Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

FVS Yamliza kocha Mashujaa FC

AMANI PIct
AMANI PIct

Muktasari:

  • Mashujaa ilipoteza kwa mabao 2-1, mechi ya Ligi Kuu Bara, Novemba 22, 2026 kwenye Uwanja wa Bukombe mkoani Geita.

KOCHA wa Mashujaa, Amani Josiah, ameeleza kutoridhishwa na matumizi ya Mfumo wa Usaidizi wa Waamuzi (FVS) katika mchezo dhidi ya Geita Gold, akidai kikosi chake hakikupata nafasi ya kunufaika na mfumo huo katika matukio muhimu kutokana na changamoto za kiufundi.

Mashujaa ilipoteza kwa mabao 2-1, mechi ya Ligi Kuu Bara, Novemba 22, 2026 kwenye Uwanja wa Bukombe mkoani Geita.

Pamoja na kukiri kikosi chake kilifanya makosa yaliyochangia kipigo hicho, Josiah amedai matumizi ya FVS hayakuwa ya kuridhisha upande wao.

Kocha huyo amesema kulikuwa na matukio ambayo walihitaji kutumia mfumo huo ili kupata mapitio ya uamuzi wa mwamuzi, lakini waliambiwa kulikuwa na hitilafu za kiufundi. Hata hivyo, alidai mfumo ulifanya kazi vizuri pale wenyeji walipouhitaji.

“Tulikuwa hatuna bahati na FVS. Kuna wakati tulipotakiwa kuitumia kwenye matukio ambayo tungeweza kunufaika nayo, tuliambiwa mfumo umepata shida. Lakini ulipotakiwa kutumiwa na wenyeji, ulifanya kazi,” amesema Josiah.

AMA 01

Licha ya kutoridhishwa na matumizi ya mfumo huo, Josiah amekiri Mashujaa pia ilijichangia katika kupoteza mchezo huo, hasa kutokana na kushindwa kutumia nafasi za kufunga na kufanya makosa katika safu ya ulinzi.

Amesema walikwenda Geita wakiwa na dhamira ya kuondoka na pointi tatu, lakini washambuliaji walishindwa kutumia vizuri nafasi walizotengeneza, hali iliyowafanya washindwe kufikia lengo lao.

“Tulijipanga kupata ushindi, lakini kwa bahati mbaya tulishindwa kutumia nafasi tulizopata. Kuna wakati tulikuwa na nafasi nzuri za kufunga, lakini hatukuzitumia vizuri,” amesema.

Josiah alibainisha pamoja na tatizo la umaliziaji, makosa katika eneo la ulinzi yaliwapa Geita Gold nafasi ya kujenga mashambulizi na kuyatumia kupata matokeo, hivyo akasisitiza umuhimu wa kuyafanyia kazi upungufu huo.

“Vilevile tulifanya makosa rahisi ambayo yaliwaruhusu Geita kujenga mashambulizi yao. Hayo ni mambo ambayo tunapaswa kuyafanyia kazi kwa sababu kwenye michezo ya aina hii makosa madogo yanaweza kukugharimu matokeo,” amesema.

AMA 02

Kipigo hicho kimeifanya Mashujaa kuendelea kukabiliwa na changamoto ya kupata matokeo ya mfululizo msimu huu. Katika mechi 11 ilizocheza hadi kukutana na Geita Gold, timu hiyo ilikuwa imeshinda tano na kupoteza sita, huku mchezo wake dhidi ya Azam FC ukiwa haujachezwa kutokana na kuahirishwa.

Ushindi wake wa mechi tano umekuja dhidi ya Coastal Union (1-0), Kagera Sugar (2-1), Singida Black Stars (2-1), Polisi Tanzania (2-1) na Pamba Jiji (1-0).

Kwa upande wa vipigo, Mashujaa imeangukia mikononi mwa Singida Fountain Gate (1-0), Mbeya City (2-1), Dodoma Jiji (1-0), Simba (6-1), Yanga (2-1) na Geita Gold (2-1).

Sasa kikosi hicho kinarejea Kigoma kujiandaa na mfululizo wa michezo ya nyumbani, kikianza na TRA United Novemba 28, 2026 kabla ya kukutana na JKT Tanzania Desemba 6, 2026 na baadaye Namungo Desemba 13, 2026.

Michezo hiyo itakuwa nafasi kwa Josiah kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza dhidi ya Geita Gold na kukirejesha kikosi chake kwenye njia ya ushindi mbele ya mashabiki wake.