Fifa waiuzia Yanga kesi ya Asamoah

kenneth asamoah
MWANDISHI WETU SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa) limerudisha majibu ya Yanga kuhusu utata wa mchezaji wao mpya na kusema: " Yanga acheni kujichanganya kuhusu Kenneth Asamoah kwani kosa ni lenu wenyewe." Yanga imekuwa ikilalamika kuwa wamekuwa wakiwekewa zengwe kuhusu mshambuliaji huyo, lakini Fifa imeitia hatiani klabu hiyo. Mshambuliaji huyo wa Ghana ambaye amejiunga na Yanga msimu huu akitokea FK Jagodina ya Serbia ameshindwa kucheza mechi yoyote ya ligi kwa sababu usajili wake bado haujakamilika. Baada ya usajili wake kukwama kwa muda mrefu, Yanga iliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuulizia swala hilo Fifa kujua tatizo kuhusu mchezaji huyo. Katika mfumo mpya wa usajili ambao hufanywa kwenye mtandao maalumu wa intaneti, Fifa ilifuatilia kwa makini suala hilo na kugundua kuwa Yanga ilikuwa imeweka baadhi ya kumbukumbu za mchezaji huyo kimakosa. Habari za ndani ambazo pia zimethibitishwa na TFF zinasema kuwa katika aina hiyo ya usajili wa kwenye mtandao, klabu mbili zinapaswa kukubaliana kabla ya kuanza kuweka kumbukumbu za mchezaji husika kwenye intaneti na inabidi kusiwe na tofauti. Habari zinasema kuwa wakati klabu hizo mbili zikiweka taarifa katika mtandao huo ikiwa ni pamoja na mkataba, TFF, Chama cha Soka Serbia na Fifa nao huwa wanaona kila kinachoendelea. Habari hizo zinasema kuwa Fifa imegundua kuwa kumbukumbu ambazo zimewekwa na Yanga kwenye mtandao kuhusu mchezaji huyo zinatofautiana na zile ambazo zimewekwa na klabu yake ya zamani ya Jagodina. Ofisa Habari wa TFF, Florian Kaijage alithibitisha kuwa matatizo makubwa ni mawili, kwani Yanga imelikosea jina la Asamoah na pia wameandika kuwa mkataba wake na Yanga ulitakiwa kuanza Julai 30 wakati Jagodina wameandika mkataba huo ungeanza Agosti Mosi. Kaijage alisema pia kuna jambo jingine ambalo Yanga waliliweka tofauti na klabu ya Jagodina na ndio maana usajili huo wa Asamoah umekuwa ukikwama kukamilika kwenye mtandao wa komputa. Kaijage alisema Yanga inatakiwa kurekebisha kasoro hizo na kuzungumza na Jagodina ili waweke kumbukumbu zinazofanana katika mfumo huo wa kompyuta. Fifa imeanzisha usajili wa Transfer Matching System (TMS) ili kujua kumbukumbu ya wachezaji wote duniani na jambo la muhimu ni pande zote zinazohusika kuweka kumbukumbu zinazofanana kwenye mtandao vinginevyo mfumo mzima 'hugoma'. "Inaniuma sana kukosa mechi za ligi kutokana na kuchelewa ITC yangu lakini nadhani hii wiki ikiisha kila kitu kitakamilika," alisema Asamoah. Kocha wa Yanga Kosta Papic alisema jana Ijumaa kuwa; "Hili suala la Asamoah linachanganya sana lakini nadhani ni mambo madogo tu ya kibinadamu ambayo yatarekebishwa ndani ya muda mfupi, ingawa sijawa na uhakika ni lini nitapata vibali na ruhusa ya kumtumia. "Kumkosa mchezaji muhimu kama huyo inavuruga utaratibu wangu kwavile nilikuwa nimeandaa mipango yangu tangu awali lakini sina jinsi inabidi nitafute njia mbadala na nimesajili timu nzuri na kila mchezaji ana uwezo tutafanya kazi, cha muhimu ni timu ishinde na kupata pointi muhimu hayo mengine ni baadaye."