Biashara United yatinga Kimataifa
HABARI ndiyo hiyo kwa timu ya Biashara United ya mkoani Mara kujikatia tiketi ya kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na maafande wa Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliofanyika katika uwanja wa Nelson Mandela, Rukwa.
Katika mchezo huo uliokuwa wa vuta ni kuvute uliwachukua Biashara United kujipatia bao la uongozi kunako dakika ya 47 ya kipindi cha pili kupitia kwa mshambuliaji wake Mghana Christian Zigah, kabla ya Maafande wa Tanzania Prisons kujibu mapigo na kusawazisha bao hilo kupitia kwa Mohamed Mkopi dakika ya 56 ya mchezo.
Kwa matokeo hayo inawafanya timu hiyo kufikisha pointi 50 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yeyote iliyoko chini huku kila timu ikibakiwa na mchezo mmoja baada ya kucheza michezo 33.
Kwa upande wa Tanzania Prisons imejiwekea nafasi kubwa ya kuendelea kuwepo msimu ujao baada ya kufikisha pointi 43 ikiwa nafasi ya sita huku pia kila timu ikisaliwa na mechi moja kabla ya kufikia tamati kwa ligi kuu msimu huu Julai 18.
Katika mtanange mwingine uliopigwa katika uwanja wa Mabatini, Pwani ulishuhudia wenyeji wa mchezo huo Ruvu Shooting wakizima ndoto za timu ya Namungo FC za kushiriki Michuano ya Kimatifa msimu ujao baada ya kuichakaza kwa mabao 2-1.
Ruvu Shooting walikuwa wa kwanza kujiandikia bao la utangulizi dakika ya 26 ya kipindi cha kwanza kupitia kwa David Uromi huku Fully Zullu Maganga akiiandikia timu hiyo bao la pili kunako dakika ya 63 ya mchezo huku pia Namungo wakijipatia bao la kufutia machozi kupitia kwa Reliants Lusajo dakika ya 79.
Kwa matokeo hayo vijana wa Boniface Mkwasa Ruvu Shooting wamefikisha pointi 41 wakiwa katika nafasi ya 10 huku vijana wa Ruangwa ya mkoani Lindi Namungo wakiwa katika nafasi ya nane wakiwa na pointi 43 huku timu zote zikiwa zimecheza michezo 33 na kubakiwa na mchezo mmoja pekee.
Katika uwanja wa Mkwakwani huko Tanga Coastal Union ilifufua matumaini ya kusalia Ligi kuu msimu ujao baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya vibonde wa ligi Mwadui FC ambao walikwisha shuka daraja mapema mabao ya Abdul Hamisi Suleiman dakika ya 12, Issa Said akipachika bao la pili dakika ya 15, Raizin Hafidh dakika ya 65 na Said Masoud aliyepachika mabao mawili dakika ya 80 na 90 ya mchezo.
Matokeo haya yanawapa ahueni vijana wa kocha Juma Mgunda, Coastal Union ya kucheza mechi za mtoano 'Playoff' baada ya kufikisha alama 37 wakiwa nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi kuu Tanzania Bara baada ya kucheza mechi sita zilizopita mfululizo bila ya kupata ushindi wowote na kusubri hatma yao mechi ya mwisho Julai 18 dhidi ya Kagera Sugar.
Kwenye uwanja wa Jamhuri Mkoani Dodoma wenyeji Dodoma Jiji walishindwa kutumia vyema uwanja wao wa nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya 0-0 dhidi ya Mtibwa Sugar hivyo Dodoma Jiji kushika nafasi ya saba wakiwa na pointi 43 huku Mtibwa Sugar wakisalia nafasi ya 13 wakiwa na alama 39 na timu zote zikisaliwa na mchezo mmoja.
Huko uwanja wa Ushirika Mkoani Moshi Polisi Tanzania walikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Kagera Sugar kwa bao la Hassan Mwaterema dakika ya 46 na kuisaidia timu hiyo kufikisha alama 40 wakiwa nafasi ya 11, huku Polisi Tanzaia wakiendelea kushika nafasi ya tisa baada ya kufikisha alama 42, timu zote zikisaliwa na mechi moja.