Beimbaya afichua jambo Kigamboni United
KOCHA Mkuu wa Kigamboni United zamani B19 FC, Twaha Beimbaya, amesema sababu zilizochangia kubakia ndani ya timu hiyo ni kutokana na mradi mzuri uliopo kwenye kikosi hicho, tofauti na angeenda sehemu nyingine kuanza kupata changamoto mpya.
Akizungumza na Mwanaspoti, Beimbaya amesema kabla ya msimu huu kuanza alikuwa na mazungumzo na timu mbalimbali zikiwemo za KMC FC na JKT Queens, japo baada ya kufikiria kwa kina aliamua kubaki Kigamboni United ili kuendeleza miradi iliyopo.
"Ni kweli nilikuwa katika hatua za mwisho za kujiunga na timu moja kati ya KMC FC au JKT Queens, ila nilifanya uamuzi wa kubakia kutokana na kuvutiwa na mradi uliopo Kigamboni United, lengo langu ni kuleta zaidi ushindani," amesema Beimbaya.
Kocha huyo aliyeifundisha Kiluvya United kwa sasa Barberian FC na Pan Africans, amesema kuaminiwa na uongozi wa kikosi hicho cha Kigamboni United kuendelea kukifundisha ni jambo muhimu kwake, licha ya ofa mbalimbali alizoendelea kuzipokea.
"Kwa akili yangu itaendelea kubakia Kigamboni United ili kuhakikisha ninatengeneza kikosi bora na cha ushindani, Ligi ya Championship ni ngumu kutokana na mahitaji ya kila mmoja wetu, ila tupo tayari kwa ajili ya changamoto hiyo mpya."