Clara Luvanga atimkia Marekani
Muktasari:
- Nyota huyo ambaye alikuwa mfungaji bora wa ligi ya Saudi Arabia msimu uliopita akifunga mabao 24 anaandika historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza ligi ya Marekani ambayo imejaa mastaa kutoka maeneo mbalimbali duniani.
MSHAMBULIAJI wa Tanzania, Clara Luvanga amejiunga na klabu ya Washington Spirit inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake nchini Marekani akitokea Al Nassr ya Saudia.
Nyota huyo ambaye alikuwa mfungaji bora wa ligi ya Saudi Arabia msimu uliopita akifunga mabao 24 anaandika historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza ligi ya Marekani ambayo imejaa mastaa kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Clara, ambaye kwa miaka ya karibuni amekuwa miongoni mwa wachezaji wanaoiwakilisha Tanzania kwa kiwango kikubwa, amejiunga na Washington Spirit kwa mkataba wa miaka minne utakaomuweka hadi mwaka 2029, ukiwa ni uhamisho unaompeleka katika moja ya ligi zinazotazamwa zaidi kwenye soka la wanawake duniani.
Hatua hiyo si ya kawaida kwa Clara, bali ni kilele cha safari iliyopitia changamoto na vituo kadhaa kabla ya kufika Marekani.
Akizungumza baada ya kujiunga na chama hilo alisema, “nina furaha sana kujiunga na Washington Spirit na kukabiliana na changamoto hii mpya katika NWSL. Najua nimewasili wakati msimu ukiendelea, lakini nina hamu kubwa kucheza katika ligi na nchi mpya.
“Pamoja na timu kuwa katika nafasi nzuri, nataka kusaidia kwa kila namna ninayoweza kuanzia sasa hadi hatua ya mtoano.”
Ndani ya misimu mitatu aliyoitumikia Al Nassr alikuwa mmoja wa wachezaji wa kigeni wenye mchango mkubwa kwenye kikosi akitwaa nacho ubingwa wa Ligi Kuu Saudi Arabia mara tatu.
Ikumbukwe Al Nassr kiujumla imetwaa taji la Ligi mara nne.
Msimu wake wa kwanza alifunga mabao 11 na asisti saba, msimu wa 2024/25 alifunga mabao 21 na asisti saba na msimu wa 2025/26 alifunga mabao 24.
YANGA HADI MAREKANI
Kipaji cha mshambuliaji huyo kilianza kuonekana akiwa na Yanga Princess msimu wa 2022/23 akiwa kwenye kikosi hicho chini ya kocha Edna Lema alikuwa mchezaji muhimu akifunga mabao 13.
Wakati huo alikuwa mchezaji mwenye kiwango kikubwa hadi kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Wanawake chini ya miaka 17 (Serengeti Girls) akifanikiwa kufunga mabao 10 katika michezo sita aliyocheza.
Mchango wake unakumbukwa zaidi kwa kuiwezesha Tanzania kufuzu fainali za Kombe la Dunia kwa Wanawake wenye umri chini ya miaka 17 zilizofanyika nchini India mwaka 2022.
Msimu wa 2023/24 akajiunga na Dux Lugrono ya Hispania ambako alicheza kwa miezi mitatu tu kisha akatimkia Saudia ambako anatajwa kuwa mmoja wa wachezaji waliopiga pesa nyingi kwenye dili hiulo.
Clara alisema uhamisho wake kutoka Hispania uligharimu kiasi cha Sh51 milioni za pesa ya usajili, lakini mshahara wake ndani ya miaka mitatu, mwaka wa kwanza alikunja milioni 19, mwaka jana alilipwa Sh23 milioni na mwaka huu analipwa kwa mwezi Sh27 milioni ambao ndio msimu wake wa mwisho.