Fountain Gate yakwama Lindi
Muktasari:
- Bao pekee la kiungo mshambuliaji wa Namungo, Herbert Lukindo ndilo lililodumu hadi dakika ya 90 na kuisaidia timu hiyo kunufaika na uwanja wake wa nyumbani.
BAADA ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Fountain Gate kwenye Uwanja wa Majaliwa, mkoani Lindi, Namungo FC imepanda hadi nafasi ya sita na kuishusha Singida Black Stars hadi nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Bao pekee la kiungo mshambuliaji wa Namungo, Herbert Lukindo ndilo lililodumu hadi dakika ya 90 na kuisaidia timu hiyo kunufaika na uwanja wake wa nyumbani.
Fountain Gate katika mechi tatu ilizocheza imeshinda moja ikiichapa bao 1-0 Mashujaa, kisha kufungwa mabao 4-3 na imepoteza 1-0 dhidi ya Namungo FC, huku Namungo, imeshinda mechi mbili kati ya tatu dhidi ya Geita Gold bao 1-0, imefungwa 3-1 dhidi ya Yanga na imeshinda 1-0 dhidi ya Fountain Gate.
Msimu uliopita Februari 4 Fountain Gate ikiwa mwenyeji wa mechi dakika 90 zilimalizika kwa sare ya bao 1-1, hivyo iligawana pointi moja moja na Namungo na mzunguko wa pili zilipokutana Juni 27, Uwanja wa Majaliwa, zilitoka suluhu.
Kwa matokeo ya leo Agosti 25 2026 Fountain Gate imeendelea kusalia nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa imeshinda mechi moja na kufungwa mbili na rekodi zinaonyesha zimekuwa na ushindani mkubwa licha ya kutokufungana mabao mengi tangu msimu uliopita.