Baada ya kutua Libya, Girumugisha aitaja Yanga
Muktasari:
- Girumugisha amejiunga na Al Ahli Tripoli akitokea Al Hilal ya Omdurman ya Sudan, huku uhamisho huo ukihusisha mazungumzo ya moja kwa moja kati ya klabu hizo.
BAADA ya kutambulishwa kuwa mchezaji mpya wa Al Ahli Tripoli ya Libya, winga wa Burundi, Jean Claude Girumugisha, amesema bado hajafunga milango ya kucheza soka Tanzania huku akielezea namna dili lake la kutua Yanga lilivyokwama.
Girumugisha amejiunga na Al Ahli Tripoli akitokea Al Hilal ya Omdurman ya Sudan, huku uhamisho huo ukihusisha mazungumzo ya moja kwa moja kati ya klabu hizo.
Ripoti zinabainisha kwamba, Girumugisha amejiunga na timu hiyo kwa uhamisho wa dola 5.5 milioni (Sh14.6 milioni), huku kabla ya hapo, Yanga ilitajwa kumuhitaji.
Winga huyo aliyesaini miaka miwili kuitumikia Al Ahli Tripoli, amesema alifurahishwa na heshima aliyopewa na viongozi wa Yanga, hasa baada ya kukutana nao na kujadiliana kuhusu uwezekano wa kujiunga na timu hiyo.
“Ni kweli Yanga walinitaka na nilikuwa tayari kwenda. Nilifurahishwa sana na namna viongozi wao walivyoniheshimu na walivyokutana na mimi,” amesema Girumugisha.
Amesema kuwa, changamoto kubwa haikuwa upande wake, bali ilitokana na masuala ya kimkataba na maslahi yaliyokuwepo kati ya Yanga na Al Hilal, jambo lililofanya dili hilo lisikamilike.
“Tatizo lilikuja kwenye maslahi ya klabu kwa klabu. Kulikuwa na mambo ambayo yalihitaji makubaliano kati ya Al Hilal na Yanga, hivyo haikuwezekana kumaliza kila kitu,” amesema na kuongeza.
“Pengine baadaye nitakuja Tanzania, nilipenda mabosi wa Yanga walivyozungumza na mimi kwa heshima kubwa.”