Fainali ya mabingwa Ngao ya Jamii
Muktasari:
- JKT ilitinga fainali baada ya kuitandika Mashujaa bao 1-0 kwenye nusu fainali ya kwanza kabla ya Yanga Princess kutandikwa mabao 3-0 dhidi ya watani zao Simba.
LEO, Jumamosi katika Uwanja wa KMC Complex saa 10 jioni kuna mechi ya kukata na shoka, fainali ya Ngao ya Jamii inayowakutanisha mabingwa watetezi kwenye soka la wanawake, JKT Queens mabingwa watetezi wa kombe hili na Simba Queens ambao ni mabingwa wa ligi.
JKT ilitinga fainali baada ya kuitandika Mashujaa bao 1-0 kwenye nusu fainali ya kwanza kabla ya Yanga Princess kutandikwa mabao 3-0 dhidi ya watani zao Simba. Mwanaspoti linakumegea jinsi vita hizi mbili zitakavyopigwa kuanzia mbinu, ubora wa mchezaji mmoja mmoja na ushirikiano wa kitimu utakavyoamua bingwa wa mashindano hayo yaliyoanzishwa mwaka 2023 huku Simba ikibeba mara moja na JKT ikichukua mara mbili mfululizo mwaka 2024 na 2025.
JKT QUEENS VS SIMBA QUEENS
JKT Queens walitinga hatua hiyo kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa Queens. Mchezo huo ulionyesha ugumu wa JKT kwenye safu ya ulinzi lakini pia ukiacha maswali kwenye ufanisi wa safu yao ya usambuliaji. Kwa upande mwingine, Simba Queens ilionyesha ubora mkubwa baada ya kuichapa Yanga Princess kwa kichapo cha mabao 3-0 katika ‘Kariakoo Derby’, wakionyesha soka la kasi, ufundi wa hali ya juu na matumizi mazuri ya nafasi.
NINI CHA KUFANYA?
JKT Queens katika mchezo wao dhidi ya Mashujaa, JKT walitengeneza nafasi nyingi kipindi cha kwanza kupitia kwa Bahati Kizanguzi, Asha Rashid na Happiness Mwaipaja lakini wakakosa utulivu kwenye umaliziaji.
Bao moja lilipatikana kipindi cha pili mara baada ya kuingia kwa nyota Fatma Muhibu aliyeleta mabadiliko ya haraka na kufunga kwa ufundi binafsi. JKT inapaswa kuongeza ufanisi eneo la mwisho, Simba Queens sio timu itakayoruhusu nafasi tano au sita bila kukuadhibu. JKT wanapaswa kuhakikisha nafasi chache watakazozipata kupitia kwa Kizanguzi na Fatma Said zinageuzwa kuwa mabao. Kuziba Mianya ya Kiungo, Simba wana viungo wenye uwezo mkubwa wa kumiliki na kupanga mashambulizi wakiongozwa na Viviane Corazone na Elizabeth Joseph. Kiungo cha JKT lazima kinase pasi hizi mapema ili kuzuia Simba wasipate mpira kwa urahisi kwenye eneo la hatari.
Nidhamu ya Ulinzi: mabeki wa JKT, Ester Maseke, Anastazia Katunzi wakiongozwa na mlinda mlango Hawa Athman unapaswa kuwa makini dhidi ya kasi ya mashambulizi ya kushtukiza ya Simba hasa upande anaocheza Mary Siyame na Aisha Mnunka ambao wote wana kasi pembeni.
SIMBA
Simba walionyesha utulivu mkubwa wa kimbini na udhibiti wa mchezo dhidi ya Yanga Princess. Magoli kutoka kwa Viviane Corazone Odhiambo, Senaf Demise na Mary Siyame yalithibitisha safu yao ya usambuliaji ilivyo na makali na mchanganyiko wa uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na ushirikiano wa kitimu. Simba inapaswa kutumia kasi Pembeni: Simba wanatakiwa kuendelea kutumia mashambulizi kupitia pembezoni mwa uwanja ili kuivuta safu ngumu ya ulinzi ya JKT.
Kuzuia mipira ya juu na mashambulizi ya kushtukiza: JKT ni timu yenye wachezaji wenye nguvu na pumzi ya kutosha na mara nyingi wanatumia mpira wa haraka kufika langoni.
Simba wanatakiwa kuzuia faulo zisizo za lazima karibu na eneo lao la hatari, kudumisha nidhamu ya mchezo kutojiamini kupita kiasi kutokana na ushindi wa 3-0 dhidi ya Yanga. JKT Queens ni mabingwa watetezi na wana uzoefu mkubwa wa mechi za fainali.
MSHINDI WA TATU
Kabla ya fainali itatangulia mechi ya mshindi wa tatu kati ya Yanga na Mashujaa. Hii ni moja ya mechi nzuri ya kutazama kutokana na ushindani mkubwa ulioonyesha kwa timu zote mbili. Mchezo huu unakutanisha timu mbili zilizotoka kuumia kwenye hatua ya nusu fainali. Yanga Princess walionekana kuchanganyikiwa dhidi ya Simba hasa baada ya kiungo wao Ritticia Nabossa kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 37, jambo lililovuruga kabisa mipango yao ya kiufundi na mbinu za ukabaji. Mashujaa Queens, licha ya kufungwa 1-0 na JKT, walionyesha nidhamu nzuri ya kuzuia wakiongozwa na kipa wao Gelwa Yona pamoja na mashambulizi ya kushtukiza kupitia kwa Zainab Ali na Neema Kiniga.
Yanga Princess chini ya Kocha Edna Lema, Wanayanga wanahitaji kurejesha saikolojia ya wachezaji wao na kucheza kwa utulivu mkubwa. Wanapaswa kurekebisha makosa ya safu yao ya ulinzi iliyokuwa inaruhusu mashambulizi mara kwa mara kwenye mchezo wa Simba. Mashujaa Queens: Mashujaa wataingia kwenye mchezo huu wakiwa hawana presha kubwa. Kama watasalia na nidhamu yao ya kuzuia kama walivyofanya dhidi ya JKT na kutumia udhaifu wa kiakili wa Yanga, wana nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kupitia mashambulizi ya kasi ya kushtukiza kupitia kwa Kiniga ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa Yanga.
WASIKIE MAKOCHA
Kocha Mkuu wa Mashujaa Queens, Rajab Ally anasema: “Tunajua tunakwenda kucheza mechi ngumu dhidi ya Yanga kwa maandalizi tuliyoyafanya tunayo nafasi ya kufanya vizuri.”
Kocha wa JKT, Kessy Abdallah anasema: “Tulichokifanya kwenye nusu fainali tutakwenda kukiongeza zaidi kwenye fainali kutokana na kwamba zinakutana timu ngumu zenye ushindani mkubwa hivyo tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunatetea taji letu ingawa haitakuwa rahisi.”