Bongo Zozo: Mama yangu alitamani Samatta aje West Ham
Muktasari:
Kwa sasa, Bongo Zozo ambaye ameoa Mtanzania wa Iringa, ameteuliwa kuwa balozi wa utalii wa Tanzania. Mwanaspoti ambalo ndilo gazeti bora la Michezo Tanzania lilifanya naye mahojiano akafunguka mambo mbalimbali ikiwemo ushikaji wake na msemaji wa Simba, Haji Manara na vile alivyopata nafasi ya kutinga bungeni kwa mara ya kwanza.
ANAFAHAMIKA zaidi kama Bongo Zozo. Mzee wa fujo zisizoumiza. Jina lake halisi ni Nick Reynolds ‘Bongo Zozo’, mapenzi yake kwa Tanzania yamembusti sana katika miaka ya karibuni.
Amekuwa akiipeperusha bendera ya Tanzania kila aendako huku akiwashangaza wengi kutokana na uwezo wake wa kuzungumza Kiswahili.
Huyu jamaa ni Muingereza ambaye alizaliwa Zimbabwe na kukulia England ambako alipata elimu kuhusu Afrika, alivutiwa na lugha ya Kiswahili, alijifunza na kutua ukanda wa Afrika Mashariki mwishoni mwa miaka ya 1990 na kujikita katika biashara.
Watanzania wengi walimfahamu Bongo Zozo wakati wa Fainali za Mataifa ya Afrika ‘Afcon’ kule nchini Misri ambako Taifa Stars ilishiriki kwa mara ya pili na kuishia katika hatua ya makundi.
Kwa sasa, Bongo Zozo ambaye ameoa Mtanzania wa Iringa, ameteuliwa kuwa balozi wa utalii wa Tanzania. Mwanaspoti ambalo ndilo gazeti bora la Michezo Tanzania lilifanya naye mahojiano akafunguka mambo mbalimbali ikiwemo ushikaji wake na msemaji wa Simba, Haji Manara na vile alivyopata nafasi ya kutinga bungeni kwa mara ya kwanza.
USHIKAJI WAKE NA MANARA
Urafiki wake na Haji Manara ulianza wakati wa Afcon pindi walipokutana kwa mara ya kwanza nchini Misri.
“Jamaa ni mtu poa sana. Sikuwa najua kama ni mtu maarufu Tanzania hadi nilipotambulishwa, kuanzia hapo tukawa na ukaribu hata kama asingekuwa maarufu kama tungekutana mtaani naamini tungekuwa marafiki kwa sababu tunaendana.
“Napenda sana vile anavyojua kuzungumza, ana maneno mengi ya utani, tukikutana tumekuwa tukitaniana na kufurahi pamoja,” anasema Bongo Zozo ambaye ana wafuasi zaidi ya 200,800 kwenye mitandao ya kijamii.
ALIMTAKA SAMATTA NORWICH
Bongo Zozo anasema kuwa mama yake alikuwa na matarajio kuwa huenda straika wa Kitanzania, Mbwana Samatta atatua Norwich au West Ham United ambazo ziko karibu na nyumbani kwake, huko Uingereza.
“Unajua mama yangu anampenda sana Samatta, alipenda apate timu ya karibu na nyumbani ili akiwa na muda awe anakuja nyumbani kututembelea, lakini ilibidi akubaliane na uhalisia.Alilia kabisa yaani machozi yalimtoka,” anasema Bongo Zozo.
Anasema pamoja na mama yake kutofurahia, alikunjua nafsi na siku chache baadaye wakapigiwa simu na Samatta na kuongea naye mawili matatu kabla ya kucheza mchezo wake wa kwanza.
WAZUNGU WAPATA TABU
Baada ya kuongea na Samatta, Bongo Zozo aliweka mipango na kwenda kufanya ‘fujo zisizoumiza’ katika mchezo wake wa kwanza ambao ulikuwa wa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Ligi ‘Carabao’ dhidi ya Leicester City.
“Nilifanya ‘fujo’ na Watanzania wengine waliojitokeza kwa ajili ya kumsapoti Samatta, nilikuwa nikiwakera Wazungu wenzangu, walikuwa wakishangaa maneno ninayoyatoa mdomoni mwangu, niliwaleza kuhusu Tanzania wakabaji wanashangaa,” anasema huku akijinasibu kwamba ni shabiki wa Lipuli hapa nchini.
Katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu England, Samatta aliipachikia bao Aston Villa licha ya mchezo wake huo wa kwanza klabu yake kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Bournemouth ambao walimaliza pungufu kutokana na mchezaji wao mmoja kuonyeshwa kadi mbili za njano mbili kisha nyekundu ikafuata.
KUHUSU UBALOZI
Januari 31, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla aliposti ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram ulioonyesha kuwa Bongo Zozo ameteuliwa rasmi kuwa balozi wa utalii.
Ujumbe huo ulisomeka: “Umefika wakati sasa nitambue rasmi Fujo Isiyoumiza kama harakati serious ya kuitangaza Tanzania na Kiswahili chetu; kwanza kwa kumtangaza Bongo Zozo kama balozi wa hiari wa utalii wa Tanzania.
“Hivyo naelekeza Bodi ya Utalii Tanzania imuandikie rasmi barua ya kutambua mchango wake na kumtangaza kuwa balozi wa hiari wa utalii, pili kumuandalia safari ya kuja kutalii Tanzania.”
Bongo Zozo, anasema nafasi aliyopewa ilikuwa ni zaidi ya heshima kwake; “Nilifurahia sana na nitaitumia nafasi hiyo kuendelea kuitangaza Tanzania kila niendapo.
“Nilivyopata mwaliko wa kwenda bungeni nilimweleza mke wangu, ikabidi nianze kuhangaika kutafuta nguo za kuvaa maana sikuwa na nguo smati. Mke wangu alitaka nivae nguo za heshima, zikatafutwa na kupata. Nilikuwa mtulivu kwa sababu ile ni sehemu ya heshima, sikufanya fujo,” anasema Bongo Zozo ambaye siku hiyo alitinga kaundasuti ya kijivu mjengoni.
INSHU YA SUZY
Kuna kipindi fulani Bongo Zozo alikuwa akihusishwa katika mitandao wa kijamii kuwa na mahusinao ya kimapenzi na Suzan Bernard maarufu kama Suzy. Lakini anasema kwa kiasi kikubwa suala lile lilimharibia kwa mkewe.
“Alichukia sana na kibaya ni kwamba watu walikuwa wakimtumia meseji hadi mke wangu Mama Jesca, kiukweli Suzy ni rafiki yangu na tulikuwa karibu kwa lengo la kuwaburudisha tu watu, hapakuwa na lolote kati yetu,” anasema.
AZIPOTEZEA SIMBA NA YANGA
Kuhusu timu za Simba na Yanga, Zozo anasema : “Siku zote nimekuwa nikipenda timu ndogo, sijawahi kuvutiwa na klabu za Simba na Yanga kwa miaka yote ambayo nimekaa Tanzania, mbali na Taifa Stars ambayo naishabikia. Nitangaze kuwa shabiki wa Lipuli na ndio maana kwa England nilikuwa shabiki wa Norwich kwa sasa nimehamia Aston Villa.”