Clara mdogo mdogo Marekani
Muktasari:
- Clara, ambaye ni mchezaji pekee kutoka Tanzania anayekipiga kwenye ligi hiyo, alipewa nafasi ya kuanza kwenye mchezo huo na kocha, ikiwa ni mwendelezo wa kuongezeka kwa nafasi yake katika kikosi hicho kinachoshiriki Ligi ya Soka ya Wanawake Marekani (NWSL).
MSHAMBULIAJI wa Tanzania, Clara Luvanga anaendelea kuonyesha dalili za kuimarika katika kikosi cha Washington Spirit ya Marekani, baada ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza kilichoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Gotham FC, Oktoba 17.
Clara, ambaye ni mchezaji pekee kutoka Tanzania anayekipiga kwenye ligi hiyo, alipewa nafasi ya kuanza kwenye mchezo huo na kocha, ikiwa ni mwendelezo wa kuongezeka kwa nafasi yake katika kikosi hicho kinachoshiriki Ligi ya Soka ya Wanawake Marekani (NWSL).
Katika mchezo huo, mshambuliaji huyo alicheza dakika 79 kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na Hatch A, huku Washington Spirit ikilinda ushindi wake wa bao moja na kuondoka na pointi tatu muhimu dhidi ya Gotham.
Kupata nafasi ya kuanza katika mchezo huo kunakuja baada ya Clara kuonyesha uwezo wake katika mechi mbili zilizopita na alianza safari yake kwa kucheza mechi yake ya kwanza, akafuata kwa kufunga bao katika mchezo wa pili, na sasa ameanza tena katika mechi yake ya tatu.
Katika mchezo wake wa kwanza wa alicheza dhidi ya Angel City FC Septemba 26, mwaka huu. Clara alitokea benchi na kucheza dakika 24, timu hiyo ikipoteza kwa bao 1-0.
Kisha akapata nafasi ya kucheza tena mchezo wake wa pili dhidi ya Houston Dash, Oktoba 4 na aliingia kipindi cha pili dakika ya 66 na kucheza dakika 25 kabla ya kufunga bao la ushindi dakika ya 84.
Bao hilo liliipa Washington Spirit ushindi wa mabao 3-2 katika mchezo huo wa ugenini, huku Clara akiweka historia nyingine ya kuwa Mtanzania wa kwanza kufunga bao katika Ligi Kuu ya Wanawake Marekani.
Ishara hiyo inaonyesha namna nyota huyo Mtanzania anavyoendelea kupata nafasi ya kuonyesha uwezo wake katika kikosi hicho, hasa baada ya kuonyesha uwezo wa kufunga katika mchezo uliomtangulia. Hata hivyo, ushindani wa nafasi ndani ya timu hiyo bado unahitaji aendelee kutumia vizuri kila nafasi anayopewa.