Dodoma Jiji yajipanga upya kwa Josiah
Muktasari:
- Josiah aliyewahi kufundisha pia timu mbalimbali zikiwemo Tunduru Korosho, Biashara United, Geita Gold na Tanzania Prisons, amekuwa miongoni mwa makocha bora wazawa nchini na sasa Dodoma Jiji inataka kumuongezea mkataba.
UONGOZI wa Dodoma Jiji unatarajia kuanza mazungumzo mapya hivi karibuni na kocha mkuu wa kikosi hicho, Amani Josiah kwa ajili ya kuongeza mkataba, baada ya ule wa awali kukaribia kufikia ukomo wake ambapo ni mwishoni mwa Oktoba 2026.
Josiah aliyewahi kufundisha pia timu mbalimbali zikiwemo Tunduru Korosho, Biashara United, Geita Gold na Tanzania Prisons, amekuwa miongoni mwa makocha bora wazawa nchini na sasa Dodoma Jiji inataka kumuongezea mkataba.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson alisema baada ya msimu wa 2025-2026 kumalizika, wataanza kukaa vikao kwa ajili ya kujadiliana juu ya mustakabali wa kocha huyo, ingawa bado ana mkataba na kikosi hicho.
"Mkataba wa Josiah na Dodoma Jiji unaisha mwishoni mwa Oktoba 2026, baada ya viongozi kukaa chini ndipo tutakapotoka na majibu ya moja kwa moja kuhusiana na suala lake, ila kwa sasa niseme wazi ni kocha tunayejivunia," alisema Fortunatus.
Josiah alijiunga na Dodoma Jiji Oktoba 16, 2025, akimrithi Mrwanda Vincent Mashami ambapo kwa msimu wa 2025-2026, katika Ligi Kuu ya NBC aliiongoza timu hiyo kumaliza nafasi ya tisa na pointi 35, ikishinda mechi nane, sare 11 na kupoteza 11.
Moja ya historia kubwa kwa Josiah aliyoiandika akiwa na Dodoma Jiji msimu wa 2025-2026, ni ya kuvunja rekodi ya Yanga ya kucheza jumla ya mechi 42 za Ligi Kuu bila ya kupoteza, wakati kikosi hicho cha 'Walima Zabibu' kiliposhinda mabao 3-2.
Ushindi wa mabao 3-2 ilioupata Dodoma Jiji katika mechi ya Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Yanga, Mei 13, 2026, ilimfanya Josiah kuivunja rasmi rekodi ya mabingwa hao ya kucheza muda mrefu bila ya kupoteza, tangu mara ya mwisho, Novemba 7, 2024.
Kabla ya kichapo hicho, Yanga ilicheza mechi 42 za Ligi Kuu bila ya kupoteza kwa siku 552, ambazo ni sawa na mwaka mmoja, miezi sita na siku sita.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Airtel mkoani Singida, mabao ya Dodoma yalifungwa na Bakari Mwamnyeto aliyejifunga, Mwana Kibuta na Waziri Junior huku ya Yanga yakifungwa yote na Allan Okello.