Choki, Tony vita ni leo
Muktasari:
- Haitakuwa vita ya makonde pekee, bali itakuwa mapambano ya mitindo miwili tofauti ya ndondi, akili dhidi ya nguvu, utulivu dhidi ya presha na mbinu dhidi ya mashambulizi ya kasi.
BAADA ya wiki kadhaa za kusubiri, siku ya hukumu imefika. Leo macho ya mashabiki wa ndondi yataelekezwa kwenye Ukumbi wa Ubungo East African Logistic Center jijini Dar es Salaam ambapo Juma Choki na Tony Rashid watashuka ulingoni kuamua nani ataondoka na heshima ya kuwa mfalme wa Dar Boxing Derby 2026.
Haitakuwa vita ya makonde pekee, bali itakuwa mapambano ya mitindo miwili tofauti ya ndondi, akili dhidi ya nguvu, utulivu dhidi ya presha na mbinu dhidi ya mashambulizi ya kasi.
Baada ya kukamilisha zoezi la kupima uzito jana kwenye uwanja wa Las Vegas Mabibo, mabondia hao sasa wapo tayari kwa dakika 12 za majaribu makubwa zitakazoamua nani atainua mkono juu na kuondoka na zawadi ya gari aina ya Toyota Crown New Model.
Lakini zaidi ya zawadi hiyo yenye thamani kubwa, kivutio kikubwa cha pambano hili ni namna litakavyowakutanisha mabondia wawili wenye falsafa tofauti kabisa ndani ya ulingo.
Kwa upande mmoja yupo Juma Choki, bondia anayejulikana kwa nidhamu, matumizi mazuri ya umbali na uwezo wa kusoma mchezo wa mpinzani kabla ya kuongeza mashambulizi.
Choki anaingia kwenye pambano hilo akiwa na rekodi iliyomjengea heshima ndani na nje ya Tanzania. Tangu aanze ngumi za kulipwa mwaka 2017, amekuwa akipanda hatua kwa hatua hadi kufikia kushiriki mashindano ya kimataifa ya WBC Grand Prix nchini Saudi Arabia, uzoefu uliompa nafasi ya kukutana na mazingira ya ushindani mkubwa.
Kwa mujibu wa takwimu za BoxRec, bondia huyo wa uzito wa Lightweight amecheza mapambano 13 ya kulipwa, akishinda 11, kupoteza moja na kutoka sare moja, huku ushindi wake manne ukiwa kwa njia ya KO.
Silaha kubwa ya Choki imekuwa mkono wake wa kushoto (southpaw), uwezo wa kutumia 'jab' kudhibiti umbali pamoja na uchezaji wake wa miguu unaomruhusu kubadilisha mwelekeo wa pambano wakati wowote.
Mara nyingi Choki huwalazimisha wapinzani wake kupigana kwa mfumo anaoutaka yeye, akitumia akili zaidi kabla ya kuachia mashambulizi makali.
"Ninaheshimu kila ninachokutana nacho kwenye ulingo. Sitakwenda kwenye pambano hili kwa sababu nimewahi kucheza Saudi Arabia, bali nitaingia kama mtu anayeanza safari yake. Tony namheshimu na nimejiandaa kwa vita kubwa," amesema Choki.
Upande wa pili wa ulingo kutakuwa na Tony Rashid, maarufu kama AK-47 Bad Belle, bondia mwenye sifa ya kuwa mmoja wa wapiganaji wanaopenda vita vya karibu na kubadilishana makonde.
Tony ni aina ya bondia ambaye akipata nafasi ya kumshambulia mpinzani wake, huongeza presha bila kumpa muda wa kupumua. Nguvu zake, kasi ya mikono na uwezo wa kutafuta KO vimekuwa sehemu ya utambulisho wake.
Hata hivyo, safari hii Tony ameonyesha kuwa hataki kutegemea nguvu pekee, bali amefanya maandalizi ya kiufundi kuhakikisha anaweza kubadilika kulingana na mchezo wa Choki.
Rekodi zinaonyesha Tony ana uzoefu mkubwa zaidi wa mapambano ya kulipwa. Amecheza mapambano 24, akishinda 17, kupoteza manne na kutoka sare matatu, huku ushindi 11 ukiwa kwa njia ya KO.
Pia amewahi kupambana kwenye viwango vya juu zaidi akishiriki mapambano ya mataji ya African Boxing Union (ABU), jambo lililomjengea uzoefu wa kucheza chini ya presha kubwa.
Kwa mtazamo wa kiufundi, changamoto kubwa ya Choki itakuwa namna ya kudhibiti presha ya Tony na kuhakikisha haruhusu pambano liingie kwenye vita ya kubadilishana makonde.
Kwa upande wa Tony, kazi yake kubwa itakuwa kuvunja mfumo wa Choki wa kutumia umbali na harakati za miguu, jambo litakalomlazimisha kutumia akili kabla ya kutumia nguvu.
Tony amesema yeye na timu yake wamefanya uchambuzi wa kina wa mchezo wa Choki na wamejiandaa kwa kila mazingira yatakayojitokeza ndani ya ulingo.
Kwa mujibu wa waandaaji, Toyota Crown New Model haitakuwa sababu pekee ya mabondia hao kupigana, kwani wote tayari wamelipwa kwa mujibu wa mikataba yao. Gari hilo limeongezwa kama motisha maalum ya kuongeza ushindani na kuonyesha uwezo wa ndondi kubadilisha maisha ya wanamichezo.
Zawadi hiyo imeandaliwa na wadhamini Smart Gin chini ya kampuni ya Euromax Limited, kwa kushirikiana na QFK Motor kupitia Pick Time Media na Pent Promotion.
Sasa jibu limesalia ndani ya kamba nne za ulingo. Je, akili na mbinu za Choki zitaweza kuzuia mashambulizi ya AK-47 Tony Rashid au nguvu ya Tony itazima mipango? Leo Dar es Salaam itapata jibu.