Greatlakes Freight & Transport yadhamini waogeleaji kusaka tiketi ya Olimpiki

Waogeleaji wa Tanzania Hilal Hilal, Austin Okore na Collins Saliboko wakiwa nchini Afrika Kusini tayari kwa mafunzo ya kuogelea ya Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea la Afrika (Cana) na baadaye kushindana kuwania nafasi ya kufuzu mashindano ya Olimpiki Mei 7 na 8.

Dar es Salaam. Kampuni ya Greatlakes Freight & Transport imepiga tafu waogeleaji wa Tanzania wanaowania nafasi ya kufuzu mashindano ya Olimpiki yaliyopangwa kufanyika mjini Tokyo, Japan kuanzia Julai 23 mpaka Agosti 8.

Waogeleaji hao wawili, Collins Saliboko na Hilal Hilal wamechagulia na chama cha kuogelea Tanzania (TSA) kusaka tiketi ya kufuzu mashindano ya Olimpiki yaliyopangwa kufanyika  Mei 7 na 8 mjini Stellenbosch, Afrika Kusini.

Wakati Collins amedhaminiwa kuanzia mazoezi ya gym na kwenye maji, Hilal ambaye alikuwa mazoezini Dubai, amedhaminiwa tiketi ya kwenda Afrika Kusini kushiriki katika mashindano hayo.

Iwapo watafuzu, waogeleaji hao watashiriki katika mashindano hayo ya Tokyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Greatlakes Freight & Transport Fahmy Ahmed alisema jana kuwa wameamua kusaidia mchezo wa kuogelea ili kuleta hamasa  katika mchezo huo na maendeleo kwa vijana.

Fahmy alisema kuwa wamedhamini waogeleaji hao kama sehemu ya kampuni kujihusisha na shughuli za kijamii, kuendeleza vipaji vya vijana wa leo na kuhamasisha mchezo huo.

Pia wanahamasisha makampuni mengine kuwaunga mkono vijana wetu, ili waweze kupeperusha bendera ya Tanzania bila vikwazo na mawazo yanayoweza sababishwa na upungufu wa mazoezi na vifaa stahiki.

Alisema kuwa mchezo wa kuogelea una vipaji vingi nchini na pia ni mchezo ambao unatazamwa zaidi katika mashindano ya Olimpiki.

Kwa hapa nchini, mchezo huo unashindwa kuendelea kutokana na kukosa sapoti kutoka kwa jamii na hasa udhamini.

“Makampuni mengi  yanapendelea zaidi kudhamini michezo maarufu, kama mpira wa miguu na ngumi na kuona mchezo wa kuogelea hauna tija na wala haufahamiki. Amewashauri watu kuweka bidii kwenye mchezo huu kwa kuwa una waogeleaji wengi ambao wanaweza kuitangaza nchi nje ya mipaka yake.

Kwa upande wake, makamu mwenyekiti wa TSA, Asmah Hilal aliipongeza kampuni hiyo kwa msaada mkubwa na kuwawezesha waogeleaji hao kujiandaa na kwenda kushindana kuwania nafasi ya kufuzu Olimpiki.

Asmah pia alitoa shukrani kwa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) na dula la kuuza vifaa vya michezo la  Just Fit kwa kusaidia waogeleaji hao.

Asmah alisema kuwa waoegeleaji walikuwa njia panda kwenda kushiriki katika mashindano hayo ambayo ni muhimu kwa ajili ya kutafuta nafasi ya kufuzu.

“Kwa niaba ya TSA, napenda kutoa shukrani kwa kampuni ya Greatlakes Freight & Transport kuweza kusaidia waogeleaji wetu. Kwa kweli tulikuwa njia panda na ujio wao dakika za mwisho umesaidia kufanikisha safari yao,” alisema Asmah.

Waogeleaji hao wameongozana na kocha Alex Mwaipasi ambapo watapata mafunzo na mwenyekiti wa kamati ya ufundi ya Shirikisho la mchezo huo duniani (FINA), Graham Hill kabla ya mashindano rasmi.

Pia yupo muogeleaji chipukizi, Austin Okore wa klabu ya Dar Swim Club ambaye atahudhuria mafunzo ya kunoa kipaji chake.
Mafunzo hayo yamedhaminiwa na shirikisho la mchezo huo barani Afrika (CANA)ambayo  inalipia gharama za kulala, chakula na masuala mengine muhimu kwa kila muogeleaji.