Del Piero atua Bigman FC
Muktasari:
- Del Piero amesema amefikia makubaliano ya kukifundisha kikosi hicho hadi mwishoni mwa msimu huu wa 2026-2027, huku lengo kubwa ni kufanya vizuri kwa sasa, licha ya timu hiyo kuanza vibaya kwa mechi ilizozicheza.
UONGOZI wa Bigman FC umefikia makubaliano ya kumwajiri Kocha Mkuu, John William Zongwe ‘Del Piero’ kuifundisha timu hiyo zamani Mwadui FC, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na mtangulizi wake, Omary Kapilima aliyeamua kuachia mwenyewe ngazi.
Del Piero amesema amefikia makubaliano ya kukifundisha kikosi hicho hadi mwishoni mwa msimu huu wa 2026-2027, huku lengo kubwa ni kufanya vizuri kwa sasa, licha ya timu hiyo kuanza vibaya kwa mechi ilizozicheza.
“Sio kazi nyepesi kwa sababu tayari makocha wawili wamepita kabla yangu, kocha mzuri ni yule anayezikubali changamoto na kuzigeuza fursa ya kufanya kitu bora zaidi, naamini tuna uwezo wa kutengeneza kikosi cha ushindani,” amesema Del Piero.
Kocha huyo aliyewahi kuzifundisha timu za Namungo FC, Pan African FC, TMA FC, Mafunzo SC ya visiwani Zanzibar, amejiunga na Bigman FC huku mara ya mwisho aliifundisha IAA SC ikiwa Ligi Daraja la Pili, ingawa kwa sasa inashiriki Championship.
Del Piero ni kocha wa tatu kuifundisha Bigman FC msimu huu, baada ya Amanzi Nurdin na Omary Kapilima na kabla ya mechi ya jana Jumapili dhidi ya Stand United, imetoa sare moja na kuchapwa tano, ikiwa mkiani mwa nafasi ya 16 na pointi moja.