Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dodoma kuwa kitovu cha mashindano ya kuogelea jumuishi

KUOGELEA Pict

Muktasari:

  • Programu hiyo inayojulikana kama Inclusive Swimming Challenge, inayoandaliwa na Swahili Talent Sports Promotion kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, itaanza kwa semina na mafunzo kwa wataalamu kabla ya kuhitimishwa na mashindano ya kuogelea kwa watu wenye mahitaji maalumu Novemba 21.

DODOMA inatarajiwa kuwa kitovu cha shughuli za kuogelea jumuishi kuanzia Novemba 13 hadi 21 mwaka huu, kupitia programu maalumu inayolenga kuongeza fursa za michezo kwa watoto na vijana wenye mahitaji maalumu, sambamba na kutoa elimu ya usalama majini.

Programu hiyo inayojulikana kama Inclusive Swimming Challenge, inayoandaliwa na Swahili Talent Sports Promotion kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, itaanza kwa semina na mafunzo kwa wataalamu kabla ya kuhitimishwa na mashindano ya kuogelea kwa watu wenye mahitaji maalumu Novemba 21.

Mbali na mashindano, programu hiyo inalenga kutumia mchezo wa kuogelea kuwajengea uwezo watoto wenye changamoto za ukuaji na mfumo wa fahamu, huku ikipanua uelewa wa jamii kuhusu usalama katika maeneo yenye maji.

KUOG 01

Akizungumza kuhusu ushiriki wao, mwakilishi wa Kitengo cha Uhusiano na Masoko cha CF Hospital, Cheusi, amesema hospitali hiyo itatoa elimu ya afya bila malipo Novemba 13 na 14, ikiwalenga walimu wa kuogelea na wahudumu wa mabwawa.

Amesema wahudumu hao wana nafasi muhimu katika kuhakikisha usalama wa washiriki, hivyo wanahitaji kuwa na uelewa wa namna ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa mazoezi au shughuli za kuogelea.

“Tumejikita katika kutoa mchango wetu kwa asilimia 100 kuanzia tarehe 13 mpaka tarehe 14 na tutakuwepo Dodoma kutoa mafunzo. Tunawaalika pool attendants na walimu wanaotoa mafunzo ya swimming waje wapate elimu itakayowasaidia watoto na watu wazima wanaoshiriki zoezi hili,” amesema Cheusi.

Ameongeza kuwa wakazi wa Dodoma wanakaribishwa kujitokeza Novemba 21 kushuhudia mashindano hayo na kuwapa moyo watoto watakaoshiriki, akiamini kuwa ushirikiano wa jamii unaweza kuwasaidia washiriki hao kutimiza ndoto zao kupitia michezo.

KUOG 02

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mishipa ya Fahamu na Ubongo wa CF Hospital, Dk. Yusuf Jam Nagarwala, amesema kuogelea kunaweza kutumika kama sehemu ya tiba kwa watoto wenye mahitaji maalumu, kupitia huduma inayojulikana kama aquatherapy.

Alifafanua kuwa tiba hiyo inayotumia maji na mazoezi inaweza kusaidia watoto kutulia, kuboresha mawasiliano na kuongeza ushirikiano kati yao, wazazi na wahudumu wanaowazunguka.

“Moja ya huduma tunazoweza kuwasaidia watoto hawa ni aquatherapy, ambayo hapa tunaongelea kuhusu swimming. Kwa tiba hii, pamoja na mazoezi, inasaidia kuwatuliza watoto, kuboresha mawasiliano na kuongeza ushirikiano kati ya wazazi, wahudumu na watoto wenyewe,” amesema.

Dk. Nagarwala amesema watoto wenye changamoto za mfumo wa fahamu na ukuaji wanahitaji kutambuliwa mapema ili kubaini aina ya huduma wanazohitaji na namna bora ya kuwasaidia.

Ameongeza kuwa elimu jumuishi ni muhimu katika kuhakikisha watoto hao wanapata fursa ya kuendelea na masomo na kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii licha ya changamoto zinazowakabili.

Katika eneo la usalama majini, mkufunzi wa Tanzania Life Saving Society, Alexander Harrison Mwipasi, amesema chama hicho kitakuwepo Dodoma Novemba 13 kutoa mafunzo ya uokoaji na kujikinga na majanga yanayotokea kwenye maji.

KUOG 03

Amesema mafunzo hayo yatahusisha elimu ya kuzuia ajali kabla hazijatokea, mbinu za mtu kujiokoa anapojikuta kwenye hatari majini na namna ya kuwaokoa wengine.

Mwipasi amesema umuhimu wa mafunzo hayo unaongezeka kutokana na changamoto za hali ya hewa, ikiwemo athari zinazoweza kuambatana na mvua kubwa na mafuriko yanayohusishwa na El Niño.

“Jukumu letu kama Tanzania Life Saving Society ni kutoa elimu ya kuzuia kwanza. Ikishindikana na mtu akajikuta kwenye mafuriko, tunafundisha namna ya kujiokoa na pia kuwaokoa watu wengine,” amesema.

Amesisitiza kuwa elimu ya usalama majini haipaswi kuishia kwa washiriki wa mashindano au wanaofanya kazi kwenye mabwawa ya kuogelea, bali inapaswa kuwa sehemu ya maarifa ya kila Mtanzania.

Kwa upande wa Tanzania Paraswimming Association, Mkurugenzi wa Ufundi, Julius Felix Maganga, amesema kuandaliwa kwa mashindano hayo ni hatua inayoongeza fursa kwa vijana wenye mahitaji maalumu kushiriki katika mchezo wa kuogelea.

Maganga amesema kwa muda mrefu chama hicho kimekuwa na mashindano machache, hivyo kuongezeka kwa majukwaa ya aina hiyo kutasaidia wanamichezo hao kupata nafasi zaidi za kuonyesha uwezo wao.

“Kwa hali ambayo tumekuwa nayo awali kama chama, tumekuwa na shindano moja tu kwa mwaka. Kwa hiyo kuja kwao maana yake wanatusaidia kuongeza fursa nyingi zaidi za vijana hawa kupata nafasi ya ushiriki wao kwenye mchezo wa kuogelea,” amesema.

Hata hivyo, amesema ni muhimu matukio yajayo yasijikite katika kundi moja pekee la watu wenye mahitaji maalumu, bali yajumuishe pia wanamichezo wenye ulemavu wa viungo na wa kuona.

Ameeleza kuwa katika mchezo wa kuogelea kuna makundi matatu muhimu ya uainishaji wa wanamichezo wenye ulemavu, ambayo ni wenye ulemavu wa viungo, ulemavu wa kuona na ulemavu wa akili.

Kwa mujibu wa Maganga, mashindano ya Novemba 21 yameelekezwa zaidi kwa watu wenye ulemavu wa akili (intellectual disabilities), lakini alitumaini kuwa hatua hiyo itakuwa mwanzo wa fursa nyingine zitakazofungua milango kwa makundi mengine.

Ameongeza kuwa maendeleo ya michezo kwa watu wenye mahitaji maalumu yanahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali, akiwataja wazazi, walimu na wataalamu wa afya kuwa sehemu muhimu ya mfumo huo.