Azam FC na mkakati wa Remontada
REMONTADA ni neno lenye asili ya kihispaniola lenye maana ya kupindua matokeo.
Neno hili lilianza kupata umaarufu mwaka 2017 lilipotumiwa na FC Barcelona kuelekea mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya 16 Bora ha ligi ya mabingwa dhidi ya PSG.
Barcelona walipoteza 4-0 kwenye mkondo wa kwanza, na baada ya mchezo, kocha Luis Enrique akiongea na waandishi wa habari akasema watafanya Remontada nyumbani...akimaanisha watapindua matokeo.
Na hapo ndipo neno Remontanda likaanza kupata umaarufu nje ya Hispania. Na kweli, kwenye mchezo wa mkondo wa pili, Barcelona ikashinda 6-1 na kupindua matokeo.
Mwaka 2020, kwenye toleo jipya la kamusi ya kifaransa, neno Remontanda liliwekwa kwa mara ya kwanza kama neno rasmi lenye maana ya kupindua matokeo.
Na mwaka 2022, Tanzania imelipokea kwa mara ya kwanza neno hili kama neno rasmi baada ya Azam FC kutangaza kulitumia kuelekea mchezo wa mkondo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Baada ya kipigo cha 3-0 ugenini dhidi ya Al Akhdar, Azam FC ikatangaza vita vya kupindua matokeo katika mchezo wa marudiano, wakitumia neno Remontanda...na hapo ndipo liliposhika kasi.
Mikakati ya kupindua matokeo ilianza kwa jaribio la kubadili muda wa mchezo kutoka saa moja usiku hadi saa tisa alasiri. Awali, kabla ya mchezo wa mkondo wa kwanza, Azam FC ilithibitisha kwa CAF kwamba mchezo huo utachezwa saa moja usiku. Lakini baada ya kupoteza mchezo wa mkondo wa kwanza, ikabadili mawazo na kutaka kuuhamisha na kuupeleka saa tisa, lakini CAF wakajibu kwamba muda ukishathibitishwa, haubadilishwi isipokuwa kwa makubaliano na mpinzani wako.
Hivyo Azam ikawasiliana na Al Akhdar kuwaeleza nia ya kubadili muda wa mchezo na sababu za nia hiyo.
Sababu zilikuwa hitilafu ya jenereta ya uwanjani kama chanzo cha umeme, ikizingatiwa Tanzania hakuna umeme wa uhakika hivyo yawezekana ukakatika na kuwa kiza endapo jenereta halitokuwepo.
Al Akhdar wakakataa wakisema hawajaridhika na sababu hizo hivyo muda uwe ule ule.
Wakasema muda wa marekebisho upo kwani mechi iko wiki moja mbele.
Baada ya jaribio hilo kukwama, Azam ikarudi kwa wenye timu yaani mashabiki.
Ikatangaza kwamba kiingilio katika mchezo huo kitakuwa jezi tu ya Azam.
Yaani mtu akiwa na jezi ya Azam ya msimu wowote, ataingia bure.
Lengo ni kuufanya uwanja uwe Azam tupu hivyo kuongeza hamasa kwa wachezaji.
Luis Enrique alipokuwa akitangaza Remontada baada ya kipigo cha 4-0 kutoka PSG, aliweka imani yake kwa mashabiki.
“Tukifunga bao la kwanza, la pili litafungwa na Camp Nou na la tatu litajifunga lenyewe.”
Hiki ndicho Azam inakitafuta kutoka kwa mashabiki wake. Endapo watajaa wakiwa na jezi za Azam huku wakishangilia kwa nguvu, kazi itabaki kutafuta bao la kwanza tu. Mabao mengine yatafungwa na mashabiki na mengine yatajifunga yenyewe.
Hayo ni ya nje ya uwanja. Ndani ya uwanja, kocha mkuu Denis Lavagne anaendelea na mipango yake kwenye uwanja wa mazoezi kwa kuimarisha mbinu na maarifa.
Daniel Amoah na Malickou Ndoye hawakucheza kwa sababu walikuwa majeruhi.
Aggrey Morris na Abdallah Kheri ‘Sebo’ hawakusafiri na timu kutokana na majeraha (Agrey) na Malaria (Sebo).
Kocha Mkuu Denis Lavagne akawa hana namna zaidi ya kuwatumia Edward Charles Manyama na Lusajo Mwaikenda kama mabeki wa kati.
Wawili katika nyakati tofauti walishawahi kucheza kwenye nafasi hiyo lakini hawakuwahi kucheza pamoja, hivyo hawakuwa na maelewano. Pia alikosekana Sospeter Bajana katika kiungo.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa na klabu, tarehe 13, ni kwamba ni Bajana pekee kati yao ambaye hajaanza mazoezi...wengine wote wameshaanza.
Hii ina maana kwamba watakuwepo kwenye mchezo wa marudiano, tarehe 16.
Azam inaweza kuandika historia kubwa kwamba imeshawahi kupindua matokeo katika wakati ambao wengi walishakata tamaa.