Eti! Ronaldo mkubwa kuliko Real Madrid
Muktasari:
Ukweli ni kwamba sio kitu rahisi sana kuziba pengo la mchezaji mkubwa kama Ronaldo kwa kufuata tu kauli hii. Real Madrid wanateseka kwa sasa
MCHEZAJI wa Kidachi aliyeitwa, Pierre van Hooijdonk nakumbuka aliwahi kuiambia klabu yake ya Nottingham Forest kwamba alikuwa mkubwa kuliko klabu yake. Nilishangaa lakini ndivyo alivyojisikia kusema. Usingeweza kumzuia.
Aliyasema hayo huku katika historia alishangaza kwa sababu imezoeleka kuanzia kwa mashabiki, wachezaji, viongozi wa klabu na kila mtu anaamini kwamba ‘hakuna mchezaji mkubwa kuliko klabu husika’. Tumejizoeasha hivyo.
Hata hivyo, Van Hooijdonk anafikirisha. Ni kweli hakuna mchezaji mkubwa kuliko klabu? Ni kweli. Kwa maana ya historia wachezaji hupita lakini klabu inabaki. Hata hivyo, kuna wachezaji ambao wakiondoka, ndani ya uwanja klabu inayumba.
Huyu hapa Cristiano Ronaldo. Ameondoka zake Santiago Bernabeu. Timu inayumba uwanjani. Hauwezi kusema kwamba Ronaldo alikuwa mkubwa kuliko Real Madrid. Kabla yake waliwahi kuwepo akina Alfredo di Stefano, Ferenc Puskas, Roberto Carlos, Ronaldo de Lima, Luis Figo na wengineo.
Enzi za akina Di Stefano Real Madrid waliwahi kuchukua ubingwa wa Ulaya mara tano mfululizo. Kuanzia mwaka 1956 mpaka 1960. Haikuonekana kama kungeweza kuwa na Madrid iliyo kubwa tena baada ya wao kuondoka. Lakini sasa Madrid wana mataji 13 ya Ulaya. Kuanzia hapo, baada ya kuondoka kwa akina Di Stefano wamechukua mataji nane zaidi.
Kwa mifano hii unaweza kuamini kwamba usemi wa ‘hakuna mchezaji mkubwa kuliko klabu’ unaweza kufanya kazi kwa urahisi. Ukweli ni kwamba sio kitu rahisi sana kuziba pengo la mchezaji mkubwa kama Ronaldo kwa kufuata tu kauli hii. Real Madrid wanateseka kwa sasa.
Ni kweli kwamba Ronaldo sio mkubwa kuliko Real Madrid lakini kuondoka kwake kunamaanisha kwamba, Madrid watapitia mchakato wa muda mrefu wa kuziba pengo lake ndani na nje ya uwanja. Haiwezi kuwa kazi ya msimu mmoja.
Kuwepo kwa Ronaldo uwanjani kulikuwa kunawafanya makocha wengi wa timu pinzani watumie ubao wao wa kufundishia kuwaelekeza namna ya kuwakaba Madrid, na hasa Ronaldo. Akili ya pili ndio inakwenda uwanjani kutafakari namna ya kushinda. Akili ya kwanza ni namna ya kumzuia Ronaldo. Ukienda na akili ya kumzuia Ronaldo asifunge tayari inamaanisha kwamba una hofu. Waingereza wanaita Fear factor. Wakati mwingine hofu inakwenda hata katika siku ambayo Ronaldo hayupo fomu. Hii haitokei kwa Ronaldo tu. Inatokea pia kwa Lionel Messi. Sio mara zote anacheza vizuri, lakini uwepo wake tu uwanjani unasababisha hofu kwa adui.
Hiki ndio kitu ambacho Real Madrid wanakikosa kwa sasa. Kwa mfano, kama Messi hachezi upande wa Barcelona kuna maadui kama akina Valencia hawahisi tofauti kubwa baina yao na Barcelona. Hapo hofu inakuwa imeondoka.
Madrid watateseka hii kitu kwa muda mrefu wakati wakijaribu kuunda timu yao upya katika misingi mingine. Hadi wapate suluhisho tayari klabu nyingi zitakuwa zimefanikiwa kupata ushindi dhidi ya wababe hawa wa Bernabeu.
Sio lazima wapate staa mkubwa mwenye hadhi ya Ronaldo lakini wanaweza pia kuiunda timu yao katika namna ambavyo Manchester City na Liverpool wameziunda timu zao. Ukienda Etihad au Anfield hakuna Messi wala Ronaldo, lakini kuna mgawanyiko mkubwa wa majukumu kwa mastaa wenye uwezo mkubwa na ambao bado wapo chini ya Messi na Ronaldo.
Madrid watarudi kivingine, tena wakiwa tishio. Jina lao litaendelea kuwa kubwa maradufu, lakini huwa haitokei muda mchache baada ya kuondoka kwa mchezaji kama Ronaldo. Wachezaji wa aina hii wanazaliwa mara moja baada ya miaka mingi. Timu inahitaji kujipanga upya na kwa staili tofauti kuweza kuziba pengo lake.
Lakini subiri. Si wanasema pia hakuna kocha mkubwa kuliko klabu? Kuanzia mwaka 2013 Manchester United haijachukua ubingwa wa Ligi Kuu ya England tangu walipochukua mara ya mwisho na Sir Alex Ferguson. Tatizo liko wapi?
Hofu ya uwepo wa Ferguson katika benchi la Manchester United imeondoka. Licha ya uwezo wake lakini kivuli chake katika benchi kilikuwa kinawatisha hata waamuzi. Mwenyewe amewahi kukiri jinsi alivyokuwa anawaburuza waamuzi kwa kuwatia hofu.
Historia yake nene katika soka ikawafanya wapinzani waamini kwamba ‘ni ngumu kuifunga timu ya Ferguson’. Leo uwezo wake haupo tena katika benchi, lakini hata kivuli chake kilichokuwa kinawatisha nacho hakipo. Makocha wengine waliokwenda pale hawakuwa na sauti kubwa tena kama ilivyokuwa kwa Ferguson. Hata zile penalti za ajabu ajabu zimetoweka Old Trafford.
Turudi kwa Ronaldo. Hili ni angalizo kwa Barcelona na Messi wao. Maisha hayatakuwa rahisi sana pindi Messi akiondoka. Kuna watu watakuwa wanakwenda Nou Camp wakiwa na kiburi cha kushinda mechi. Kwa sababu wanakwenda na hofu.
Nawaonea huruma Real Madrid. Nitarudi hapa wiki ijayo au wiki chache zijazo. Nitakuja kwa ajili ya kumjadili zaidi Zidane na kuyumbayumba kwa Madrid kunakoendelea. Lakini Ronaldo ilikuwa kesi maalumu zaidi kwa sababu mashabiki wamekuwa wakijichanganya na kauli hii. Kwamba hakuna mchezaji mkubwa kuliko klabu. Ukweli ni kwamba wachezaji wa aina hii wapo ingawa hali hii haidumu kwa muda mrefu. Inahitaji muda mrefu kuondoa vivuli vyao katika klabu.
Haiwezekani mchezaji aliyekuwa anafunga mabao 50 kwa msimu aondoke na tofauti isiwepo. Lazima itakuja tofauti ya wazi zaidi. Kuanzia kupungua kwa idadi ya mabao hadi kupungua kwa hofu katika vifua vya wachezaji wa timu pinzani.
Hata hizi timu kubwa kuna wakati zilipitia vipindi virefu vya ukame wa mataji kwa sababu kuna baadhi ya vizazi vyao viliondoka na wakalazimika kurudi kivingine.