Cheka amkubali Mwakinyo

BONDIA bingwa wa zamani wa dunia wa WBF, Francis Cheka amemtaja Hassan Mwakinyo kuwa ni bondia wake bora kwenye kizazi cha ngumi cha sasa.
Bondia huyo amekwenda mbali zaidi na kueleza ushindani wa ndondi nchini bado sio wa kiwango cha kimataifa, huku akivikataa viwago vya mabondia kama Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’, Twaha Kassim ‘Kiduku’ na wengine.
Amesema mabondia hao wanatakiwa kuingia kwenye levo ya kidunia kwanza ili wawe bora, lakini ushindani wa kitaifa pekee hautoshi kuwafanya kuwa bora.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Cheka alisema katika orodha ya mabondia wa sasa anamkubali Mwakinyo.
“Tena ni baada ya kuweka rekodi ya kuwa bondia namba moja Africa na wa 14 duniani alipomchapakwa TKO, Sam Eggington wa Uingereza mwaka 2018,” alisema bondia huyo na kuongeza.
“Ili bondia awe bora kwangu, kwanza ashinde ubingwa wa dunia, awe kwenye rekodi bora ya dunia na Afrika, lakini mabondia wengi wa sasa hawajafikia rekodi hiyo, Mwakinyo alipambana mwaka 2018, japo hana ubingwa wa dunia,” alisema.
Bondia huyo mwenye ndoto ya kurudi ulingoni baada ya kupotea tangu 2018 alipochapwa na Dullah Mbabe kwa Knock Out amesema bado ana amini ana kiwango bora.
Alisema uwezo wa kupigana anao na kiwango chake bado kipo na kuwahakikishia mashabiki wake ujio wake utakuwa kivingine.
Cheka, bingwa wa zamani wa dunia wa WBF ana rekodi ya kuwahi pia kutwaa mataji ya Afrika ya IBF, UBO na WBO aliyoyatetea zaidi ya mara moja.
IMEANDIKWA NA GLORIAN SULLE, SJMC