Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bulls yaweka rekodi, TDS mambo magumu Dar Youth League

DAR Pict
DAR Pict

Muktasari:

  • Michuano hiyo inayoendelea katika Viwanja vya Ufundi, Lugalo, inatarajiwa kuhitimisha hatua ya makundi wikiendi hii na baada ya hapo, timu mbili za juu kutoka kila kundi zitamenyana katika nusu fainali.

MASHINDANO ya vijana wenye umri chini ya miaka 18 ya Dar Youth League yameendelea tena wikiendi hii kwa raundi ya pili ya hatua ya makundi, huku Bulls Football Academy ikiwa ndiyo timu pekee iliyofanikiwa kujihakikishia kutinga nusu fainali, wakati nyingine zikisubiri mechi za mwisho kujua hatma zao.

Bulls, ambayo imetinga nusu fainali baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Magnet Academy na kupanda hadi nafasi ya kwanza katika Kundi B ikiwa na alama sita, ndiyo pekee iliyofanikiwa kushinda mechi mbili mfululizo za makundi katika ligi hiyo.

Katika mechi yake ya kwanza, Bulls iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Brothers Jr, na kabla ya mechi ya jana, ilikuwa ikilingana pointi na New Life iliyokuwa ikiongoza msimamo wa kundi lao.

DA 01

Akizungumzia ushindi huo wa pili mfululizo, Kocha wa Bulls, Fadhil Said, amesema kilichowabeba zaidi ni uzoefu waliokuwa nao katika michuano hiyo. Ameongeza kuwa sasa nguvu zao zote wamezielekeza katika mechi ya mwisho dhidi ya New Life, ambayo hadi sasa ina pointi nne.

"Tunajipanga kwa ajili ya mechi yetu ya mwisho, huku tukiendelea kufanyia kazi mapungufu tuliyoyaona katika mechi hizi mbili za makundi ili kuhakikisha hayajirudii tena kwenye mechi zijazo. Kuna wachezaji waliocheza mashindano ya U-15 ambao wengi wao tumewapa nafasi; hata katika mechi hii ya pili tumewaingiza takribani wachezaji sita tuliowapandisha kutoka timu hiyo," amesema Kocha Fadhil.

DA 02

Mbali na mechi hiyo iliyoiwezesha Bulls kusonga mbele, mchezo mwingine wa Kundi B uliopigwa jana ulikuwa kati ya New Life na Brothers Jr, ambao ulimalizika kwa sare ya 1-1. Matokeo hayo yaliiwezesha New Life kufikisha pointi nne na kukaa nafasi ya pili, lakini yalichochea zaidi vita ya kuitafuta timu moja ya kuungana na Bulls itakayopatikana katika mechi za mwisho.

Brothers Jr na New Life zote zinaweza kufuzu, ingawa Brothers Jr itahitaji matokeo ya ushindi pekee ili kufikisha pointi nne ilizonazo New Life kwa sasa, wakati New Life yenyewe itahitaji walau sare katika mechi yao ya mwisho dhidi ya Bulls ili kufuzu.

DA 03

Wakati huo huo, katika Kundi A, safari inaonekana kuwa bado mbichi na hakuna timu yoyote yenye uhakika wa kufuzu hadi sasa. Kundi hilo linaongozwa na TDS yenye pointi nne ilizofikisha baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Spotlight leo Jumapili katika mechi iliyokuwa na ushindani wa aina yake, huku TDS ikikosa mkwaju wa penalti iliyopata kipindi cha kwanza.

Nafasi ya pili ya kundi hilo inashikiliwa na West FA, ambayo pia ina pointi nne ilizofikisha baada ya kuichapa Kakakuona mabao 3-1 katika mechi ya mapema iliyopigwa leo kuanzia saa 8:00 mchana.

DA 04

Katika mechi za mwisho wikiendi ijayo ambazo zinatarajiwa kuamua timu zipi zitafuzu nusu fainali na zipi zitatolewa, TDS itaumana na West FA ambapo timu itakayoshinda itaingia nusu fainali ikiwa na alama saba. Vilevile, Spotlight itakuwa na kibarua mbele ya Kakakuona, ambayo imekuwa timu ya pili kuaga mashindano baada ya Magnet, zote zikiwa hazijapata pointi hata moja.

DA 05

Michuano hiyo inayoendelea katika Viwanja vya Ufundi, Lugalo, inatarajiwa kuhitimisha hatua ya makundi wikiendi hii na baada ya hapo, timu mbili za juu kutoka kila kundi zitamenyana katika nusu fainali.