Goba Hills Marathon kufanyika Januari 23
Muktasari:
- Klabu ya riadha ya Goba Roads Runners (GRR), imetangaza rasmi maandalizi ya mashindano hayo, ambayo mwaka huu yamebeba kaulimbiu ya ‘Run Beyond Hills’, inayolenga kuendeleza utamaduni wa riadha, kuhamasisha maisha yenye afya na kuunganisha jamii kupitia michezo.
MASHINDANO ya Goba Hills Marathon 2027, yatafanyika Januari 23, 2027 katika viwanja vya Shule ya Sekondari Goba, Dar es Salaam, huku yakitarajiwa kuwakutanisha wakimbiaji kutoka makundi mbalimbali katika msimu wake wa nane.
Klabu ya riadha ya Goba Roads Runners (GRR), imetangaza rasmi maandalizi ya mashindano hayo, ambayo mwaka huu yamebeba kaulimbiu ya ‘Run Beyond Hills’, inayolenga kuendeleza utamaduni wa riadha, kuhamasisha maisha yenye afya na kuunganisha jamii kupitia michezo.
Katibu Mkuu wa Goba Roads Runners, Similwa Mdumbwa, amesema maandalizi ya mashindano hayo yameanza rasmi na klabu inatarajia kuona mwitikio mkubwa kutoka kwa wakimbiaji, klabu za riadha, familia na wananchi kwa ujumla.
Mdumbwa amesema msimu huu umeandaliwa kwa kuzingatia makundi mbalimbali ya washiriki ili kutoa nafasi kwa watu wa rika tofauti kushiriki na kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi.
Amesema kutakuwa na vipengele vinne vya mbio, ambavyo ni kilomita 2.5 kwa watoto, kilomita tano, kilomita 10 na nusu marathon ya kilomita 21.
Washiriki watatakiwa kulipa Sh45,000 kwa ajili ya ushiriki wao katika mashindano hayo.
Amesema kaulimbiu ya mwaka huu ya ‘Run Beyond Hills’ ina maana pana zaidi ya kushiriki mbio zinazopitia vilima vya Goba, kwani inalenga pia kuhamasisha watu kutambua fursa zilizopo katika jamii zao na umuhimu wa kujituma katika kufikia malengo mbalimbali.
Mbali na ushindani wa riadha, Mdumbwa amesema Goba Hills Marathon imeendelea kuwa sehemu ya jitihada za klabu kutumia michezo kuchangia maendeleo ya jamii, hususan katika kuboresha afya ya mama na mtoto.
Amesema kupitia mashindano hayo, klabu inaendelea kuunga mkono juhudi za kuboresha mazingira na huduma za kujifungulia katika vituo vya afya vilivyopo Kata ya Goba.
Lengo ni kusaidia kuwepo kwa mazingira salama na rafiki kwa akina mama wakati wa kujifungua, pamoja na kuboresha huduma zinazotolewa kwa mama na mtoto.
Kwa mujibu wa klabu hiyo, kufanyika kwa mashindano hayo kwa msimu wa nane kunaonesha dhamira yake ya kutumia riadha kama nyenzo ya kuhamasisha afya, mshikamano na maendeleo ya jamii.
Mdumbwa pia amezialika kampuni, taasisi na wadau wa sekta binafsi kuungana na klabu kufanikisha mashindano hayo kupitia udhamini, ufadhili na aina nyingine za ushirikiano.
Amesema ushiriki wa wadau ni muhimu katika kukuza mashindano hayo na kuongeza mchango wake katika jamii, huku ukiwapa nafasi taasisi mbalimbali kuonesha dhamira yao katika kuendeleza michezo na afya.