Farid Musa amuibua kocha Coastal Union
Muktasari:
- Farid, ambaye alijiunga na Coastal Union msimu huu akitokea Yanga, amekuwa akipewa muda wa kujiandaa na kurejesha utimamu wa mwili baada ya kutokuwa akipata mechi za ushindani kwa muda katika klabu yake ya zamani.
FARID Mussa anaonekana kuwa miongoni mwa silaha ambazo Coastal Union imekuwa ikizisubiri kwa hamu, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Fikiri Elias, akisema wakati umefika kwa winga huyo kuanza kuonyesha kile alichonacho na kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho.
Farid, ambaye alijiunga na Coastal Union msimu huu akitokea Yanga, amekuwa akipewa muda wa kujiandaa na kurejesha utimamu wa mwili baada ya kutokuwa akipata mechi za ushindani kwa muda katika klabu yake ya zamani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Elias amesema Farid alikuwa akifanyiwa maandalizi maalumu katika kipindi cha mwanzo ili kufikia kiwango kinachohitajika, lakini sasa anaamini mchezaji huyo anaweza kuanza kutumika zaidi na kuwa sehemu muhimu ya mipango ya Coastal Union.
“Farid alikuwa anawekwa sawa kwa sababu alitoka kwenye kipindi ambacho hakuwa anapata mechi za ushindani. Tuliona ni muhimu kumpa muda wa kujiandaa vizuri na kufikia kiwango tunachokitaka.
Kocha huyo amesema uzoefu ambao Farid amekusanya katika timu alizopita unaweza kuwa nyongeza kubwa kwa Coastal Union, hasa katika kipindi ambacho timu hiyo inahitaji wachezaji wenye uwezo wa kubadilisha mchezo.
“Farid ni mchezaji mwenye uzoefu, amepita kwenye timu kubwa na mazingira tofauti ya ushindani. Akianza kucheza kwa kiwango tunachokitarajia, atatupa kitu kikubwa ndani ya timu,” amesema.
Farid mwenyewTe tayari amewahi kueleza kuwa alipofika Coastal Union alizungumza na benchi la ufundi na kuomba muda wa kufanya maandalizi zaidi kabla ya kuanza kuipigania timu hiyo uwanjani.