Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Darasa: TP Mazembe inatoa mafunzo haya kwa Simba, Yanga

Mshambuliaji wa TP Mazembe na Taifa Stars, Mbwana Samatta

Muktasari:

Azam ambayo ndiyo timu inayoonekana kujiweza zaidi Tanzania, haifiki hata nusu ya Mazembe. Timu hiyo imejitanua kiasi kwamba unaweza kuifananisha na timu kubwa za Ulaya kama Arsenal, Liverpool na Manchester United.

TP Mazembe inajiweza. Ni timu ya sayari nyingine ukifananisha na timu za Simba na Yanga ambazo ndizo kubwa zaidi kwa Tanzania. Ni kama kufananisha mdoli na binadamu.

Azam ambayo ndiyo timu inayoonekana kujiweza zaidi Tanzania, haifiki hata nusu ya Mazembe. Timu hiyo imejitanua kiasi kwamba unaweza kuifananisha na timu kubwa za Ulaya kama Arsenal, Liverpool na Manchester United.

Makala haya yanakuletea orodha ya mambo ambayo timu za Tanzania hususan Simba na Yanga zinaweza kujifunza kutoka kwa TP Mazembe.

Uwekezaji wa maana

Unapoamua kufanya kitu usifanye nusu nusu, fanya kitu kizima. Hivyo ndivyo alivyofanya mmiliki wa TP Mazembe, Moise Katumbi kwa kufanya uwekezaji wa maana katika klabu hiyo.

Tajiri huyo amejenga uwanja wa maana wenye uwezo wa kubeba mashabiki 30,000, ni uwekezaji mkubwa. Mbali na hilo, timu hiyo ina kliniki ya kisasa kabisa, hospitali ya timu pamoja na ‘gym’ ya kisasa.

Hii ni aina ya uwekezaji wa kipekee ambao unapaswa kuigwa na timu za Tanzania.

Bidhaa za klabu

Pembezoni mwa Uwanja wa Mazembe kuna duka kubwa la bidhaa za timu hiyo kama jezi, madaftari, kalamu, vikombe, kofia na nyingine nyingi ambazo hutengenezwa na kuuzwa na klabu hiyo.

Bidhaa hizo zimepata soko kubwa kwa mashabiki wa Mazembe pamoja na wa timu nyingine, hivyo kuwa moja ya vyanzo muhimu vya mapato klabuni hapo.

Simba na Yanga zinabidi kuiga mfano huo kwani licha ya Mazembe kuwa klabu tajiri, imejitahidi kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato ili iweze kujiendesha.

Timu za vijana

Mazembe ina timu ya vijana inayoonekana kuwa imara na kupata matunzo ya maana pengine kuliko baadhi ya timu kubwa za Tanzania. Katika kuonyesha umuhimu wa soka la vijana, Mazembe imewapa kazi Wazungu watatu kufundisha kikosi hicho ili kiweze kuzalisha mastaa wa maana.

Mbali na hilo, vijana hao wamekuwa wakisomeshwa na Mazembe pamoja na kupewa Dola 500 (900,000) kama posho ya kujikimu kila mwezi.

Timu za vijana za Tanzania ni kama zimetelekezwa kwani wachezaji wake hawana viwanja vya maana vya kufanyia mazoezi, pia makocha wake wamekuwa wa kuungaunga.

Afya za

wachezaji

Mchezaji yeyote anayeumia katika majukumu ya klabu huudumiwa na Mazembe. Wachezaji wakiwa na majeraha makubwa hupelekwa katika hospitali ya klabu wakati wale wenye majeraha madogo huudumiwa katika kliniki yao.

Hili ni jambo la kujifunza kwa timu za Tanzania ambazo zimeacha mzigo mkubwa wa matibabu kwa wachezaji wenyewe licha ya kwamba wamekuwa wakiumia katika majukumu ya klabu.

Timu inahitaji vikosi viwili imara

TP Mazembe imecheza mechi tatu za kimataifa za kirafiki na kushinda zote licha ya kuwakosa nyota wake tisa wa kikosi cha kwanza waliokwenda kwenye majukumu ya timu za taifa.

Hii inaonyesha kuwa, timu hiyo ina vikosi viwili vyenye uwezo unaokaribiana, hivyo pale inapokuwa na mechi za ligi na Klabu Bingwa Afrika huweza kuchezesha vikosi viwili tofauti katika mechi hizo ili kujihakikishia ushindi.

Wachezaji watano wa

kigeni hawatoshi

Tuachane na siasa za kujenga timu ya taifa, ukweli ni kwamba idadi ya wachezaji watano wa kigeni katika klabu moja haiwezi kuisaidia timu kufika mbali katika michuano ya kimataifa.

Ukiwatazama wachezaji wazawa walivyokuwa wakicheza mechi za kimataifa za kirafiki hapa Lubumbashi unaona kabisa kwamba hawajapevuka vilivyo kuweza kuisaidia timu kufika mbali.

TP Mazembe ambayo inafanya vizuri katika michuano ya Afrika, ina wachezaji 11 kutoka nje ya Congo.

Hili limewasaidia katika kujenga timu inayoweza kushindana na timu kubwa.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liache siasa na kuukubali ukweli kwamba, kama klabu zetu zinataka kufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika, ziongezewe idadi ya wachezaji wa kigeni ili kuwa na timu imara.

Mashabiki wa timu

Achana na Simba Ukawa wanaosifika kwa kushangilia hapa Tanzania, TP Mazembe ina kikundi chao cha ushangiliaji ambacho kinafanya mazoezi kila siku na kina uwezo wa kushangilia bila kuchoka kwa dakika zote za mchezo.

Kikundi hicho kina vifaa vya maana kama matarumbeta na ngoma ambazo zikilia uwanja wote unazizima.

Ukipoteza mechi utatakiwa kujiuliza

Timu za Tanzania zimekuwa hazina tabia ya kujiuliza punde zinapofungwa hasa katika michuano ya kimataifa lakini Mazembe imekuwa ikifanya hivyo mara kwa mara.

Mmiliki wa Mazembe, Moise Katumbi aliamua kujenga kliniki ya klabu hiyo baada ya kufungwa na Inter Milan katika fainali ya Klabu Bingwa ya Dunia mwaka 2010.

Katumbi aliuliza sababu ya Milan kucheza bila kuchoka licha ya kuwa na mechi nyingi mfululizo na kuambiwa kuwa timu hiyo ina kliniki ambayo huwasaidia wachezaji kupunguza uchovu na ndipo alipokuja kujenga ya kwake.

KLINIKI YA MAZEMBE

NI AIBU TUPU

UKIIONA kwa haraka unaweza kusema ni eneo la kufanyia mazoezi ‘gym’ lakini siyo. Ni kliniki ya Klabu ya TP Mazembe ambayo ni mahususi kwa kuwatibu wachezaji wake waliokumbwa na majeraha mbalimbali na kuwarejesha uwanjani kwa wakati.

Mbali na matibabu, kliniki hiyo inatumika kama sehemu ya kuwapunguzia wachezaji uchovu wa mechi (rehabilitation) ili kuwaweka fiti kwa mapambano zaidi hasa pale wanapokuwa na ratiba ngumu.

Mwanaspoti imefanya ziara katika kliniki hiyo na kuzungumza na daktari msimamizi wa kliniki hiyo, Lutula Vincent.

Daktari huyo alimtembeza mwandishi wa gazeti hili katika maeneo mbalimbali ya kliniki hiyo na kumwelezea matumizi ya vifaa vilivyopo. Fahamu jinsi ilivyo.

Sehemu ya tiba

Sehemu ya kwanza ya kliniki hiyo ni ya tiba ambapo Dokta Vincent anasema mchezaji mwenye majeraha ya goti, nyama za paja na mengine ambayo hayahusiki na kuvunjika mfupa hupatiwa tiba hapo.

“Hapa (anaonyesha kitanda kidogo kilichopakana na mashine) ndipo wachezaji wanapotibiwa, hiyo mashine unayoiona ni ya kuongeza kasi ya uponyaji hasa kwa wale walioumia goti na enka,” anasema.

Mashine za mazoezi

Sehemu ya pili katika chumba cha kwanza cha kliniki hiyo imewekwa vifaa mbalimbali vya mazoezi kulingana na tatizo la mchezaji husika. Kuna vifaa vya mazoezi ya kukimbia ambavyo hutumika kupasha mwili joto kabla ya mchezaji kuanza mazoezi ya sehemu ya jeraha.

“Mchezaji akishapona majeraha anaanza mazoezi mepesi hapahapa, hiyo mashine ya kwanza ni ya kipa kama ameumia, zile kule chini ni za kupashia mwili moto na hizi nyingine ni za mazoezi ya jeraha husika,” anasema.

Bwawa la kuogelea, majakuzi

Sehemu ya tatu ya kliniki hiyo ina bwawa la kuogelea pamoja na majakuzi matatu makubwa ambayo hutumiwa na wachezaji siku ya pili baada ya kucheza mechi.

Chumba cha pembeni ya majakuzi na bwawa hilo kuna vyumba vya kubadilishia nguo ambapo makabati yake yameandikwa majina ya wachezaji wa timu hiyo wakiwemo Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu raia wa Tanzania.

“Jakuzi moja ni la maji ya moto na hicho chumba kingine hapa ni cha joto (sauna), wachezaji wakitoka kwenye mechi leo, kesho asubuhi huja hapa kupata hiyo programu ambayo inapunguza uchovu,” anaeleza Vincent.

“Wakitoka kwenye joto wanakwenda kwenye majakuzi yenye barafu ama kwenye bwawa la kuogelea kule.”

Mashine ya kuondoa vumbi

Mambo ya Mazembe ni kama Ulaya kwani wachezaji wao wakienda kucheza na timu pinzani kwenye viwanja vibovu na vyenye vumbi siku inayofuata huingizwa katika mashine maalumu ili kuondoa vumbi mwilini.

“Hii ni mashine ya kuondoa vumbi, hawa wachezaji wanaingia tunafunga milango na kisha tunaiwasha, inatoa mvuke ambao husaidia kusafisha koo na kuondoa vumbi ndani ya mwili,” anaeleza.

Sehemu ya masaji

TP Mazembe ina wafanyakazi zaidi ya 100 ambao hufanya kazi mbalimbali ikiwemo kuwafanyia masaji wachezaji wa timu hiyo. Wachezaji baada ya kupitia programu zote za kuondoa uchovu huenda kuoga na kisha kurejea kwa ajili ya kufanyiwa masaji katika vitanda vidogo.

“Wachezaji wakitoka katika majakuzi ya moto huingia kwenye maji ya baridi ambayo ni kwenye hilo jakuzi moja na kule kwenye bwawa la kuogelea ambako maji yake ni ya baridi kama barafu.

“Wakitoka huko huenda katika mabafu ya kawaida kuoga na kisha kuja hapa kufanyiwa masaji, tuna watu maalumu hapa kwa ajili ya kazi hiyo,” anafafanua.