michezo ni afya, hivi unavyoniona ni kwasababu ya kushiriki mazoezi, kama ningekuwa sijishughulishi afya yangu ingekuwa imetetereka,” alinukuliwa Kinyogoli.