Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Enzi za ubabe wa Manchester United zimepita

Muktasari:


Kama si Mourinho na hamasa aliyoingia nayo katika Ligi Kuu England kiasi cha kuiibua Chelsea ikaanza kupumulia kisogoni mwa timu kubwa kama Manchester United na Arsenal, burudani ya soka inayohusishwa naye isingekuwa jinsi ilivyo sasa.

MWANDISHI yeyote wa soka hawezi kufurahia kuondoka kwa kocha mashuhuri, tena kinara, kama Jose Mourinho.
Katika muongo mzima uliopita, Mourihno amekuwa mtu muhimu sana katika soka la England na Ulaya na bado ameendelea kuwa hivyo hadi wiki iliyopita alipofukuzwa.
Ingawa Manchester United wamejikuta wakiwa nyuma ya jirani zao na mahasimu wao Machester City katika miaka ya hivi karibuni, hasa katika masuala ya dimbani, tunapotazama maeneo mengine, mambo ni tofauti kabisa.
Moja ya mambo muhimu yasiyosahaulika kuhusu Mourinho ni uwezo wake wa kuburudisha waandishi na wapenzi wa soka kwa kutoa majibu yenye burudani, akijibu maswali ambayo si kila kocha angependa kuyajibu.
Kama si Mourinho na hamasa aliyoingia nayo katika Ligi Kuu England kiasi cha kuiibua Chelsea ikaanza kupumulia kisogoni mwa timu kubwa kama Manchester United na Arsenal, burudani ya soka inayohusishwa naye isingekuwa jinsi ilivyo sasa.
Bahati mbaya, hakuweza kudumisha makali hayo katika kipindi alichokaa na Manchester United ambayo nayo aliipokea ikiwa tayari imenyong’onyea.
Tangu Sir Alex Ferguson alipostaafu, kiwango cha Manchester United kilishuka na hakijapanda tena. Wamekwama.
Ingawa Mourinho alianza kwa kujaribu kujenga hisia, alikuwa maarufu au mkubwa kuliko klabu, hakuweza kuiinua timu hiyo na kuirejesha pale ilipozoeleka ikiwa mikononi mwa Ferguson.
Hakufaulu kuiondoa katika mkosi ulioachwa na watangulizi wake wawili, David Moyes na Louis van Gaal.  Licha ya fedha nyingi alizopewa na wamiliki wa klabu kusajili wachezaji kwa gharama kubwa, hakufaulu kutimiza ndoto ya waliomkabidhi mikoba.
Sana sana, alibaki kulalamikia ukubwa wa kiwango kikubwa zaidi cha fedha zilizotumiwa na Manchester City katika usajili, ingawa ukweli mwingine usiofichika, Man City wamefanikiwa pia kwa sababu ya karama binafsi ya Kocha wao, Pep Guardiola na utajiri mkubwa wa wamiliki wa klabu hiyo.
Mourinho na Ed Woodward walikuwa na mzozo mkubwa katika msimu huu kwa sababu ya kiwango kikubwa cha fedha kilichotumika bila kuonyesha faida yake haya yaliyotokea hayakushangaza mtu anayefuatilia soka, hasa baada ya kuona wachezaji waliosajiliwa kwa pesa nyingi mno wakikalishwa kwenye benchi badala ya kupangwa kwenye kikosi cha kwanza.
Kwa mfano, walipomchukua Paul Pogba, kama nia yao ilikuwa kujulisha dunia sasa wana msuli wa kusajili mchezaji wa kiwango chochote kutoka popote, ujumbe uliofika kwa walengwa haukuwa mzuri.
Mwezi uliopita, Mourinho alikiri Man United inakabiliwa na changamoto kubwa na wakati mgumu katika kuvutia na kuhudumia wachezaji muhimu inaowahitaji.
Zipo klabu ambazo tayari zimejipanga kupambana bila fedha nyingi kujihakikishia nafasi ya kucheza soka la Ligi ya Mabingwa, klabu ambazo zina viwanja vizuri, visivyojaza mashabiki wanaoishia kulilia mafanikio ya miaka iliyopita, zenye matumaini ya kushinda walau taji moja msimu huu.

Man United imebadilika kutoka klabu yenye kubeba makombe, ambayo kila mchezaji alikuwa anapania kujiunga nayo. Katika miaka mitano ya kuanguka kwa Manchester Unit, klabu nyingine zimeinuka na kuimarika.
Miaka kadhaa iliyopita, klabu kama Manchester United au Liverpool, ingetumia fursa ya ubabe wake kutesa timu nyingine kwa kuzinyang’anya wachezaji muhimu, kuua matumaini ya timu ndogo hizo na kukuza matumaini yake binafsi.
Bahati mbaya, enzi za ubabe wa klabu moja zimepita. Hata Man City, licha ya utajiri mkuwa ilionao sasa, haijafikia umaarufu na makali ya Liverpool ya miaka ya 80 au Man United ya miongo michache iliyopita.
Tayari Man City, ambayo imekuwa inajiwekea mazingira ya kuwa mbabe asiyeshindika, ilipigwa na Liverpool na Wigan msimu uliopita. Tayari Chelesea imeshaiondoa kwenye usukani wa ligi.
Ni wazi kuwa Mourinho asingeweza kuirejesha Manchester United katika enzi yake iliyopita. Naye alikiri suala hili hata kabla hajaondolewa.
Alisema haikuwa haki kulinganisha enzi zake hizi na enzi zilizopita kwa sababu mazingira hayafanani. Huko nyuma, Man United ilikuwa imefikia kiwango cha kutoshindika, kiasi kwamba karibu kila ilichotaka ilikipata.
Jukumu la kocha mpya ajaye ni kuirejesha Man United katika enzi zake zilizoachwa na Ferguson. Hata hivyo, haijulikana itafikia katika kiwango kile baada ya makocha wangapi kupita.
Si habari nzuri kwa mashabiki au wapenzi wa soka kwamba timu iliyowahi kuwa mbabe kiasi kile imebaki kukimbizana na timu nyingine ndogondogo mbali kabisa na uongozi wa ligi.
Haitarajiwi Man United itatumia miaka 28 kurejesha enzi zake kama ilivyotkea kwa Liverpool. Vile vile, haitarajiwi timu chache zilizo imara katika ligi zitaruhusu timu moja itawale tena ligi yao kwa miaka 10 au 15 mfululizo.
Enzi hizo zimepita, kama alivyosema Mourinho mwenyewe. Jambo kubwa wanalohitaji Man United sasa ni kocha ambaye ataleta mawazo mapya na mwamko mpya wa soka kwa staili mpya.