Futakamba matumaini kibao Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- Futakamba aliweka mabao hayo katika mchezo uliochezwa Agosti 30, 2026 na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3 kwenye Uwanja wa Mao A, Unguja.
BEKI wa kati wa timu ya Mlandege, Raphael Charles 'Futakamba' amesema amejisikia furaha baada kufunga mabao mawili katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Zanzibar dhidi ya JKU, huku akibainisha kwamba hali hiyo imempa matumaini ya kuendelea kufanya vizuri.
Futakamba aliweka mabao hayo katika mchezo uliochezwa Agosti 30, 2026 na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3 kwenye Uwanja wa Mao A, Unguja.
Beki huyo amesema aliingia kwenye mchezo huo kwa lengo la kuisaidia timu kupata ushindi, lakini kwa bahati mbaya hawakufanikiwa ingawa kwa upande wake mabao aliyofunga yanampa matumaini ya kufanya vizuri zaidi.
"Mlinzi wa kati kwa kawaida ana majukumu makubwa ya kuisaidia timu iwe kulinda tusifunge au hata kwenda kuongeza kasi ya mashambulizi ndio maana ninahakikisha hilo linawezekana kila mechi," amesema.
Mbali na hilo, amesema pointi moja waliyoipata kupitia mchezo huo imewaamsha kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi michezo ijayo.
Mlandege jana Ijumaa ilikuwa na mechi ya pili ya Ligi Kuu Zanzibar dhidi ya Polisi Zanzibar kwenye Uwanja wa Mao A, Unguja.