Beki Simba Queens aanza kuona mwanga
Muktasari:
- Kutsanedzi raia wa Ghana, alijiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Epiphany Warriors ya nchini kwao na alifunga bao hilo katika mechi ya Agosti 5, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam wakati Simba Queens ikishinda 2-0, lingine lilifungwa na Elizabeth Wambui.
BEKI wa kushoto wa Simba Queens, Hellen Kutsanedzi amesema bao alilofunga katika mechi ya kirafiki dhidi ya Zesco Ndola Queens ya Zambia ni sehemu ya maandalizi kuelekea tamasha la Simba Day linakalofanyika leo Jumamosi, huku akibainisha, kikosi kizima kinaendelea kujenga morali kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa mashindano.
Kutsanedzi raia wa Ghana, alijiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Epiphany Warriors ya nchini kwao na alifunga bao hilo katika mechi ya Agosti 5, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam wakati Simba Queens ikishinda 2-0, lingine lilifungwa na Elizabeth Wambui.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kutsanedzi, ambaye pia ana uwezo wa kucheza nafasi ya winga wa kushoto, amesema ushindi na kiwango walichoonyesha katika mechi ya kirafiki vinawapa imani kubwa ya kufanya vizuri msimu ujao, hususan kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Kanda ya CECAFA.
“Bao nililofunga linaongeza kujiamini kwangu, lakini kikubwa zaidi ni kwamba linaonyesha maandalizi yetu yanaenda vizuri. Simba Day ni fursa ya kuwaonyesha mashabiki tulipojiandaa kabla ya kuanza kwa msimu mpya,” amesema Kutsanedzi.
Ameongeza, mechi za kirafiki zimekuwa na faida kubwa kwa wachezaji wote kwani zimewapa nafasi ya kuelewana zaidi ndani ya uwanja, kurekebisha makosa na kuongeza ushindani wa ndani ya kikosi.
“Kila mechi tunayocheza inatupa kitu kipya. Tunapata uzoefu, tunajenga maelewano na kuongeza utayari wa kukabiliana na changamoto za mashindano yajayo. Lengo letu ni kuanza msimu kwa nguvu na kufanya vizuri CECAFA pamoja na mashindano mengine,” amesema beki huyo.
Simba Queens imekuwa ikiendelea na maandalizi ya msimu mpya kutokana na mechi za kirafiki huku benchi la ufundi likiitumia kutathmini kiwango cha wachezaji wapya na wale waliosalia kikosini.
Kikosi hicho kinatarajia kutumia tamasha la Simba Day kama sehemu ya kuonyesha utayari wake mbele ya mashabiki kabla ya kuanza kwa ratiba rasmi ya msimu wa 2026-2027 ambalo Simba itaanza kwenye michuano ya kimataifa nchini Rwanda.