Arajiga kapewa kipyenga Star Sport Academy v Berkane CAFCL
Muktasari:
- Arajiga atakuwa mwamuzi wa kati katika mchezo huo wa hatua ya pili ya mchujo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akiongoza kikosi cha waamuzi kutoka Tanzania.
Mwamuzi wa kimataifa wa Tanzania, Ahmed Arajiga, amepewa jukumu la kuongoza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Star Sport Academy ya Sierra Leone na RS Berkane ya Morocco utakaochezwa Oktoba 17.
Arajiga atakuwa mwamuzi wa kati katika mchezo huo wa hatua ya pili ya mchujo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akiongoza kikosi cha waamuzi kutoka Tanzania.
Waamuzi wasaidizi watakuwa Hamdani Said Ally na Ally Ramadhani, wakati Nasir Siyah atakuwa mwamuzi wa nne.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa nchini Liberia, katika Uwanja wa Samuel Kanyon Doe, baada ya Star Sport Academy kushindwa kutumia uwanja wake wa nyumbani kutokana na kutokidhi vigezo vya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Uteuzi huo unaongeza nafasi ya Arajiga kuendelea kupata uzoefu katika mechi za mashindano ya kimataifa yanayosimamiwa na CAF.
Kwa upande wa RS Berkane, timu hiyo ya Morocco ni miongoni mwa klabu zinazoshiriki mara kwa mara mashindano ya CAF na itakuwa na jukumu la kutafuta matokeo mazuri katika mchezo huo.
Star Sport Academy, yenye makao yake Sierra Leone, itakabiliana na miongoni mwa timu zenye uzoefu mkubwa katika mashindano ya klabu barani Afrika.
Mchezo huo utakuwa muhimu kwa timu hizo katika harakati za kutafuta nafasi ya kusonga mbele katika Ligi ya Mabingwa Afrika.