Dalali hajakanyaga Msimbazi miaka mitatu
HASSAN Dalali
MWANDISHI WETU HASSAN Dalali, Mwenyekiti wa zamani wa Simba ametoa mpya baada ya kusema hajakanyaga makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam kwa miaka mitatu. Licha ya hilo, Dalali maarufu kama Field Marshal alisema hajawahi kwenda kuona mechi yoyote inayoihusu Simba au timu nyingine yoyote kwenye Uwanja wa Taifa au uwanja mwingine wowote kwa miaka hiyo mitatu. Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam jana Ijumaa, Dalali alisema amempumzika kwa muda kujihusisha na soka na sasa anafanya biashara zake binafsi pamoja na siasa. "Mambo ya mpira nimepumzika bwana. Hivi unajua sijaenda makao makuu ya Simba wala Uwanja wa Taifa kwa miaka mitatu," alisema Dalali, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Simba kabla ya uongozi wa sasa. Dalali, ambaye hakuwa tayari kuzungumzia maoni yake kuhusu mgogoro unaoendelea Simba alisema licha ya biashara zake za kawaida yeye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Mzimuni, Wilaya ya Kinondoni. Alipoulizwa kama yupo tayari kurejea kuokoa jahazi Msimbazi alisema: "Nimekwambia kwa sasa nimepumzika soka, nafanya biashara zangu na pia mimi ni Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mzimuni." Wakati wa utawala wa Dalali, licha ya kuwa na changamoto kadhaa, lakini utawala wake ulileta umoja miongoni mwa wanachama, mashabiki na viongozi kwa ujumla.