Mzize ndani, kocha akimtaka Job
Muktasari:
- Mzize aliyeingia uwanjani juzi Jumanne katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa KMC Complex, Dar es Salaam ambayo Yanga iliichapa Geita Gold bao 1-0, alikuwa nje kwa muda mrefu akiuguza majeraha ya goti.
BAADA ya siku 447 ambazo ni sawa na mwaka mmoja, miezi miwili na siku 21, hatimaye mshambuliaji wa Yanga SC, Clement Mzize amecheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho.
Mzize aliyeingia uwanjani juzi Jumanne katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa KMC Complex, Dar es Salaam ambayo Yanga iliichapa Geita Gold bao 1-0, alikuwa nje kwa muda mrefu akiuguza majeraha ya goti.
Mzize alipata majeraha makubwa ya goti katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete Benguela ya Angola yaliyomlazimu kufanyiwa upasuaji. Mchezo huo wa hatua ya awali uliopigwa Septemba 27, 2025 nchini Angola, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Jeraha hilo lilimweka Mzize nje ya uwanja kwa muda huo akipitia mchakato mrefu wa matibabu na upasuaji kabla ya kurejea rasmi uwanjani Septemba 15, 2026 kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Geita Gold ambayo Yanga ilishinda 1-0.
Kabla ya kupata majeraha hayo, Mzize alicheza mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara Juni 25, 2025, siku ambayo Yanga iliifunga Simba mabao 2-0, huku mshambuliaji huyo akifunga la pili dakika ya 88 baada ya Pacome Zouzoua kutangulia dakika ya 67. Akamaliza msimu wa 2024-2025 akiwa kinara wa mabao ya Ligi Kuu Bara ndani ya Yanga alipofunga 14, mawili nyuma ya kinara wa jumla, Jean Charles Ahoua aliyekuwa Simba akitupia 16.
Tangu hapo, Mzize hakucheza mechi yoyote ya Ligi Kuu Bara akiukosa msimu mzima wa 2025-2026 kutokana na majeraha hayo aliyoyapata mwanzoni mwa msimu huo.
Juzi alipoingia dakika ya 65 kuchukua nafasi ya Seleman Mwalimu, Mzize alionekana kuwa na hamu kubwa ya kuiwakilisha Yanga kama hapo awali kwani mapema tu alifanya shambulizi la kwanza ambalo halikulenga lango.
Hata hivyo, kutokana na Yanga kuwa pungufu muda mwingi tangu dakika ya 18 alipotolewa kiungo wa kikosi hicho, Stephane Aziz KI kwa kuonyeshwa kadi nyekundu, Geita Gold kwa kiasi kikubwa ilionekana kutawala mchezo. Mzize aliyetumika kwa dakika 25, alimaliza na mashuti mawili ambayo yote hayakulenga lango.
Akizungumzia kurejea kwake, Kocha Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi alisema: “Nimefurahi sana kwa sababu naamini ni mmoja wa wachezaji wangu bora kwa sasa. Amecheza vizuri sana kwa mtu aliyekuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu. Nilifurahi sana na nilitamani angehitimisha kiwango hicho kwa bao zuri.”
Wakati Mzize akirejea, bado beki na nahodha msaidizi wa kikosi hicho, Dickson Job aliyeumia Machi 1, 2026 ambaye inaelezwa naye huenda akaonekana mechi ijayo kufuatia kupona majeraha ya goti.
Kuhusu kurejea kwa Job, Manqoba alisema: “Sasa namsubiri Job naye aingie pia, kwa sababu nahitaji wachezaji hawa wote wawe tayari na fiti kwa ajili ya msimu ujao.”
Mzize ambaye Juni 25, 2025 katika mechi ya kuhitimisha Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025 alifunga bao dhidi ya Simba, baada ya hapo alicheza mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Singida Black Stars ambayo Yanga ilishinda 2-0, kisha Ngao ya Jamii dhidi ya Simba (Septemba 16, 2025) Yanga ikishinda tena 1-0 kwa bao la Pacome.
Mshambuliaji huyo ambaye baada ya msimu wa 2024-2025 ilielezwa kulikuwa na dili kadhaa za timu zilizohitaji huduma yake kabla ya kubaki Yanga, ndipo Septemba 19, 2025 katika safari mpya ya Ligi ya Mabingwa Afrika akaumia.
Kuumia kwake kukawa pigo kwa Yanga, akakaa nje kwa takribani miezi mitano, Februari 7, 2026 akacheza dakika tisa za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS FAR Rabat ugenini. Tangu hapo, hakucheza tena ikielezwa alijitonesha, ndipo akahitajika kukaa nje kupona kabisa.
Majeraha hayo ya Mzize yalimfanya kukosa jumla ya mechi 58 za mashindano yote ambayo Yanga ilishiriki kuanzia 2025-2026 hadi sasa 2026-2027. Katika mechi hizo, za Ligi Kuu Bara ni 35 zikiwemo 30 za msimu mzima wa 2025-2026 na tano msimu huu. Ligi ya Mabingwa Afrika (10), Kombe la Shirikisho la CRDB (5), Kombe la Mapinduzi (4), Kombe la Muungano (3) na Ngao ya Jamii (1).