Datius afunguka rafu ya Aziz KI
Muktasari:
- Katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Septemba 15, 2026, Yanga ikiwa pungufu ilishinda bao 1-0, huku Stephane Aziz KI akionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 18 kwa kumkanyaga beki huyo ambaye alishindwa kumaliza dakika 90 kutokana na maumivu.
BAADA ya kushindwa kumaliza mchezo uliopita dhidi ya Yanga, beki wa Geita Gold, Datius Peter amesema kwa sasa afya yake imeimarika na anasubiri ripoti ya daktari na uamuzi wa Kocha Mkuu, Zuberi Katwila kumjumuisha kikosini mechi ijayo.
Katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Septemba 15, 2026, Yanga ikiwa pungufu ilishinda bao 1-0, huku Stephane Aziz KI akionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 18 kwa kumkanyaga beki huyo ambaye alishindwa kumaliza dakika 90 kutokana na maumivu.
Datius amesema kwa sasa afya yake inaimairika na ameanza mazoezi akieleza kuwa matarajio yake mchezo ujao dhidi ya Pamba Jiji, anasubiri uamuzi wa kocha iwapo atampanga kuanza.
Amesema katika historia ni ajali ya kwanza kwake uwanjani, akieleza kuwa rafu hiyo ilitokea bahati mbaya kwakuwa Aziz KI hajawahi kuwa na rekodi ya kucheza madhambi.
“Binafsi nashukuru naendelea vizuri japo haikuwa kazi nyepesi, kwa sasa naendelea vizuri na ninaanza mazoezi, ripoti ya daktari ndio itaeleza zaidi na kocha kuamua, ila niko tayari hata mechi ijayo.
“Aziz KI hajawahi kucheza rafu kama hizo, nafikiri ilikuwa bahati mbaya kwakuwa mguu wake ulitaka kukinga mpira sasa uwepesi wangu uwanjani ndio ikatokea hivyo, ila natembea vizuri kwa sasa”.
Amefafanua kuwa baada ya rafu hiyo, ilibainika uvimbe kwenye enka na ugoko eneo la juu, lakini kwa matibabu yaliyofanyika ameweza kurejea vyema akiwatoa hofu wadau na mashabiki wake wa soka kuwa atarudi tena uwanjani.